loader
Maajabu magofu ya urithi wa dunia Kilwa Kisiwani

Maajabu magofu ya urithi wa dunia Kilwa Kisiwani

UTALII wa vivutio vya malikale, fukwe, magofu na viumbe vya chini ya bahari ni eneo linaloanza kupata umaarufu mkubwa duniani kutokana na idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje kuvutiwa navyo.

Eneo mojawapo linalosifika kwa maajabu hayo ni pamoja na Mji Mkongwe wa Kilwa Kisiwani.

Licha ya utalii unaofahamika kwa miaka mingi kuwa ni wa kutembelea hifadhi za taifa na wanyamapori, miaka ya hivi karibuni sehemu ambayo yenye kuvutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchi ni utalii wa malikale, fukwe, magofu na viumbe vya chini ya bahari.

Mji Mkongwe wa Kilwa Kisiwani ni moja ya maeneo yenye vivutio vya malikale na upo katika orodha ya urithi wa utamaduni wa dunia. Vivutio hivyo vinasimamiwa chini ya Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Majengo ya zamani na mabaki ya kiikolojia yanayopatikana Kilwa Kisiwani na Kisiwa cha Songo Mnara yanaelezea maendeleo ya kijamii, kibiashara na kiutamaduni ya watu wa Pwani ya Afrika Mashariki kati ya karne ya tisa na 19 baada ya Kristo.

Magofu na mabaki haya ni ushahidi na uthibitisho wa kipekee wa umuhimu wa utamaduni wa Kiswahili na misikiti ya zamani iliyoko katika eneo hilo inaonesha ukongwe na kushamiri kwa dini ya Kiislamu tangu karne ya 11.

Masalia haya pamoja na meli za zamani zilizozama katika Pwani ya Kilwa ni ushahidi wa maendeleo ya kibiashara kati ya Kilwa na miji mingine kati ya karne ya 11 na 16.

Uwepo wa malikale nyingi, zikiwemo vigae vya zamani, sarafu ya kale ya Kilwa na shanga kutoka maeneo mbalimbali duniani vinaonesha umaarufu na ustawi wa mji mkongwe wa Kilwa Kisiwani.

Magofu hayo ni kati ya vivutio vilivyokuwa chini ya usimamizi wa Idara ya Malikale ambavyo Wizara ya Maliasili na Utalii ilikasimisha kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Kutokana na umuhimu wa mji mkongwe Kilwa Kisiwani, jitihada zilifanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kufanya utafiti na kuanzisha makumbusho maalumu ambayo baadaye ilikabidhiwa kwa TAWA.

Makumbusho ya Kilwa Kisiwani yameanzishwa kwa kushirikiana na wataalamu wa mambo ya kale waliofanya utafiti kuhusu kisiwa hicho na hivyo kupata historia ya zaidi ya miaka 1,000 kuhusu mji mkongwe wa Kilwa Kisiwani.

Uwekaji wa makumbusho katika mji mkongwe wa Kilwa Kisiwani ni mwendelezo wa jitihada zilizoanza zaidi ya miaka 600 iliyopita ambapo wenyeji wa Kilwa Kisiwani walifanya jitihada kutunza na kuhifadhi historia ya mji wao.

Mhifadhi wa Wanyamapori na Malikale kutoka Tawa, Samson Gisiri, anasema jitihada za kuhifadhi na kutunza urithi wa Kilwa ziliongezeka na hasa kuanzia miaka ya 1900.

Gisiri anatolea mfano mwaka 1902, aliyekuwa msimamizi wa eneo la Kilwa alimwandikia barua aliyekuwa mkuu wa jimbo la Lindi-Mtwara akimwelezea umuhimu wa kuhifadhi urithi wa utamaduni wa Kilwa Kisiwani.

Anataja baadhi ya vioneshwa (Archeological findings) vilivyohifadhiwa kwenye makumbusho hiyo ya kihistoria ya mji mkongwe Kilwa Kisiwani ni pamoja na Ndatu.

Gisiri anasema, Ndatu ni kandambili za asili ya watu wa Kilwa Kisiwani zilizotengenezwa na minyaa ambazo zilitumiwa na wavuvi ili kukinga miguu yao isikatwe na mawe makali ya Pwani.

Baadhi ya vioneshwa vingine ni Dema ambao ni mtego wa samaki wa asili unaotumiwa na wavuvi kwenye kina kirefu cha maji.

Katika makumbusho hayo pia kuna Nanga iliyotengenezwa kwa jiwe lenye urefu wa mita 1.2 na upana mita 0.35 na inasadikika ilitengenezwa India au nchi nyingine ya Uarabuni.

Anaeleza kuwa Nanga inayofanana na hiyo imepatikana katika Pwani ya mji wa Sirafu, Mashariki ya Kati ikikadiriwa kuwa ni ya karne ya 11.

Kupatikana kwa Nanga hii Kilwa Kisiwani kunaonesha kushamiri kwa uhusiano wa kibiashara kati ya wakazi wa Kilwa Kisiwani na mataifa mengine.

Gisiri anasema jitihada zinazofanywa na Tawa kutangaza malikale katika Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara zinaendelea kuleta tija.

Anasema mamlaka hiyo imeanza kujenga sehemu maalumu ya mapokezi na malazi kwa ajili ya watalii wanaotembelea mji mkongwe wa Kilwa Kisiwani ili kuwafanya wafurahie muda wao ndani ya visiwa hivyo.

“Utalii wa majini ni kivituo kikubwa cha watalii hapa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, watalii wanaweza kuona chini ya bahari matumbawe na viumbe vingine kupitia boti ya kisasa iliyonunuliwa na Tawa,” anasema Gisiri.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainabu Kawawa anasema ujio wa watalii 120 kutoka mataifa mbalim-bali duniani yakiwemo ya Marekani, Japan, Uingereza, Ujerumani na Uswisi waliowasili mwishoni wa Desemba mwaka jana (2021) na meli ya kisasa ya Le Bellot ni ishara nzuri ya kuifungua Kilwa kiuchumi.

Zainabu anaeleza kuwa kundi la watalii hao waliwasili mwishoni wa Desemba mwaka jana (2021) na kuutembelea mji huo mkongwe wa Kilwa Kisiwani kwa ajili ya kujionea magofu ya urithi wa dunia.

Anasema uamuzi uliochukuliwa na mamlaka hiyo kufungua milango kwa kutangaza vivutio vinavyopatikana wilayani Kilwa hasa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ni sehemu ya fursa kwa wananchi kuanza kuwekeza kwenye sekta ya utalii.

“Hii ni fursa iliyojitokeza wilayani kwetu ni vyema wananchi sasa wajitokeze kuwekeza kwenye ardhi zao kujenga hoteli za kitalii, nyumba za kisasa za kulala wageni ili kukidhi mahitaji ya watalii siku za usoni,” anasema Zainabu.

Zainabu anasema magofu ya Kilwa yanayosimamiwa na mamlaka hiyo yameendelea kuipa heshima Wilaya ya Kilwa na taifa ambayo kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu imewasili eneo hilo meli yenye kuwaleta watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu (Desemba 26, 2021) tumepokea tena meli ya kitalii iliyowaleta watalii 120 kutembelea magofu haya, ambayo ni urithi wa dunia na wameshangazwa na upekee wa kisiwa hiki na vivutio vilivyomo,” anasema Zainabu.

Zainabu anasema, ujio wa wageni hao ni matunda ya uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza vivutio vya utalii vya hapa nchini, kupitia filamu inayotarajiwa kuzinduliwa mwaka huu (2022) ya “Tanzania Royal Tour”.

Katika kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii na uvuvi anasema Rais Samia ameidhinisha fedha kiasi cha Sh milioni 50 kwa ajili ya kujenga bandari ya uvuvi wilayani humo ikiwa ni hatua ya kukuza ajira kwa wananchi.

Zainabu anasema kutakuwepo na kiwanda cha kuchakata samaki, wavuvi kuleta shehena ya samaki ambao hawapatikani nchi za Ulaya kwa ajili ya kuwauzia watalii.

“Katika jambo hili Kilwa tunatarajia kuwa na mapinduzi ya kiuchumi katika sekta ya uvuvi na sekta ya utalii kupitia bahari yetu kwa maana uchumi wa buluu kama ambavyo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilivyoelekeza,” anasema Zainabu.

Hivyo anawahimiza vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili kupata mikopo inayotolewa na halmashauri ya asilimia 10 (4 vijana, 4 wanawake na 2 walemavu) kwa ajili kuboresha shughuli zao za kiutalii kuuza katika sekta ya uvuvi. “Lengo la mikopo hii ni kuona namna vijana wanavyoweza kujiandaa kununua zana bora na za kisasa za kuvulia samaki wanaohitajika, walio bora na ukubwa kwa ajili ya kuwauzia watalii,” anasema Zainabu.

Ofisa Utalii Mwandamizi wa Tawa, Steven Madenge anasema Tawa imefarijika kwa ujio wa watalii katika Wilaya ya Kilwa hasa mji mkongwe wa Kilwa Kisiwani na kuishukuru serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuratibu kikamilifu masuala yote yanayohusiana na utalii na uhifadhi nchini.

Nao baadhi ya wananchi wa Kilwa Kisiwani kwa nyakati tofauti wanasema hivi sasa watakuwa na fursa mpya za ajira katika utalii jambo ambalo litasaidia kuacha kutegemea uvuvi na kilimo pekee katika kuendesha maisha yao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/872b97c58e03209b92628200cbb6654b.png

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi