loader
Wamanyema na utamaduni wa kusafiri na ugali kwenye begi

Wamanyema na utamaduni wa kusafiri na ugali kwenye begi

UTAMADUNI ni jumla ya mila, desturi na mitindo ya maisha ya watu wa jamii fulani.

Utamaduni unaangalia namna watu wanavyofanya mambo yao kwa kawaida kama vile; wakati gani au nini wanakula, mavazi yao, wanasalimiana vipi, mambo ambayo ni adabu, miiko yao, mambo wanayoamini na mengineyo.

Mambo ambayo yanaweza kuutambulisha utamaduni wa watu wa jamii fulani ni mengi na anuwai, kujaribu kuyazungumzia yote kwa kina na mapana yake katika makala fupi kama hii inaweza kuwa ni kazi isiyo na tija.

Katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Wamanyema.

Wamanyema (una-ma-nyema, yaani wala-samaki), ni shirikisho la makabila yapatayo 12 ya Kibantu (wakati mwingine husemwa kuwa ni makabila 18) yanayopatikana Kusini Mashariki mwa beseni la Mto Kongo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na katika Mkoa wa Kigoma nchini Tanzania.

Baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1930 ndipo walipoungana kuwa wote Wamanyema hasa kupitia vyama vya kijamii vya Manyema Association (Ujiji) na Manyema Union (Zanzibar).

Kilichowaunganisha wote, mbali na kuwa wakati huo tamaduni zao hazikuingiliana sana, ilikuwa ni dini ya Kiislamu na ndiyo maana viongozi wa vyama vyao pia walikuwa ni viongozi wa kidini (mashehe) na walisherehesha katika shughuli za kidini ambazo ndizo zilikuwa zikiwakusanya wote hususani swala za Idi, Maulidi na khitma za mazishi na kufturu funga ya Ramadhani.

Hivyo ukipitia historia kwa kina ni ukweli usiofichika kuwa utambulisho wa Kimanyema umebebwa kwa asilimia kubwa sana na dini ya Kiislamu kuliko hata uenyeji wa Ujiji, asili ya Mashariki ya DRC n.k.

Kwa hali hiyo wanahistoria wanakubali kwa kiasi kikubwa kuwa Wamanyema ni “ethno-religious group” yaani jamii iliyounganishwa kidini kuliko kuwa jamii iliyounganishwa kitamaduni, hasa kutokana na sababu za uzamani wa sasa wa historia yake na kila kabila kushikilia utambulisho wake, kama ilivyo kwa Wabembe.

Historia ya Wamanyema

Wamanyema hapo zamani hawakuitwa wote Wamanyema bali mbali na kuwa wana makabila yao pia walikuwa jamii mbili za Waarabu-Congo na Watanganyika, miji yao mikuu ikiwa ni Machazo na Gungu yote kama sehemu ya Ujiji.

Kwa Tanzania, Wamanyema wanajumuisha makabila ya Wagoma, Wabwari, Wamasanze, Wabembe, Wahorohoro, Wabangubangu, Wakusu, Wakwalumona (Wanyakaramba) n.k ambao wote hujiita Wamanyema.

Yapo baadhi ya makabila yaliyoamua kuendeleza tamaduni, mila na lugha zao na sasa makabila hayo hayahesabiwi kama ni Wamanyema kwa sababu wao walijiweka mbali kwenye huo mjumuiko.

Kwa sehemu kubwa ya karne ya 19, Wamanyema waliwindwa sana na Waarabu waliofanya biashara ya watumwa.

Wamanyema walipofika Kigoma kuna ambao walipata majina katika miji kama Katonga, Kabwe, Mkabogo au Kabogo; hao wote walikuwa Wamanyema wenye asili ya DRC.

Wakati huo walikuwa wameshajipa jina la Waswahili na Uarabu, hii ni kwa sababu walipofika Tanganyika hawakuendeleza mila zao kama walivyokuwa Congo.

Jambo hilo ndilo limewafanya Wamanyema wafahamike sana kwenye Bara la Afrika kwa kujikita na kuwa kivutio kwa sababu ya wao kuongea Kiswahili na kujiita Waswahili.

Na Wamanyema waliokuwa Tanga hasa Wagoma walibadili jina lao na kuliweka katika lugha ya Kiarabu, yaani ‘Al-ghamawiyy’ kama walivyofanya Wagoma waliokuwa Kigoma ambako kuna msikiti unaitwa Msikiti wa Wagoma. Na pia Dar es Salaam kuna Msikiti wa Manyema.

Kwa ajili hiyo Wamanyema hutaniwa na pia wanafahamika na wenyeji wao Waha kama Waswahili.

Hapo Ujiji waliendeleza Uislamu kama walivyokuwa huko DRC na walitokomeza mila zao moja kwa moja na wakawa Waislamu kweli kweli.

Walianzisha shule za Kiislamu (Madrasa) na kipindi cha ukoloni wa Waingereza Wamanyema hawakuwapeleka watoto wao kwenye shule za misheni wakihofia watoto wao wangeweza kubatizwa au kutumia nyama ya nguruwe. Hata hivyo, baadhi yao waliwapeleka watoto wao na baadaye wakaja kuwa wanasiasa wakubwa nchini.

Wamanyema wanajulikana kama watu wenye harara (hasira za haraka) na ushujaa. Mmanyema anaweza kuulipia fedha ugomvi ili na yeye awemo na kadri mpinzani anavyokuwa na nguvu na hodari, ndivyo Mmanyema anavyofaidi ugomvi wake.

Hawaogopi ugomvi hasa pale anapoona haki imepindishwa na hii ndiyo ilikuwa sababu ya wao kuwa mstari wa mbele kuipinga serikali ya kikoloni Tanganyika.

Sababu ya wao kuwa watumwa ni miili yao kuwa na nguvu na ujuzi wa kazi mbalimbali na wanawake wao walikuwa ni wazuri na ndio wengi waliolewa na Waarabu na pia Wazaramo.

Katika siku hizo Wamanyema walikuwa wameshikwa katika magomvi. Katika mwaka 1941 ilibidi serikali ya kikoloni, Maimamu na Mashehe wa misikiti mingine mjini Dar es Salaam kuingilia kati ili kuamua ugomvi uliowakumba Wamanyema kuhusu msikiti wa Manyema uliopo Kariakoo, Dar es Salaam.

Wamanyema hawakumstahi mtu yeyote pale wanapoona mambo ya ubatilifu (si waoga), waligombana na mtu yeyote yule bila kujali ni nani ilimradi kafanya jambo lisilopendeza.

Katika Umanyema si ajabu mtu wa kabila mojawapo ambalo Ujiji huitwa Mmanyema akawa si Mmanyema ikiwa ni Mkongomani au akiwa si Muislamu na hii hujitokeza hususani katika migongano ya Wagoma na Wabembe.

Mmanyema hayupo mbali sana na utamaduni wa Kiislamu. Wamanyema, Warufiji na Wadigo ni katika makabila ambayo ni tabu kumpata Mkristo.

Baadhi ya Wamanyema maarufu ni pamoja na Shehe Amri Abed Kaluta, aliyekuwa mpigania uhuru kutoka kabila la Wagoma; Dk Walid Aman Kaburu (alikuwa mwanasiasa mkongwe kutoka kabila la Wabwari); Shehe Yahya Hussein (alikuwa mnajimu na mtabiri maarufu kutoka kabila la Wabwari); Shehe Issa Ponda (mwanaharakati wa Kiislamu kutoka kabila la Wabwari).

Utani kati ya Wamanyema na Waha

Inafahamika kuwa Waha ni moja ya makabila kutoka Wabantu wa Mashariki. Wabantu hao walipata kufika maeneo hayo hata kabla ya miaka ya 600 yaani kabla ya Wamanyema.

Waha waliwapokea watani wao Wamanyema na kuanza kuishi pamoja mpaka sasa. Hivyo Wamanyema na Waha ndio wenyeji wa Kigoma.

Uenyeji huu tunaouzungumza ni miaka ya zamani sana, hata kabla ya kuanza kwa ukoloni hawa watu tayari walikuwa wakiishi pamoja na walikuwa wakipendana na kuthaminiana.

Kuna vitu Waha waliwafundisha Wamanyema na pia kuna vitu Wamanyema waliwafundisha Waha na wote hawa waliipigania Tanganyika kutoka mikononi mwa serikali ya kikoloni.

Hata mradi wa kuligawa Bara la Afrika kati ya nchi kadhaa za Ulaya ulikuwa bado kabisa Wamanyema na Waha walikuwa wakiishi pamoja.

Kupiga chuku “kilumiko”

Hii ni tiba ya kale sana ya kabila la Goma na makabila mengine ya Kimanyema.

Ilifanywa na mababu toka enzi na enzi kabla hata ya mwingiliano na wageni, tena tofauti na ilivyofanywa na wageni hasa Waarabu, Wazungu na Wahindi ambao hutumia kikombe cha kioo kisicho na mkono na mwale wa moto au “vacuum tube”.

Wagoma walitumia kikonyo cha kibuyu kilichotobolewa mdomoni kwa ajili ya kuvutia damu kutoka katika sehemu ya mwili yenye maradhi.

Tiba hii kwa sasa inatumika duniani kote hasa China na India ambako ndiko chimbuko la udaktari wa kisasa.

Chakula cha asili cha Wamanyema

Chakula cha asili cha Wamanyema (na Waha) ni ugali wa rowe ambao unatokana na muhogo.

Baada ya kupikwa ugali huu unahifadhiwa kwenye majani maalumu ya mgomba na unaliwa kwa mboga ama bila mboga, pia unaweza kusafiri nao popote kwenye begi.

Ugali huu hauwezi kuharibika hata ukikaa mwezi mzima, ni ugali unaotengenezwa kutokana na muhogo na masharti yake ni kwamba usihifadhiwe kwenye jokofu ama sahani. Ugali huu huandaliwa kwa siku nne mpaka saba.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@ gmail.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/acdd863a95075a6bb34f7aa9e11495c3.png

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi