loader
Nguvu zaidi inahitajika kukomesha ukatili dhidi ya watoto

Nguvu zaidi inahitajika kukomesha ukatili dhidi ya watoto

UKATILI dhidi ya watoto umekuwa ukishika kasi nyakati hizi licha ya juhudi nyingi zinazofanywa na watetezi wa masuala ya haki za watoto na serikali katika kudhibiti uovu huo lakini bado vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika kwa wingi.

Kumekuwa na matukio mengi ambayo yametokea na kuleta taswira tofauti kwa namna ambavyo mtoto amekuwa akichukuliwa katika jamii.

Mfano wa matukio hayo ni pamoja na la Desemba 2, 2021 ambapo mwanamke kutokea Geita aliyefahamika kwa jina la Veronica Gabriel aliwanywesha sumu watoto wake watano kisha na yeye mwenyewe kunywa sumu kwa madai ya ugumu wa maisha.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Polisi nchini, kuna ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto.

Katika mwaka 2020 matukio 7,388 yaliripotiwa nchini ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo matukio 5,803 yaliripotiwa.

Matukio kama haya wamefanyiwa watoto na watu wao wa karibu kabisa kama vile wazazi, walezi na ndugu wa karibu na watoto hao. Mwishoni mwa mwaka 2021 matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa kwa wingi huku Kanda ya Ziwa ikitajwa kuongoza.

Kumekuwa na sababu nyingi zinazoelezwa kuwa ndio chanzo cha ukatili dhidi ya watoto nchini, miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na imani za kishirikina.

Watu wengi wanaofanya ukatili dhidi ya watoto huwa na imani kuwa utajiri hupatikana kwa kushiriki au kufanya vitendo viovu na hii ndio husababisha kuwaweka watoto wengi kwenye hatari zaidi ya kukutana na ukatili.

Hasssan Abdallah (28) mkazi wa Morogoro, anasema ukatili dhidi ya watoto umekuwa mwingi katika maeneo yao kwa sababu wakazi wengi wa maeneo hayo wamekuwa wakipenda kuamini waganga wa kienyeji wanaowatuma kufanya vitendo hivyo na kusababisha ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto.

Ugumu wa maisha pia unatajwa kuwa sababu ya ukatili dhidi ya watoto. Mara nyingi uhusiano wake huwa ni pale wazazi wanaposhindwa kubeba majukumu ya kulea watoto hivyo kuwatupa watoto wakiwa wachanga kabisa.

Tukio kama hili lilitokea Machi 5 mwaka jana, Zanzibar baada ya mzazi kuamua kumtupa mtoto wake sehemu ya kutupia taka. Tanzania Bara matukio kama haya yameripotiwa mengi huku baadhi ya watu wakiwatupa watoto katika mashimo ya vyoo.

Sababu nyingine ni uelewa mdogo wa wazazi hasa katika upande wa malezi kwa watoto. Wazazi wengi wamekuwa wakilea watoto kinyume na malezi mema. Hii husababisha watoto kufanyishwa kazi katika umri mdogo sababu wazazi wameshindwa kusimamia majukumu yao katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira sahihi.

Katika nyakati hizi ambazo wazazi wamekuwa na majukumu mengi ya kikazi ufuatiliaji wa watoto wameachiwa zaidi wasaidizi wa ndani (house girl) ambao ni ngumu kuthibitisha kuwa mtoto anapata malezi yalio bora.

Mwanaharakati wa haki za 

watoto, Issa Baruti anasema: “Mtoto anamuhitaji zaidi mzazi kuliko dada wa kazi, kwa bahati mbaya siku hizi dada wa kazi ndie anamjua mtoto zaidi kuliko mzazi aliyemzaa.”

Hii inaonesha ni kwa namna gani wazazi wengi wamekuwa wakikimbia na kusahau majukumu ya kuwalea watoto wao na matokeo yake vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wadada wa kazi vinaongezeka japo si wote wanaofanya hivyo.

Katika kupigania na kulinda haki za watoto kumekuwepo na juhudi zinazofanywa na serikali ikishirikiana na mashirika binafsi katika kuhakikisha mtoto anakuwa salama. Zimekuwepo kampeni mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendeshwa na mashirika ya kupigania haki za watoto kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kuhakikisha wanadhibiti ukatili dhidi ya mtoto.

Lakini pia utafiti uliofanywa na taasisi inayohusika na masuala ya watoto iitwayo DSW yenye ofiis zake mkoani Arusha, katika baadhi ya kata mkoani humo ulibaini kuwa kuna ukatili unaoendelea kwa mabinti kukeketwa

na ndoa za utotoni hivyo katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16 mwaka 2021, ilifanyika sambamba na kampeni ya “Binti na Maendeleo” itakayomjengea uwezo binti kutambua haki zake.

Kampeni kama hizi ni muhimu sababu zitaongeza ufahamu na utambuzi kwa watoto na jamii kwa ujumla hivyo kujua ni hatua gani za kuchukua kujikinga dhidi ya vitendo hivi visivyofaa.

Pia ni wito kwa wazazi na walezi kubadilisha mtazamo na kumlinda mtoto sababu ndiye rais wa kesho, au kiongozi yeyote mkubwa wa jamii hivyo ni wajibu kwa kila mlezi kuhakikisha watoto wote wanapata elimu sawa na si kubagua mtoto wa kiume aende shule na wa kike akaolewe.

Mtoto ana haki zote za kwenda shule awe wa kiume au wa kike haitakiwi mtoto kunyimwa haki zake za msingi kutokana na jinsi yake.

Ikiwa mtoto anaathirika zaidi na mazingira au yale anayoyaona katika jamii yake au watu wanaomzunguka basi ni wajibu wa

kila mzazi, mlezi na mwananchi yeyote kuhakikisha wanakuwa walinzi wa watoto hawa na wasifanye vitu visivyofaa mbele ya watoto kama ambavyo tunaona kuna ukatili mwingine husababishwa na watoto wenyewe dhidi ya watoto wenzao.

Lakini ni wajibu kwa vyombo vya habari kukemea kwa nguvu ukatili unaofanywa dhidi ya watoto. Kama chombo cha habari ni muhimu kupaza sauti kwa matatizo yote yanayotokea katika jamii hivyo ni wajibu wa kila gazeti, radio na televisheni zote kupiga vita ukatili dhidi ya watoto na kutokomeza sababu watoto ndio taifa la kesho.

Aidha, ni wajibu wa serikali kuhakikisha inatetea haki za watoto kwa kuweka sera, kanuni na sheria kali na kuchukua hatua na kutoa hukumu kali kwa wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/51e0f0b399dd0400de7fbbb6f0da5787.jpeg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Ally Mfaume

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi