loader
Wazee wanaposahaulika dunia inazeeka kwa kasi

Wazee wanaposahaulika dunia inazeeka kwa kasi

T

AKRIBANI watu wanaokaribia bilioni moja kwa sasa wamefikia umri wa miaka 60, na ifikapo mwaka 2050 watu bilioni mbili ambayo ni zaidi ya asilimia 20 ya idadi ya watu duniani watafikisha umri wa miaka 60 au zaidi.

Pamoja na ukweli huo miaka 41 tangu kutangazwa kwa Azimio la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1991, bado kuna shida kubwa kuhusiana na haki za wazee.

Imeelezwa kuwa mtu mmoja kati ya watu sita walio na umri wa miaka 60 na zaidi amejikuta katika changamoto kubwa na kuishi maisha yasiyokuwa na amani.

Katika tafiti mbalimbali zilizotolewa na taasisi za kimataifa, wafanyakazi wawili kati ya watatu wanaohudumia wazee katika makazi yao wamekiri kuhusika kuwanyanyasa wazee hao.

Kutokana na shida hizo Shirika la Afya Duniani (WHO) linapigana vita kutaka wazee kuendelea kuzeeka kistaarabu kwa amani na kushiriki uchumi na kuwa kuwanyanyasa kunawasababishia ulemavu na pia tatizo la kisaikolojia na kufa mapema.

Takwimu za WHO zinasema ni asilimia nne tu ya wazee wanaonyanyaswa taarifa zao zinafika katika maeneo husika kama polisi na mahakamani.

Kuna changamoto kubwa jinsi umri wa binadamu 

unavyoendelea kukua. Mathalani wale wenye miaka 80 hujikuta na matatizo ya kumbukumbu, afya ya akili na pengine hata uwezo wa mwili ukilinganisha na vijana wa miaka 20.

Ili kuwasaidia wazee ni lazima kuwa na sera na sheria ya kuwalinda ili waweze kuishi kwa amani ikiwemo kuwapatia ruzuku

kwa kutambua mchango wao walioutoa kwa nchi walipokuwa na umri wa kufanya kazi.

Utafiti wa WHO uliofanyika nchini Uingereza na Ireland ya Kaskazini mwaka 2011 unaonesha kuwa mchango wa wazee kupitia kodi, matumizi yao na masuala mengine yanayohusu fedha ni zaidi ya Paundi za

Uingereza bilioni 40 kuliko mapato yanayotolewa kwa ajili yao katika mfumo wa pensheni, afya na ustawi ukichanganya pamoja. Inakadiriwa kwamba fedha kutoka kwa wazee ifikapo mwaka 2030 katika nchi hizo zitakuwa ni Paundi bilioni 77.

Pamoja na hayo tafiti zinaonesha kuwa nchi za

uchumi wa kati na wa chini mchango wa wazee yaani kuanzia miaka 60 kuendelea ni mkubwa. Nchini Kenya, kwa mfano, wazee ni asilimia 60 ya wakulima wadogo ambao ndio msingi wa usalama wa chakula nchini humo.

WHO inasema kwamba dunia inazeeka kwa kasi zaidi kuliko inavyofikiriwa

kutokana na kuendelea kukua kwa kundi la wazee na hivyo ni vyema kuangalia kila eneo ili kuhakikisha katika maendeleo ya dunia wazee hawaachwi nyuma.

Janga lililoibuka sasa hivi duniani la Covid-19 limeonesha mapengo makubwa katika sera, mifumo na huduma na hivyo mpango mkakati wa miaka 10 wa WHO umelenga kushawishi nchi kutekeleza mipango ya kusaidia wazee kwa kuangalia athari zilizopo sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom akizungumzia mpango huo wa miaka 10 kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2021-2030 anasema umelenga uwepo zaidi wa sauti za wazee wenyewe kuona mahitaji yao na kuyaboresha.

Hapa nchini, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) iliungana na wadau wote duniani mwaka jana, Oktoba Mosi katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani kwa kutoa wito wa kuendeleza uhai na uchumi wa wazee kupitia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo, “Matumizi Sahihi ya Kidigitali kwa Ustawi wa Rika zote.”

Kaulimbiu hii inalenga kuhakikisha kuwa matumizi ya kidijiti yanachangia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, wakiwemo wazee na kuchochea ubunifu kwa shughuli zinazolenga kuimarisha ustawi wa wazee na wananchi wote.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Maimu akizungumza katika maadhimisho hayo aliwataka wadau katika maeneo mbalimbali nchini hupata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo kuhusiana na mustakabali wa haki na ustawi wa wazee kwa ujumla.

Jaji Maimu alisema katika matumizi ya teknolojia serikali imechukua hatua kadhaa, ikiwemo kukamilisha mkongo wa taifa wa mawasiliano ambapo mikoa yote ya Tanzania (Bara na Zanzibar) imeunganishwa na kuwezesha uwepo wa kampuni mbalimbali za mawasiliano ambazo zimeunganishwa kwenye mkongo huo.

Alisema hatua hizo zimetoa fursa kwa wananchi wengi wakiwemo wazee kutumia huduma za kimtandao kutatua changamoto zinazowakabili na hivyo kujiletea maendeleo.

Hata hivyo, jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa katika kuboresha matumizi ya teknolojia kwa wazee kwa kuwa idadi ya wazee imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina wazee 2,507,508 ambapo wanawake ni 1,307,358 na wanaume 1,200,210 na hadi mwaka 2021 idadi hiyo imeongezeka. Ongezeko la wazee huashiria uhitaji wa ongezeko la huduma kwao ikiwemo za kidijiti.

Tume inaipongeza serikali kwa hatua zilizochukuliwa kuboresha maisha ya wazee nchini ili kuhakikisha wanapata huduma jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee kuwa ni moja ya vipaumbele vya serikali.

Pia Tume inaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutunga Sheria ya Masuala ya Wazee Namba 2 ya mwaka 2000; kuweka utaratibu wa kuwapatia pensheni jamii na vitambulisho vya kupatiwa huduma mbalimbali wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70.

Aidha, Tume inaipongeza serikali kwa kuendelea 

kutoa huduma ya matunzo, ulinzi na usalama kwa wazee wote. Huduma hizi zimesaidia kupunguza vifo na mauaji kwa wazee hapa nchini.

Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, bado wazee wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwepo kwa sheria mahususi ya wazee, kuchelewa kwa malipo ya mafao kwa wastaafu na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wazee.

Tume inatoa rai kwa serikali kukamilisha mchakato wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 kwa kushirikiana na wadau ili sheria inayosimamia masuala yote ya wazee iweze kutungwa.

Pia serikali iongeze jitihada kutatua changamoto za upatikanaji wa dawa katika hospitali na zahanati ili wazee wafaidi huduma hizo kama ilivyokusudiwa. Serikali ihakikishe mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati ili kuwaondolea wazee usumbufu wa kufuatilia.

“Tanzania yenye matumizi sahihi ya kidijitali kwa ustawi wa rika zote inawezekana endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake,” alisema.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Kitaifa yaliyofanyika katika Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ally Khamis, alisema wanawake na wazee ndio makundi yaliyoachwa nyuma katika matumizi ya dijitali na kusisitiza kuwa serikali itahakikisha hawaachwi nyuma na wanawezeshwa kushiriki kikamilifu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/13eb62b11d1e86eb3e89e6f7cb558b7b.png

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi