loader
RUWASA yaendelea kumtua mama ndoo kichwani

RUWASA yaendelea kumtua mama ndoo kichwani

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Mwanza inayosimamia upatikanaji wa maji vijijini unaendeleza juhudi kabambe za kumtua mama ndoo kichwani mkoani humo kupitia programu mbalimbali ili kutekeleza lengo la serikali kufikisha huduma hiyo vijijini kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.

Mwanza inakadiriwa kuwa na watu 3,016,307 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ambapo watu 2,121,371 wanaishi maeneo ya vijijini na maeneo ya mjini yenye hali ya vijiji huku vyanzo vikuu vya maji safi na salama ni visima vifupi, virefu na Ziwa Victoria.

Serikali kwa kutambua kuwa maji ni uhai, imekuwa na mipango mingi ya kuhakikisha kuwa Mtanzania ana uhakika wa kupata maji safi na salama karibu na makazi yake na mojawapo ya mikakati hiyo ni uboreshaji wa huduma ya maji unaofanywa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya II (WSDP II).

Mkakati mwingine ni kupitia fedha za mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya Covid-19 ambapo miradi tisa ya Sh bilioni 4.5 imeanza kutekelezwa kwa mwaka 2021/22 ambapo watu 205,147 watanufaika mkoani Mwanza.

Meneja wa Ruwasa mkoani Mwanza, Godfrey Sanga alisema hivi karibuni jijini Mwanza alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli zao katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kuwa miradi tisa itajengwa na kuboreshwa katika kipindi cha miezi sita na kukamilika kwa miradi hiyo kutafanya eneo hilo kuwa na asilimia 75 ya huduma ya maji safi na salama.

Alitaja wilaya zitakazonufaika na miradi hiyo kuwa ni Sengerema, Kwimba, Misungwi, Ukerewe, Magu, Ilemela na Nyamagana huku miradi hiyo ikitarajiwa kukamilika Juni mwaka huu (2022).

“Miradi hiyo ni mwendelezo wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan kumtua mama maji kichwani kwa kumwezesha kupata huduma hiyo karibu na nyumbani kwake,” alisema Sanga.

Sanga alisema vijiji 13 vitanufaika na miradi hiyo huku shule za msingi, zahanati, shule za sekondari na vituo vya afya navyo vikiwa ni miongoni mwa taasisi zita kazonufaika na huduma hiyo kwa kufikishiwa mabomba.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel alitaka hatua madhubuti kuchukuliwa ili kutekelezwa kwa miradi hiyo kwa ubora unaotakiwa na unalingana na thamani ya fedha hizo.

Alisema kwa vile maji ni uhai kukamilishwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi katika kuwawezesha kuwa na rasilimali hiyo muhimu kwao.

Gabriel alipongeza uamuzi wa serikali kuelekeza fedha hizo katika miradi inayogusa maisha ya watu na hivyo aliitaka mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa azma ya kusudio la fedha hizo inatimizwa.

Katika kuhakikisha kuwa hilo lengo la kumtua mama maji kichwani mwanzoni mwa mwezi huu Ruwasa mkoani Mwanza imetiliana saini na wakandarasi watano wa kizalendo kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwa zaidi ya Sh bilioni tatu.

Utiaji saini huo umefanywa jijini Mwanza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ngussa Samike ambaye aliwataka wakandarasi hao kutekeleza kazi hizo walizozipata kwa uadilifu mkubwa.

Aliwataka wakandarasi hao kuepuka kutoa visingizio vyovyote vile katika shughuli zao hizo watakazokwenda kufanya ili kuwezesha taifa kupata huduma ya maji safi na salama kama ambavyo inasisitizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Samike aliwataka wakandarasi hao kushirikisha viongozi wa serikali katika maeneo wanayokwenda kufanya kazi ili kuwepo uwazi na uwajibikaji katika miradi hiyo.

“Tumieni wafanyakazi wa maeneo husika katika utekelezaji wa shughuli zenu ili wananchi wanufaike na kazi hizo na mpate ushirikiano mzuri kutoka kwao,” alisema Samike.

Meneja Ruwasa mkoani Mwanza, Sanga alisema miradi hiyo ina thamani ya Sh bilioni 3.44 na utekelezaji wa kazi hizo utafanywa kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja ambapo wilaya zitakazonufaika ni Sengerema, Kwimba, Misungwi, Ukerewe na Magu.

Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha kunufaisha Watanzania 85,179 katika wilaya hizo na kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 66 hadi kufikia asilimia 70 ya wakazi hao katika Mkoa wa Mwanza ifikapo Desemba 2022.

Kampuni zilizotia saini makubaliano ya kutekeleza shughuli hizo za usambazaji maji vijijini ni Simba Plastic Co. Ltd, M/S Dynotech Engineering Ltd, M/S Pet Cooperation Ltd, Tanzania Steel Pipes Ltd na M/S Consel Construction & Engineering Services LTD.

Sanga alisema pia kuwa mkoa unatarajiwa kupata miradi mingine itakayotekelezwa na ofisi ya makao makuu ya Ruwasa ya

thamani ya Sh bilioni 66.79 ambayo itafanywa kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi miaka miwili nayo inatarajiwa kusainiwa mwezi huu mkoani Dodoma. Anasema ikikamilika itahudumia wakazi 347,464 sawa na asilimia 16 ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza.

Alisema kuwa ongezeko la huduma ya maji kwa wakazi waishio vijijini katika Mkoa wa Mwanza itaongezeka kutoka asilimia 66 iliyopo sasa na kufika asilimia 86 na asilimia 90 kwa wakazi wa mjini ifikapo Desemba 2023.

“Tunashukuru serikali ya Rais Samia kwa kutupatia Sh bilioni 70.23 kwa mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu ya maji mkoani humu,” alisema Sanga.

Sanga alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo itasaidia katika kutimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 inayotaka kufikisha huduma ya maji katika maeneo ya vijijini nchini kwa asilimia 85 ifikapo 2025.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/87f253535ebf0071b396bf7dd41642c3.png

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Suleiman Shagata

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi