loader
Usafiri wa vivuko wazidi kuimarika

Usafiri wa vivuko wazidi kuimarika

UKUAJI wa uchumi imara katika taifa lolote duniani pamoja na mambo mengine unategemea uimara wa sekta ya usafirishaji wa aina zote.

Lakini kwa nchi ambazo zimezungukwa na mito, maziwa na bahari, uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji wa majini ni muhimu zaidi katika ustawi wa jamii inayoishi kuzunguka maeneo hayo.

Uboreshaji wa miundombinu ya usafiri wa majini kama vile ujenzi wa vivuko, boti za kisasa na meli imara hufanya shughuli za usafirishaji wa mizigo na mazao ya wakulima na wafugaji kwenda kwa haraka zaidi.

Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Mwanza ambao unasimamia vivuko vyote vya serikali katika uendeshaji, ukaguzi, matengenezo na usimamizi wa miradi mipya ya ujenzi wa vivuko na maegesho umefanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano.

Kaimu Meneja wa Temesa Mkoa wa Mwanza, Abdallah Atiki anasema wakala umeendelea na matengenezo ya mara kwa mara ya vivuko kwa ufanisi katika pantone zote zinazotoa huduma kwa wananchi katika Ziwa Victoria.

Anasema katika kipindi cha Machi, 2020 hadi Desemba mwaka jana, matengenezo ya kinga yameendelea kufanyika kama yalivyopangwa, matengenezo ya dharura pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara yamekuwa yakifanyika kwa wakati ili kuimarisha ufanisi wa uendeshaji wa vivuko hivyo.

Atiki anasema katika kipindi hicho, kivuko cha Mv Temesa kwa sasa kipo katika Kampuni ya Songoro Marine Boat Yard kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa ili kufanya matengenezo ya kubadilisha ‘shaft ya propel ya gearbox’, mifumo ya upoozaji injini na gearbox na mifumo ya uwashaji injini.

“Kivuko cha Mv Chato tayari kimefanyiwa matengenezo makubwa na kivuko cha Mv Saba Saba na boti ya uokoaji ya Sir III vimefanyiwa matengenezo ya mifumo ya upoozaji injini na ‘gear box’ na mifumo ya uwashaji injini,” anaeleza.

Anasema katika mwaka wa fedha 2021/22 wakala ulivifanyia matengenezo vivuko vyote inavyovisimamia ili kutoa huduma salama kwa wananchi na mali zao.

Anaongeza kuwa wakala uliunda pia vikosi kazi vya wataalamu wa vivuko Novemba 2018 ambapo kimojawapo kipo jijini Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma za matengenezo kwa vivuko vilivyoko Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla ambavyo vina wataalamu waliobobea katika matengenezo ya vivuko.

“Timu hiyo imekuwa ni msaada mkubwa sana kwa kuhudumia vivuko hivyo kwa wakati,” anasema Atiki.

VILIVYOJENGWA

Anazitaja shughuli zilizofanyika katika mwaka wa fedha 2021/22 kuwa ni ujenzi wa kivuko kipya chenye tani 85 ambao umekamilika na pantoni hiyo inatoa huduma kati ya Kayenze na Kisiwa cha Bezi.

Shughuli nyingine ni ujenzi wa maegesho, nyumba za wafanyakazi na ofisi kwa ajili ya kivuko cha Kayenze na Bezi na ujenzi huo unaendelea kwa sasa.

“Shughuli nyingine ni ujenzi wa kivuko cha Mv Ukara II ambacho kimekamilika na kwa sasa kinafanya kazi na ujenzi wa kivuko cha Mv Chato II ambacho kwa sasa kinatoa huduma Chato, ujenzi wake ulikamilika mwishoni mwa Desemba, 2020,” anaeleza Atiki.

Anaitaja miradi ya vivuko inayotarajiwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2021/22 kuwa ni ujenzi wa maegesho ya vivuko vya Kigongo/Busisi, matengenezo makubwa ya kivuko cha Mv Misungwi, ujenzi wa maegesho mapya ya kivuko katika kisiwa cha Kayenze na Bezi, matengenezo makubwa ya kivuko cha Mv Nyerere yanaendelea na ununuzi wa boti tatu zitakazotoa huduma kati ya visiwa vya Ilugwa, Nafuba na Ghana vilivyoko wilayani Ukerewe.

Atiki anasema kwa upande wa matengenezo ya uendeshaji wa vivuko katika kipindi cha kuanzia Machi, 2020 hadi Desemba 2021 vivuko vyote vilitoa huduma nzuri bila matatizo makubwa.

“Vivuko viliendelea kufanyiwa matengenzo ya 

kinga na ya uharibifu kwa nia ya kuvifanya viendelee kutoa huduma bora, uhakika na yenye usalama kwa wananchi,” anasema na kuvitaja vivuko vingine kuwa ni Kigongo-Busisi, Rugezi/Kisorya, Nyakaliro/ Kome na Bugorola/ Ukara.

“Eneo la Bugorola/Kome linahudumiwa na Kivuko cha Mv Kome II, kivuko hiki kina hali nzuri na kinaendelea kutoa huduma nzuri ya uvushaji wa wananchi na mali zao kati ya Nyakaliro wilayani Sengerema na kisiwa cha Kome kilichopo Halmashauri ya Buchosa,” anaeleza Atiki.

Anasema katika mwaka wa fedha 2021/22 wakala unatarajia kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali ya vivuko ikiwemo ya ujenzi wa maegesho ya vivuko Kigongo/ Busisi, matengenezo makubwa ya kivuko cha Mv Misungwi, ujenzi wa maegesho mapya ya kivuko katika visiwa vya Kayenze na Bezi.

CHANGAMOTO Kaimu Meneja huyo wa Temesa anasema wakala unakabiliwa na changamoto za uendeshaji, matengenezo na miradi ya vivuko kuikamilisha.

Anasema changamoto ya uwepo wa magugu maji ambayo huziba njia za pantoni na kuifanya kuwa finyu na hivyo kuathiri utoaji wa huduma ya uvushaji.

“Magugu maji haya hukokota nyavu na mishipi ya wavuvi na kuvisogeza kwenye njia ya pantoni na hivyo kusababisha uharibifu wa ‘oil seal’ za ‘lower gear box’ na ‘propel’ za vivuko,” anasema.

Anasema changamoto nyingine wanayokabiliana nayo

ni baadhi ya watu binafsi kuendesha shughuli za kuvusha abiria na mizigo katika maeneo ya vivuko vya serikali vinavyovusha wananchi na mali zao na hivyo kusababisha wananchi hao na mali zao kutovuka kwa usalama.

“Hali hii huathiri mwenendo wa mapato ya vivuko na kusababisha vishindwe kujiendesha,” anasema na kuvitaja vivuko vilivyoathiriwa na hali hiyo kuwa ni pamoja na Kivuko cha Mv Temesa kinachotoa huduma katika eneo la Luchelele na Irunda na kivuko cha Mv Kome II kinachotoa huduma katika eneo la Nyakaliro wilayani Sengerema.

“Hali ya utendaji wa vivuko vyote 12 imefanyika karibu wa asilimia 100 kuanzia Machi 2020 hadi Desemba 2021,” anasema.

WANANCHI WANENA Wakazi wa Wilaya ya Misungwi wameuomba uongozi wa wakala kuendelea kuboresha huduma zake hususani kwa vivuko vinavyofanya safari kupitia maeneo ya Kigongo-Busisi ambapo kuna uhaba wa vivuko unaosababisha foleni nyingi za magari yanayotokea MwanzaSengerema-Geita nyakati za usiku.

Pili Seif, mjasiriamali na mkazi wa wilayani Sengerema anasema changamoto hiyo huwaathiri watumiaji wa vivuko na kutotekeleza shughuli zao kwa wakati.

“Huduma za vivuko hivi ni nzuri, lakini naona kwa wakati wa usiku bado kuna changamoto ya kuvusha abiria na magari kwa wakati,” anasema Pili.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b37afa954000e2e5e15d084e7fd13542.png

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi