loader
Kukausha mboga kwa mfumo wa jua, vitalu nyumba na faida zake kiafya, kiuchumi

Kukausha mboga kwa mfumo wa jua, vitalu nyumba na faida zake kiafya, kiuchumi

MABADILIKO ya kiteknolojia yanayoendelea duniani yana msukumo mkubwa kwa jamii kubuni teknolojia mbadala zinazoweza kuikomboa kimaisha na kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi makabila yaliyopo nchini kupitia ubunifu yameendelea kuzikabili changamoto mbalimbali ikiwemo udumavu.

Kabila la Wasukuma kwa upande wao hukausha mbogamboga na viazi juani bila kuzingatia utaratibu wa kitalu nyumba na hivyo pamoja na kwamba ni ubunifu wa kiteknolojia lakini vimekuwa vikipoteza virutubisho.

Kiongozi wa Kikundi cha Iponya Matembe na mkazi wa Kijiji cha Inolelo, Kata ya Ngofila, Halmashauri ya Kishapu, Helen Emmanuel, anasema kikundi chao wanatumia teknolojia ya mfumo wa jua kupitia kitalu nyumba kukausha mbogamboga na viazi lishe bila kupoteza virutubisho vya asili vilivyomo.

Emmanuel anasema kuwa teknolojia hiyo wamepata mafunzo kutoka shirika la kujinyanyua kiuchumi la Redeso lililopo wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga.

Anasema kabla ya hapo walikuwa wakitumia njia ya kuanika juani na kuhifadhi kwa ajili ya matumizi ya chakula baadaye hali ambayo wataalamu walidai kupoteza virutubisho na kuwa makapi.

“Kutumia mfumo jua katika ukaushaji mbogamboga na viazi lishe tumejiingizia vipato na kujishughulisha na kilimo cha viazi lishe na mbogamboga ambapo tumeanza kusindika unga wa viazi lishe ukiwa na mchanganyiko wa vitu vingine,” anasema Emmanuel.

Emmanuel anasema kuwa mfumo wa ukaushaji kisasa unaendeshwa na kikundi chao na unachukua muda wa siku mbili kukauka kwani wamekuwa wakikausha mbegu za maboga na mbogamboga za aina zote.

Pia anasema wamekuwa wakikausha viazi lishe na baadaye kusaga kupata unga kwa ajili ya kutengeneza keki, biskuti na maandazi.

Emmanuel anasema faida ya kukausha kwenye teknolojia hiyo wanayoipata kwenye viazi lishe ni kutopoteza uhalisia wa madini ya vitamini A ambayo mjamzito na mtoto chini ya umri wa miaka mitano akila ataepuka kudumaa.

“Kitalu nyumba tulijenga kwa kushirikiana na fundi kutoka shirika la Redeso ni njia nzuri kupitia mfumo huu kukausha, hauna gharama wala kupoteza muda ukiweka kwenye vichanja vinakauka vyenyewe, hakuna vumbi wala mchanga unaoingia na kubaki vyakula kuwa safi tofauti na zamani tulivyokuwa tukikausha kwa kuanika juani,” anasema Emmanuel.

Anasema kuwa mtu anayehitaji kukausha kwenye mfumo huo ambaye si mwanakikundi analipia Sh 1,000 na wamekuwa wakitengeneza unga wa viazi lishe ulio na mchanganyiko wa vyakula kwa Sh 5,000 kwa kuweka vifungashio vilivyo na ubora na soko lipo.

Aidha, Emmanuel anaiomba serikali iwasaidie kuboresha zaidi teknolojia hiyo waliyoibuni na kuendelea kuwapatia elimu kwani elimu iliyotolewa na Redeso kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Oxfarm ni nzuri.

Anasema teknolojia hiyo inachukua muda mfupi na imeweza kuwaibua na kuisaidia jamii vitu vingi ikiwemo kuepuka suala la udumavu.

“Matarajio tuliyonayo ni kufungua kiwanda cha kusindika viazi lishe kwani eneo la Kishapu historia yake haipati mvua za kutosha, kila mwaka kuna ukame lakini wamefanya kipindi chote cha masika na kiangazi mboga zipatikane kwa wingi muda wote zenye virutubisho halisi,” anasema Emmanuel.

Nyanzobe Kuzenza ni mwanakikundi wa Iponya Matembe anasema kuwa mboga zimekuwa na soko kubwa hasa msimu wa kiangazi na familia zimekuwa zikija kununua kwa kupimiwa kwenye kikombe cha chai. Anasema mbogamboga iliyokaushwa ni Sh 300 hadi Sh 500.

Kuzenza anasema kuwa kabla ya kuja teknolojia hiyo walikuwa wakikausha mbogamboga juani kama vile majani ya kunde, mchicha, kisamvu na matembele au majani ya viazi.

Meneja wa Redeso, Charles Buregeya, anasema kuwa vikundi vilivyoundwa vinakabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri usalama wa chakula na lishe kwenye jamii ambapo wao walikuja na mradi wa kuwajengea uwezo katika uzalishaji na kuongeza thamani baada ya kukausha kwa mionzi ya jua.

“Teknolojia hiyo imekuwa na thamani yake ya kukausha mbogamboga na viazi lishe na kudumu kwa muda mrefu bila kupoteza uhalisia wa virutubisho vilivyopo kwani hakuna kitu mbadala kwenye mboga za majani kama ukizikosa mwilini,” anasema Buregeya.

Buregeya anasema mboga za majani zina mchango mkubwa kwa wajawazito na watoto kwa kuongeza damu kwa haraka na lengo la kusindika vyakula ni kuanzisha vitalu nyumba, bustani na ukaushaji wa viazi lishe ambao umewafanya kuandaa unga kwa ajili ya watoto walio chini ya miaka mitano.

“Mafunzo tuliyoyatoa walikwenda watu 14 mkoani Morogoro na walirudi na baadaye kuyafanyia kazi mafunzo hayo lakini sasa wameonesha mafanikio kwa mitazamo waliyokuwa nayo kutoka kilimo cha mazoea na kwenda kisasa pia ukaushaji wa kitaalamu kupitia vitalu nyumba,” anasema Buregeya.

Ofisa lishe kutoka Shirika la World Vision, Magreth Charles, anasema kuwa mtoto anatakiwa apewe mbogamboga sababu zina madini ya vitamini A wanapokuwa wakikausha juani wanapoteza virutubisho na kubaki kula makapi hivyo si sawa kukausha mbogamboga juani moja kwa moja.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/821f16e21fce3f0aa48706ad25389b0c.png

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi