loader
Samia afunda mawaziri

Samia afunda mawaziri

RAIS Samia Suluhu Hassan amewafunda mawaziri na naibu mawaziri katika mkutano wake na viongozi hao huku akiwataka kuacha ubabe, kutunishiana misuli, kuondoa muhali na kuepuka kutoa ajira za kirafi ki au kindugu.

Aidha, amewataka watendaji hao kudhibiti siri za serikali zisisambae mitandaoni huku akionya kugombana wenyewe kwa wenyewe kwa kuangalia maslahi yao binafsi badala ya wananchi.

Mkutano huo aliufanya jana mjini Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake kwa viongozi hao aliyoitoa siku chache zilizopita wakati akiwaapisha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu katibu wakuu walioteuliwa kuongoza wizara mbalimbali katika mabadiliko ya baraza la mawaziri aliyoyafanya hivi karibuni.

Akizungumza na watendaji hao, Rais Samia alisema mawaziri wanafanya kazi kwa muhali na hakuna anayemwambia kiongozi mwenzake ukweli hadi tatizo linatokea na wengine wanatumia ubabe kwa viongozi wenzao na kuonya vitendo hivyo.

“Hivi mnajua muhali ni nini?, Muhali ni jambo ambalo umemuona kiongozi ana tatizo ila humwambii na tatizo linaendelea na linakuja kuharibu kazi, sasa kitendo cha kutomwambia mtu ukweli wa tatizo lake ndio muhali, kama mwenzio ana tatizo muite kistaarabu, sio kibabe.

“Sio unatumia komandi, njoo hapa au nitakwenda kumwambia mama, mimi hapana rekebishaneni kwanza huko ndani, mkianza kutunishiana misuli na kuoneshana ubabe ndio matatizo yanaanza ndani ya wizara au taasisi mnazoziongoza,” alisema

Siri za serikali

Akizungumzia siri za serikali, Rais Samia alionesha kukerwa na mwenendo wa sasa ambao siri na nyaraka mbalimbali za serikali za ndani ziko kwenye mitandao watu wanatumia kubishana.

“Hii nalo ni madhara, ducuments (nyaraka) za serikali tunazikuta kwenye mitandao, watu wanabishana huku mtu anakwenda kuchomoa nyaraka inayobishaniwa na kuweka ushahidi, nendeni kasimamieni na kudhibiti siri za serikali zibaki ndani ya serikali, hata makatibu wakuu tutawaambia hili,” alisisitiza na kuongeza: “Unalimiliki sekta yako, unaendeshaje timu yako, uifanye kama mali yako iendeshe kwa tija, nyie ni wanasiasa watendaji, sio wale waliopewa tu mawizara kwa siasa huko zamani, nyie ni wanasiasa watendaji, nendeni mkasimamie hutakiwi kuwa meneja, ila ufuatilie ifanye vizuri.”

Ajira za kirafiki na kindugu

Rais Samia alizungumzia masuala ya ajira kwenye taasisi na wizara mbalimbali na kuonya mawaziri na naibu mawaziri kutoa ajira kwa kuangalia ukaribu wa wanaowaajiri ama ni rafiki au ndugu kwa sababu kufanya hivyo ni kuiharibu taasisi wanazoziongoza.

“Ukiajiri rafiki zako au ndugu zako ni mwanzo wa tatizo, unaweza kumvuta rafiki ukiamini mtachapa kazi ni sawa, ila ukiwavuta kirafiki au kindugu tu utaua taasisi unayoiongoza, naomba sana mkazingatie hayo,” alisema.

OPRAS

Rais alizungumzia Fomu za Upimaji Utendaji Kazi wa Watumishi (OPRAS) na kuwataka watendaji hao wakazishughulikie kwa sababu hazina matokeo wala mwongozo mzuri.

“Watumishi wasiowajibika sheria zipo, kuna kitu kinaitwa OPRAS, kila wakati zinajazwa halafu sioni matokeo yake sijui zinaenda kwa nani halafu wapo watumishi wanajaziwa vibaya hizo fomu na ukiangalia ni wale wanaochukiwa na mabosi wao, lakini pia wapo wasiofanya vizuri ila wamejaziwa vizuri na mabosi wao kwa vile tu ni watiifu kwa mabosi hao,” alisema Rais Samia. Alisema katika fomu hizo hakuna mrejesho wa aliyefanyiwa upimaji huo na wala haijulikani inapelekwa wapi na nani anatoa mrejesho na kuitaka Menejimenti ya Utumishi wa Umma ikasimamie jambo hilo vizuri liwe na tija.

Taasisi ya urais

Katika mkutano huo, Rais Samia alifafanua kuhusu Taasisi ya Urais na kusema urais sio mtu binafsi na kuwa rais anakuwa kiongozi katika taasisi hiyo kwa mujibu wa Katiba akae pale kuangalia mambo yanavyokwenda.

“Taasisi ya urais sio mtu binafsi, yeyote anayekuwa hapo anafanya kazi ya taasisi, sasa kama humpendi aliyeko, penda nchi yako, lakini pia tunaambiwa mamlaka zinatoka kwa Mungu sasa kama humpendi huyo rais, Mheshimu Mungu wako, maana mamlaka imetoka kwake.”

Hata hivyo, alionya mawaziri na naibu hao kwa kuwaambia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni taifa kamili na kama ni kulibomoa wao ndio wa kwanza kulijenga au kulibomoa na kuwaambia wao wamebahatika kuwa na nafasi mbalimbali hivyo wazitumikie kwa uadilifu kwa mujibu wa viapo vyao.

“Sasa kama unakwenda kinyume na kiapo cha dini yako nenda kajitathmini mwenyewe, hakuna anayeweza kupasua moyo wako kujua unachokitathmini, ila tambua umeibeba nchi,” alisema.

Rais aliwataka mawaziri hao kujenga pia utamaduni wa kufuatilia utekelezaji wa kazi mbalimbali za serikali kwa wananchi na kuwataka kuwa na taarifa na takwimu sahihi badala ya kupika takwimu pale viongozi waombapo wakati wanajua taarifa hizo sio za kweli.

“Wakati tunaomba taarifa ya utekelezaji basi itakusanywa na kuletwa, ukifuatilia unakuta sio halisi ama takwimu au taarifa zimepikwa au zimepitwa na wakati, tunapotaka ripoti toeni za uhalisia tuko hapa kuwashughulikia wananchi, msitufurahishe sisi mbele wananchi nyuma,” alisema

Mawaziri kutoelewana

Rais Samia alionya pia mawaziri hao na Naibu mawaziri kwa kutoelewana baina yao kwenye utendaji kazi na kusema anashangaa na haelewi kwa nini wanagombana wakati kila mmoja amechaguliwa kwa vigezo vyake.

“Waziri na naibu hawaelewani, Katibu Mkuu na naibu wake hawaelewani, mimi sielewi, hapa kila mtu yuko kwenye nafasi yake kwa vigezo vyake, sijui kwa nini kuna migongano, mnagombania safari, mara hii ilikuwa yangu, mara yeye hanipi safari…gawaneni maeneo mfanye kazi, migongano ndani yenu haina tija,” alisema.

Aliwafunda kuwa yeye alipoingia ndani ya siasa aliwahi kuchaguliwa kuwa Waziri lakini hajawahi kugombana na wa chini yake hata siku moja na kuwataka kila mmoja atimize wajibu wao na kuondokana na ugomvi baina yao.

“Sijawahi kugombana na wa chini yangu, nilikuwa waziri, lakini sijawahi kugombana na wenzangu na wakati mwingine mnagombana kwenye mgongano wa maslahi, wengine wanasema hili mbona mimi sijapata, sio kwamba hampati kwenye maeneo yenu bali mnakula mnavimbiwa ni kufuru,” alionya.

Alitaka pia mawaziri hao kufanya kazi kwa kufuata sheria, sera na katiba na kila mmoja akaangalie sera inayomuongoza na kama imepitwa na wakati zibadilishwe ziendane na wakati ili kuwa na matokeo chanya ya maendeleo kwa wananchi na taifa.

Katika hatua nyingine aliwapongeza mawaziri wote na kusema hata waliobadilishiwa wizara alifanya hivyo kwa kuona kuwa watafanya vizuri zaidi kwenye maeneo hayo na kuwataka wakafanye kazi na lengo ni kutoa huduma bora kwa wananchi.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/3b1420262b70b9b5a2754870c35274b1.jpg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi