loader
Wana-CCM wapigana vikumbo  kumrithi Ndugai, sasa wafikia 49

Wana-CCM wapigana vikumbo kumrithi Ndugai, sasa wafikia 49

WAZIRI wa zamani wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Msalala, mkoani Shinyanga Ezekiel Maige ni miongoni mwa wanachama 19 waliojitokeza jana kuchukua fomu za kuomba kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi(CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge na kufanya waliochukua fomu mpaka sasa kufi kia 49.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu jana, alisema yeye ndio anayefaa kwenye nafasi hiyo kwani ana uzoefu katika uongozi na bunge hilo kwa kulitumika kwa zaidi ya miaka 15.

Alisema ana historia nzuri na chama tangu alipojiunga akiwa na umri wa miaka 19, hivyo ana uwezo wa kukiwakilisha vema katika kuleta maendeleo ya nchi hasa katika kupambana na umaskini, ujinga na maradhi.

Akizungumza jana kwa niaba ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, Katibu Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM, Solomon Itunda aliwataja waliochukua fomu kwenye Ofisi ya Makao Makuu ya chama hicho Dodoma ni Maige, Wakili Emmanuel Mng’arwe, Aziz Mussa, Wakili Onyango Otieno, Doto Mgasa, Profesa Edison Lubua, Fikiri Said, Profesa Itikija Mwanga na Peter Njemu.

Alisema katika Ofisi Ndogo ya CCM Dar es salaam waliochukua fomu ni, Ndurumah Mejembe, Godwin Maimu, Johnson Japhet, Mohamed Mmanga, Esther Makazi, Mariam Moja, Joseph Anania, Samweli Xaday, Arnold Peter na Joseph Sabuka na katika Ofisi ya CCM Zanzibar hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu hadi sasa.

Wanachama wengine waliochukua fomu mpaka sasa ni mwanasiasa mkongwe na Mbunge wa zamani wa Bariadi, Andrew Chenge na Dk Titus Kamani.

Pia Dk Mussa Ngonyani, Wakili Faraji Rushagama, Hamisi Rajabu, Dk Titus Kamani na Asia Abdallah, Festo Kipate, George Nangale, Barua Mwakilanga, Zahoro Haruna, Thomas Kirumbuyo, Angelina John na Jaaf Hussein nao wamejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wengine waliochukua fomu ni Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu, Emmanuel Mwakasaka Mbunge wa Tabora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Profesa Mpoki Mafwenga ambaye ni Ofisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Msukuma, Goodluck ole Madeye, Sophia Simba, Juma Hamza Chum na Baraka Byabyato.

Pia wamo Simon Ngatunga, Tumsifu Mwasamale, Merkion Ndofi, Dk Tulia Ackson, Godwin Kunambi, Ambwene Kajula, Patrick Nkandi, Steven Masele na Hamidu Chamami. Itunda alisema uchukuaji wa fomu utafungwa Januari 15 na gharama za kuchukua fomu ni Sh milioni moja.

Baada ya uchukuaji na urejeshaji fomu kukamilika, Januari 17, mwaka huu Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa wagombea waliojitokeza kuomba kiti cha uspika.

Januari 18 hadi 19 kutakuwa na kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu itafanya kazi hiyo.

Aidha, Januari 21 hadi 30, mwaka huu kikao cha chama cha wabunge wa CCM kitapiga kura kumpata mgombea ambaye atakwenda kusimama bungeni kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa kuwa Spika. Mchakato huo unafanyika kutokana na kujiuzulu kwa Job Ndugai katika nafasi hiyo Januari 6, mwaka huu.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/9716b366a0ec1c270d6ab99c1fd91fc9.jpeg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi