loader
Dk Mpango aonya mawaziri  rushwa, ulevi, majungu

Dk Mpango aonya mawaziri rushwa, ulevi, majungu

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameonya mawaziri, naibu mawaziri kujiepusha na vitendo vya rushwa, ngono, ulevi, majungu na tuhuma za uchawi na kuwataka walinde hadhi zao kwa mwenendo na matendo yao.

Alitoa onyo hilo jana wakati akihitimisha mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi hao aliowaita na kuzungumza nao juu ya utendaji na masuala mengine ya utumishi na utawala bora ili kuwepo na tija katika kuwatumikia wananchi na taifa.

Aidha, Dk Mpango alisema wamepokea maelekezo yote ya Rais na ushauri wake na kuwa mambo yote aliyoonya wameyasikia na watayafanyia kazi ikiwamo kukomesha migongano baina ya mawaziri na naibu mawaziri.

“Hatutarajii kuona tena migongano baina yenu, jiepusheni na vitendo vya rushwa ikiwamo ya ngono isitajwe kwenu hata tuhuma tu, kuweni watendaji wenye maadili, ulevi, majungu na tuhuma za uchawi havistahili kwenu,” alisema Dk Mpango.

Alisema hadhi zao na nafasi zao kiutendaji vinapaswa kuheshimiwa na kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa weledi na utu, huku wakimsaidia Rais katika kazi zake na sio kumtwika mzigo.

“Rais kasisitiza viongozi kuzingatia kanuni na miongozo ya nchi, masuala mengine yaishie kwa Waziri Mkuu sio kila jambo mnamtwika Rais,” alisema.

Alisema ni wakati sasa wa kufanyakazi kwa kujipima na kuangalia wapi wamekwama na kujisahihisha na kuhakikisha jambo la msingi kwao ni kutimiza wajibu wao.

Dk Mpango aliwataka viongozi hao waguswe na shida za watu na kuwahudumia, huku akiwasisitiza kuwa jambo linaloamuliwa kwenye Baraza la Mawaziri ni lao wote na sio la waziri mmoja mmoja hivyo wanapaswa kuliunga mkono na kulitetea.

Alisema katika kutekeleza wajibu wao, viongozi hao wanapaswa kufahamu kuwa hawatakuwa mawaziri wa milele, hivyo wawe wanyenyekevu na kukumbuka majimbo yao ya uchaguzi kwa sababu wao ni wabunge na wametokana na kura za wananchi kwenye maeneo yao.

Aidha, aliwakumbusha kumtegemea Mungu na kumtanguliza huku akimhakikishia Rais Samia kuwa wamemsoma na kumuelewa na wametoka na mtazamo chanya.

“Tumekusoma mama, tumekusoma Rais, tunatoka na mtazamo chanya, tumepata shule ya nguvu,” alisema

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/99c7e451a6b0da71182c3d016ea9c59e.jpg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi