loader
Shahidi aeleza  alivyotoa taarifa  miamala simu  ya Mbowe

Shahidi aeleza alivyotoa taarifa miamala simu ya Mbowe

S HAHIDI wa tisa katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu ameanza kutoa ushahidi wake.

Alitoa ushahidi jana katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa kueleza namna alivyotoa taarifa za usajili na miamala ya simu ya Mbowe kwa Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi.

Shahidi huyo, Gladys Fimbari ambaye ni Mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya simu za mkononi ya Airtel alieleza hayo jana mbele ya Jaji Joachim Tiganga anayeendesha kesi hiyo.

Fimbari alidai Julai 2, 2021 akiwa anatekeleza majukumu yake ya kila siku katika Ofisi za Airtel Morocco, alipewa jukumu na mkuu wake wa Idara la kushughulikia maombi ya taarifa za miamala ya fedha na usajili wa namba za simu 0782 237 913, 0787 555 200 na 0784 789 944.

“Baada ya kupokea maagizo hayo nilihakiki barua kama ni kweli imetoka katika taasisi husika ya uchunguzi wa kisayansi ambayo ilikuwa inaongelea taarifa za kiuchunguzi na niliangalia taarifa inayoombwa pamoja na kuhakiki kama imegongwa muhuri wa idara ya uchunguzi wa kisayansi,” alidai.

Alidai baada ya kujiridhisha aliingia kwenye mfumo kupitia kompyuta yake na kuingiza namba za simu zilizoombewa taarifa moja moja na kupata ambazo zilikuwa ni za usajili wa namba za simu pamoja na miamala ya fedha iliyofanyika kupitia namba hizo na kisha ‘aliprinti’ na kuandaa barua aliyoiambatanisha na taarifa alizopata kutoka katika mfumo.

Shahidi huyo pia alizitambua nyaraka alizozifanyia kazi alipooneshwa mahakamani na kutaja alama zilizomo katika nyaraka hizo ikiwemo jina, saini yake pamoja na muhuri wa Kampuni ya simu ya Airtel.

Alitaja alama nyingine kuwa ni namba ya kumbukumbu ya barua kutoka Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi. Baada ya kutambua nyaraka hizo ambazo ni barua kutoka Ofisi ya Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi, barua kutoka idara ya sheria ya Airtel na taarifa za usajili na miamala ya fedha, shahidi huyo aliomba kuzikabidhi mahakamani ziwe sehemu ya vielelezo katika mwenendo wa shauri hilo, jambo ambalo upande wa utetezi walikubaliana na nyaraka hizo zikapokelewa mahakamani hapo.

Alipoulizwa kuhusu usajili wa namba hizo alidai kuwa moja ilikuwa imesajiliwa kwa jina la Freeman Mbowe, nyingine ilisajiliwa kwa jina ya Denis Urio ambazo alidai zilifanya muamala wa Sh 500,000 kutoka kwa Mbowe kwenda kwa Urio ambaye katika ushahidi uliotangulia anatajwa kuwa alimtafutia Mbowe vijana wa kumsaidia kutekeleza mpango wa ugaidi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Khalfan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya ambao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwemo kufadhili na kupokea ufadhili wa kutekeleza vitendo vya ugaidi ikiwemo kulipua mikusanyiko ya watu na vituo vya mafuta nchini.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/f1407b6f9ab4b41fbab56753ae8eef5c.jpg

MSANII wa Filamu nchini, Isarito Mwakalindile, maarufu kama ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi