loader
Aliyejifanya mtumishi TRA  ahukumiwa jela miaka 2

Aliyejifanya mtumishi TRA ahukumiwa jela miaka 2

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma imemhukumu mkazi wa jijini Dar es Salaam, Kitareti Mahuti kifungo cha miaka miwili gerezani na kulipa faini ya Sh milioni mbili baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kujifanya kuwa Mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Aloyce Katemana baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka. Katika kesi hiyo namba 170 ya mwaka 2019, Hakimu Katemana alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.

Alisema hukumu hiyo ya kutumikia kifungo cha miaka miwili na kulipa faini ya Sh milioni mbili iwe fundisho kwa watu wanaojifanya watumishi wa umma na kutenda makosa.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Miyango Kezilahabi alidai mshtakiwa alifikishwa mahakamani mara ya kwanza mwaka 2019.

Mwanasheria wa TRA, Hadija Senzia alidai mshitakiwa alikuwa akitumia kitambulisho feki cha mamlaka na alikuwa akizunguka kwenye maduka na nyumba za kulala wageni na kujitambulisha kuwa ni mtumishi akiwa na fomu za mamlaka. Alidai alikuwa akiwakagua wateja na kuwatishia kwa makosa mbalimbali na nyaraka nyingi zilikuwa za kughushi.

“Alikuwa akiwatishia wale wasiotoa risiti kwa njia ya kielektroniki (EFD) na alikuwa akidai fedha,” alisema.

Kwa mujibu wa Senzia, mshitakiwa alikuwa akitumia majina tofauti kwenye kitambulisho chake ambacho kilikuwa na namba za kuonesha kuwa ni mwajiriwa wa TRA.

“Alikuwa na kitambulisho feki cha TRA chenye jina la Miringe James, kazi Ofisa wa Kodi.” Senzia alidai mshitakiwa huyo alikamatwa Agosti 2019 na alikuwa akizunguka mikoa mbalimbali akijifanya Ofisa Kodi wa mamlaka na alikuwa akitumia gari aina ya IST.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/68177d99684998cc624569c860dd811b.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi