loader
Serengeti pekee utawaona wanyama ‘Big Five’

Serengeti pekee utawaona wanyama ‘Big Five’

KWA muda mrefu Tanzania imeendelea kusifi ka duniani kwa kuwa na utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii ambavyo hapa nchini huchangia asilimia 17.2 ya pato la taifa.

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linalosimamia na kuendeleza utalii nchini chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, lililoanzishwa kwa Sheria za Tanganyika Sura 412 ya mwaka 1959, tangu kuanzishwa kwake limefanya mambo mengi na makubwa.

Mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali na viongozi wake ikiwemo pia mwaka 2017 kubadilisha rasmi utaratibu wake wa utendaji kazi kutoka mfumo wa kiraia kwenda kwenye mfumo wa Jeshi Usu.

Likiwa linasimamia jumla ya hifadhi 22, zilizo katika kanda nne, Kaskazini yenye hifadhi tano, Kusini tatu, Mashariki nne na Magharibi 10 limechangia katika maendeleo ya utalii kupitia katika hifadhi zake. HIFADHI YA SERENGETI Katika Hifadhi ya Serengeti ambayo ndiyo ya kwanza kuanzishwa nchini mwaka 1959, iliongezwa kukidhi mfumo kamili wa kiikolojia kwa tangazo katika Gazeti la Serikali (GN) Namba 235 la mwaka 1968.

Ofisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindaga George anasema hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 na ni sehemu ya urithi wa dunia na eneo la usitiri wa maisha. “Ni miongoni mwa hifadhi maarufu na bora duniani na imepata tuzo ya hifadhi ya kwanza ya ubora barani Afrika mwaka wa tatu mfululizo,” anasema George.

Anasema jina la Hifadhi Serengeti limetokana na neno la Imsaidi “Siringeti” linalomaanisha mbuga pana zisizokuwa na mwisho. George anasema ilianzishwa rasmi mwaka 1951 ikiwa ni hifadhi ya kwanza Tanganyika ikiwa na ukubwa kilometa za mraba 14,763 na mwaka 1959 ilitangaza rasmi mipaka yake na Ngorongoro.

Watu waliokuwepo pia walihamishwa. HADHI/TUZO Kutokana na kusifika kwa ubora wake duniani, anasema mwaka 2019/20 na 2021 ilitangazwa kuwa hifadhi bora barani Afrika na kupata tuzo ya Hifadhi Bora Afrika (The Best National Park in Africa). “Ni hifadhi inayofuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii na imepata tuzo ya kuwa ni eneo la urithi wa dunia na usitiri wa maisha tangu mwaka 1981,” anasema.

Anasema uhamaji wa nyumbu, pundamilia, swala tomi na pofu katika hifadhi hiyo umekuwa pia ni moja ya maajabu saba ya asili duniani 2008 na kuiongezea hadhi kubwa.

“Ni moja ya maajabu makubwa katika ulimwengu wa asili kwani hakuna sehemu nyingine duniani wanyama wanahama kwa idadi kubwa kama Serengeti,” anasema.

Kwa upande wa tuzo, George anasema imepata tuzo ya urithi wa dunia na usitiri wa maisha ya UNESCO mwaka 1981, tuzo ya Maajabu Saba ya Asili ya Afrika na Dunia 2006 na tuzo ya kuwa Hifadhi Bora barani Afrika kwa mwaka 2019, 2020 na 2021 iliyotolewa na The World Travel Awards.

“Imeshika nafasi ya pili katika Jarida la Forbes kama sehemu nzuri zaidi kutembelea duniani kwa mwaka 2021,” anasema. Anazitaja sababu za kupata tuzo hiyo ni jitihada zinazofanywa na serikali katika kuunga mkono shughuli za uhifadhi nchini, imekuwa ni eneo la urithi wa dunia na usitiri wa maisha UNESCO mwaka 1981 na ipo kwenye mfumo wa ikolojia wa Serengeti-Mara ambao ni wa makazi ya wanyama wahamao.

“Lakini ina idadi kubwa ya wanyamapori, ndege, mimea, wadudu na viumbe maji,” anasema. Anazitaja sababu zingine za kupata tuzo kuwa ni ari, utendaji kazi na moyo wa uzalendo wa maofisa na askari, usimamizi wa sheria na miongozo hasa baada ya kuingia kwenye mfumo wa kijeshi, ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama.

“Sababu nyingine ni ushirikiano mkubwa wa jamii kwenye uhifadhi na utalii,” anasema na kuongeza kuwa inatoa huduma zake za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa (ISO 9001:2015). VIVUTIO VYA UTALII Anasema Serengeti ina vivutio vingi vizuri vya kipekee vya utalii vikiwemo zaidi ya 27 ya wanyama walao nyama kama simba, tai, fisi na duma ambapo nyumbu na pundamilia wamekuwa ni kivutio kizuri cha watalii kutoka nje ya nchi.

“Hifadhi yetu ya Serengeti ina uwanda usio na mwisho ambao ni kivutio kizuri,” anasema George. Anasema Serengeti ni moja ya maeneo machache duniani ambayo mtu anaweza kuwaona wanyama maarufu wajulikanao kama “Big five,” ambao ni faru mweusi, tembo, nyati, chui na simba.

“Hifadhi ya Serengeti ina aina ishirini na nane (28) za wanyama walao majani kama vile swala tomi, pundamilia, twiga,” anaeleza. Anasema pia ina aina zaidi ya 540 za ndege, baadhi wakisafiri kutoka sehemu nyingine duniani wakiwemo jamii ya tai, mwewe, kasuku na ina utajiri mkubwa wa maeneo ya kihistoria na kitamaduni kama vile michoro ya maasai, ngome ya Fort Ikoma na nyinginezo.

MFUMO WA IKOLOJIA

Anasema Hifadhi ya Serengeti ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia, Serengeti Mara yenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,000 ambao hutafasiriwa kama eneo la uhamaji wa nyumbu na wanyama wengine.

“Maeneo yanayounda mfumo huu ni pamoja na:- Mapori ya akiba ya Maswa, Ikorongo-Grumeti, Kijereshi, Pori Tengefu la Loliondo, eneo la Mamlaka ya Ngorongoro, Hifadhi ya Serengeti na Hifadhi ya Maasai Mara iliyoko Kenya,” anaeleza.

AINA ZA UTALII

Anasema hifadhi hiyo ina aina mbalimbali za utalii kama wa mbuga na kuvinjari nyikani, wa upigaji picha, mali kale, wa kupata chakula porini, wa puto na utalii wa kutembea kwa mguu ambao hufanyika maeneo maalumu ambapo watalii husindikizwa na askari wa hifadhi.

GHARAMA ZA KUTALII

Anasema watu wanapowasili Serengeti hupata malazi katika hoteli na nyumba za kulala kwa gharama nafuu kwa makundi yote. “Tofauti na watu wengi wanavyofikiria, gharama kwa Mtanzania na Afrika Mashariki kutalii Hifadhi ya Serengeti ni nafuu sana,” anasema.

Anasema mtu mzima ili aingie hifadhini anatakiwa kulipa Sh 11,800, mtoto wa miaka mitano hadi 15 ni Sh 2,360 na watoto chini ya miaka mitano hawalipi viingilio. Kwa upande wa malazi hifadhini, anasema bei ya mtu mmoja ni Sh 23,600 kwa siku moja na kwamba mtu anatakiwa kufanya ‘booking’ ya kupata chumba wiki moja au mbili kabla ya safari ya kuingia hifadhini.

“Gharama za malazi kwa aina zingine ambazo hazimilikiwi na Hifadhi zitakuwa tofauti kulingana na sehemu husika,” anaeleza. Kuhusu gharama za magari yanayoingia hifadhini, anasema magari yenye uzito wa tani 0 hadi mbili ni Sh 23,600, tani 2.1 hadi tatu ni Sh 41,300 na magari yenye uzito wa tani 3.1 hadi saba ni Sh 70,800 na magari yenye uzito kuanzia tani 7.1 hadi 10 ni Sh 177,000 na tani 10.1 na kuendelea ni Sh 354,000.

“Magari kuanzia tani 10 lazima yapate kibali kutoka makao makuu ya shirika,” anasema. Anasema baada ya serikali kuongeza idadi ya watalii watakaoingia nchini kufikia milioni tano kwa mwaka ifikapo 2025, mkakati uliopo kwa sasa ni kukuza utalii wa ndani na nje na kuandaa safari za kutembelea vivutio vya utalii kwa jamii.

“Tutaanzisha vikundi vya waongoza utalii na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa,” anasema. MAONI YA WADAU Rajab Nassib, mkazi wa Mwanza anasema pamoja na mafanikio hayo bado sekta ya utalii nchini inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za ubovu wa miundombinu kwenda kwenye maeneo ya hifadhi.

Naye Yohana Maiko kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii anasema utalii katika hifadhi zilizopo nchini unaimarisha afya ya akili na matarajio yake ni kuona usalama wa watalii katika hifadhi unakuwepo zaidi na kujengwa kwa uhusiano mzuri kati ya uongozi wa hifadhi na jamii.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7737e52664bc0ddb64eb39c11123fa61.jpeg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Na Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi