loader
Hatua za serikali kukabili ukame Kiteto, Simanjiro

Hatua za serikali kukabili ukame Kiteto, Simanjiro

INASIKITISHA, inaumiza na kutia uchungu kila eneo unalopita katika Wilaya ya Kiteto na Simanjiro mkoani Manyara unaona maelfu ya mifugo imeanguka chini, haiwezi kusimama na mingine imekufa.

Hali hiyo inatokana na janga la ukame lililoibuka katika wilaya hizo kutokana na kuchelewa kunyesha mvua na hivyo kusababisha uhaba wa chakula na malisho ya mifugo. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amefika maeneo hayo kujionea madhara ya ukame na kuwapa pole wafugaji wa Kiteto waliopoteza ng’ombe 1,874 na Simanjiro waliopoteza mifugo 62,585.

Katika kipindi cha Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu Mkoa wa Manyara umepoteza mifugo 64,459. Ulega amepokea ripoti ya Wilaya ya Kiteto na Simanjaro hali ilivyo kwenye vijiji na kisha alikwenda kwenye maeneo hayo kuzungumza na wafugaji walioathirika na janga hilo.

“Mifugo maelfu imekufa kwa sababu ya athari za ukame na hivyo wafugaji kukosa malisho ya mifugo,” anasema Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Kiteto, Dk Lunonu Sigalla. Sigalla anasema hali ya malisho katika maeneo yaliyotengwa ya Kimana, Mbigiri, Partimbo, Ilera, Namelock, Laalala, Ndeleta, Ndorkon, Ilpogong’I, Loorera, Amei, Lempapuli, Lesoit, Orkitikiti, Engang’uengare, Lerug na Enguserosidan hayana malisho sababu ya kuchelewa mvua.

“Hali halisi ya malisho ya mifugo kwa kipindi cha Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, si ya kuridhisha kutokana na kuchelewa kwa mvua, hivyo kusababisha vifo vya mifugo hususani ng’ombe,” anasema Sigalla.

Naye Ofisa Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Simanjaro, Dk Swalech Masaza anasema: “Wananchi wa Simanjiro hawana chakula, wametumia kulisha mifugo na sasa hawana akiba, wana njaa, mifugo yao imekufa mingi na iliyobaki imekonda na haiwezi kuuzika.” “Maeneo mengi hayana malisho, lakini yaliyopata mvua yamekwenda kutupa malisho katika maeneo ya kata za Loibosiret, Emboreet, Komolo, Terrat, Naisanyai na Naberera.

Hivyo msongamano mkubwa zaidi wa mifugo upo kutoka katika maeneo ya vijiji vya Endonyongijape, Langai, Ngage, Laoibosoit B, Kitwai B na Lerumo katika wilaya hiyo ya Simanjiro,” anasema Masaza. Masaza anasema katika Wilaya ya Simanjiro mifugo 62,585 imekufa ambapo ng’ombe ni 35,746, mbuzi 10,033, kondoo 15,136 na punda 1,670.

Ulega alitembelea kata na vijiji ambavyo vina maafa makubwa na wafugaji wamepoteza mifugo yao akatoa neno kwao. “Poleni sana wafugaji, serikali haijawaacha katika kipindi cha janga la ukame, imenituma kuja kuwapa pole kwa kukumbwa na janga hili. Kuona ni kuamini,” alisema Ulega na kuongeza:

“Nimeshuhudia kwa macho yangu mifugo mingi ipo katika hali mbaya katika maeneo yote ambayo yamekumbwa na ukame mkali na kusababisha mimea imekauka na visima vya maji na kusababisha mifugo kukosa maji na malisho.”

Ukipita kwenye mazizi Wamaasai wanayaita maboma, huwezi kuamini mizoga ya ng’ombe ilivyojaa, baadhi imeshachunwa ngozi ili kutunza ngozi na pia ili isivimbe na nyama hiyo ikauke na kuchomwa moto. Katika maeneo hayo kuna makundi ya ng’ombe dhaifu ambao hawawezi kutembea wamelala sababu ya kukonda huku mifupa yake ikionekana kudhihirisha kukosa maji na malisho.

Hali hiyo inawalazimu wafugaji kusafiri umbali mrefu lakini mifugo mingine kufa njiani. Katika baadhi ya maboma wamebaki wanawake wanalinda nyumba na kulisha watoto, wanaume wamesafiri kwenda kutafuta malisho katika maeneo ya mbali hasa karibu na hifadhi ya Tarangire na Mkomazi au kwenye pori la Mkungunero kutafuta malisho.

“Hali ya ng’ombe ni mbaya, wamekonda na hawa Simanjiro, Christopher ole Sendeka. “Wananchi wangu wana hali mbaya, hawana chakula kwa sababu mahindi kidogo waliyokuwa nao wamelisha mifugo na mifugo yenyewe sababu ya kukosa malisho na maji haiuziki,” anasema Ole Sendeka.

Mbunge wa Kiteto, Edward ole Lekaita anasema eneo lake lenye wengi asilimia 65 mifugo yao imekufa na hawana chakula ambacho wazalishaji ni asilimia 35 na wameshindwa kuzalisha sababu ya ukame. Ulega, baada ya kusikiliza kilio hicho na kushuhudia kwa macho hali hiyo alisema mkakati wa serikali wa kudumu wa namna ya kukabiliana na hali hiyo siku za mbeleni.

“Licha ya serikali kuwapa pole, imekuja kuwapa matumaini kwamba changamoto ya ukame ni mipango ya Mungu, lakini sisi kama binadamu tunatakiwa kujiandaa kukabiliana na hali hiyo kwa kuchimba mabwawa na malambo ya kunyweshea mifugo hasa maeneo yenye ukame,” anasema Ulega.

Alisema serikali ni sikivu, imetenga Sh bilioni 130 kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kunywesha mifugo katika maeneo mbalimbali hasa yenye changamoto ya mvua kama ya wafugaji. Fedha hizo zilizopo chini ya Wizara ya Maji zitatumika kununua mitambo ili kila mkoa uwe na mtambo wake mmoja kwa ajili ya kuchimba malambo au mabwawa ya kunywesha mifugo ya kutosha katika maeneo hayo.

Ulega anawataka viongozi wa wilaya hizo mbili za Kiteto na Simanjiro kujiandaa na kuwa tayari kwa kuwa na madokezo, maandiko na nyaraka za utayari wa kuwa wa kwanza kupewa mitambo hiyo ili kuchimba mabwawa. Alisema serikali pia imejiandaa kukabiliana na ukame kwa kusambaza nyasi za malisho ya mifugo katika wilaya hizo ili wananchi wapande, wavune na wahifadhi na kuzitumia wakati wa ukame kama huu.

Katika mkakati huo mahususi wa kusambaza nyasi nchini chini ya mtaalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Lucy Chacha itasaidia wafugaji kuwa na malisho wakati wote na kutumia wakati wa kiangazi au ukame kama huo. Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mbunge wa Kiteto, Lekaita akampa ahadi Ulega kwamba atakuwa wa kwanza kupanda nyasi hizo ili shamba lake kuwa darasa kwa wafugaji wengine kujifunza na kupanda katika mashamba yao.

Ulega pia aliwataka wafugaji kubadili mitazamo, kuacha kufuga kwa mazoea kwa kuwa na makundi makubwa ya mifugo isiyo na afya.

Akawataka wabadilike kadiri ya mfumo wa kufuga ng’ombe wachache lakini walio bora. Naibu waziri huyo aliwataka wafugaji waanze kupunguza mifugo kwa kuuza na kupata fedha na kufanyia shughuli za maendeleo kama kujenga nyumba bora na za kisasa, kusomesha watoto na kuboresha maisha yao.

Ulega aliwataka wafugaji wakubali agizo la wizara la kuweka hereni kwenye masikio ya mifugo ili kujua mifugo lakini pia kukatia bima ili hapo baadaye ikitokea changamoto ya ukame wa kukosa malisho na maji na mifugo kufa, walipwe fidia. Anawataka viongozi wa wilaya kuhakikisha suala la maji linapewa kipaumbele kwani bila maji hakuna maisha.

Ulega alitaka wawe mstari wa mbele kuhakikisha maji yanaendelea kupatikana kwenye visima vya asili pamoja na yanayosafirishwa kutoka maeneo ya mbali ikiwemo Ruvu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8aa706fcac45a2b9a526a292eaf4612d.jpeg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Na Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi