loader
Sensa ni mwaka huu, tujiandae

Sensa ni mwaka huu, tujiandae

SENSA ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemografi a, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalumu ama kilichopangwa.

Aidha, sensa ni zoezi maalumu lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi (eneo), kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, ajira, vizazi na vifo na makazi yao.

Takwimu hizo zinazotokana na sensa ndizo zinazoainisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwamo makundi maalumu yenye uhitaji maalumu. Makundi hayo ambayo tunaishi nao katika jamii ni watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.

Sensa ina umuhimu mkubwa katika kuharakisha shughuli za maendeleo. Mwaka huu sensa inatarajiwa kufanyika Agosti. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar inaendelea na maandalizi ya sensa hiyo inayofanyika nchini kila baada ya miaka 10.

Sensa ya mwisho ilifanyika nchini mwaka 2012. Nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012. Ifahamike kuwa maandalizi ya sensa yanafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 na sensa hiyo kwa mwaka huu inatarajia kutangaza nafasi 300 za ajira. FAIDA YA SENSA Sensa inapokuwa imefanyika kikamilifu inaisaidia serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa vipaumbele vyake muhimu ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Husaidia pia kwenye mageuzi mbalimbali yakiwemo ya masuala ya afya na jamii, ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo kimataifa na kwa upande wa halmashauri kuwepo kwa taarifa sahihi ya idadi ya watu baada ya sensa husaidia katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika.

Husaidia katika uwiano wa mgawanyo wa rasilimali, sensa pia ni kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano pato la mtu mmoja mmoja, pato la taifa, ajira na ukosefu wa ajira na taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote.

Lakini pia jamii itambue kuwa sensa ni taarifa muhimu itakayoiwezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo wa viashiria vingine ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira, ukiwemo msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia.

Mfano takwimu sahihi za sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala kwa upande wa mamlaka za serikali za mitaa. Ili sensa ifanyike vizuri kwa kawaida hutumia madodoso. Sensa ya mwaka huu kwa mujibu wa taarifa kutoka NBS itatumia aina mbili za madodoso.

Kwa mujibu wa NBS, madodoso hayo ni marefu na mafupi na dodoso refu litatumika kuhoji asilimia 30 ya maeneo yote ya kuhesabia watu na dodoso fupi litatumika kwenye asilimia 70 ya maeneo yote ya kuhesabia watu. Kwa kawaida utekelezaji wa sensa hufanyika katika awamu kuu tatu ambazo ni kipindi kabla ya kuhesabu watu, wakati wa kuhesabu na kipindi baada ya kuhesabu.

Kipindi cha kabla ya kuhesabu watu kwa mujibu wa NBS kinajumuisha uandaaji wa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa na nyaraka nyingine, utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu na uzalishaji wa ramani, uandaaji wa nyenzo yakiwemo madodoso na miongozo mbalimbali.

Uuundaji wa kamati za sensa kufanya mikutano na wadau wa takwimu, kufanya manunuzi, kufanya uchaguzi wa aina ya teknolojia itakayotumika, kuajiri wadadisi na wasimamizi, usambazaji wa vifaa na kufanya maandalizi ya tathimini ya sensa.

Kipindi cha kuhesabu kwa mujibu wa NBS kinajumuisha kazi kuu na ya muhimu katika hatua ya kuhesabu watu na kipindi cha baada ya kuhesabu watu kinajumuisha uchakataji wa taarifa za sensa, uchambuzi, utoaji wa matokeo ya awali, usambazaji wa matokeo ya mwisho, uhamasishaji wa matumizi ya takwimu kwa watumishi wa wizara, idara na taasisi za serikali.

Kwa mujibu wa NBS, kitabu cha mkakati wa usimamizi na utekelezaji wa sensa kimeshazinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kwa mara ya kwanza takwimu za sensa hiyo zitachukuliwa hadi kwenye kitongoji.

KAULI YA SERIKALI

Rais Samia Suluhu Hassan anasema Sensa ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Bila kuwa na takwimu huwezi kushughulikia changamoto za ajira, matatizo ya watu wenye mahitaji maalumu, kutoa huduma za kijamii wala kufanya maendeleo,” anasema Rais Samia katika moja ya hotuba zake.

Kamisaa wa Sensa nchini, Anna Makinda anasema mradi wa matumizi ya anwani za makazi na postikodi uliozinduliwa rasmi mwaka jana jijini Mwanza una umuhimu mkubwa katika kuharakisha shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya, kijiji hadi taifa.

Anawataka watendaji wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na viongozi wengine wa mikoa na halmashauri kuhakikisha wanakamilisha zoezi la uwekaji wa anuani za makazi haraka iwezekanavyo kurahisisha sensa.

Makinda anasema kutokana na umuhimu wa mfumo wa anwani za makazi serikali imeona ni vyema kufanya ushirika wa pamoja kwenye shughuli za utekelezaji wa sensa ili kwa pamoja kuwatambua wananchi, anuani zao za makazi, ajira na shughuli za kiuchumi. Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa anasema sensa hiyo kwa mwaka huu itafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kupitia setelaiti ambayo itafanyika kwa kutumia vishikwambi na hakutakuwepo na karatasi za dodoso.

Chuwa anasema muda wa kupanga na kuchambua takwimu utapungua na takwimu zitakazopatikana zitakuwa sahihi zaidi na matokeo yake yatapatikana kwa haraka zaidi kuliko sensa zilizotangulia. Anasema gharama za kufanya sensa hiyo kwa mwaka huu zitaongezeka ikilinganishwa na za mwaka 2012, sawa na ongezeko la Sh bilioni 172.2, ambapo kwa mwaka huu kitatumika kiasi cha Sh bilioni 328.2 (sawa na Sh 3,472 kwa mtu mmoja) ambapo mwaka 2012 zilitumika Sh bilioni 156.

Mkazi wa Ilemela aliyejitambulisha kwa jina la James Charles, anaiomba serikali iendelee kutoa elimu kuhusu faida ya sensa ili wananchi wote washiriki.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/50bb21428cc681928c0e191395b592a4.jpeg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Na Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi