MPELELEZI wa Makosa ya Jinai katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Askari Polisi namba H4347 Goodluck, amedai aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, ACP Ramadhan Kingai, aliunda timu maalum kwa ajili ya kudhibiti kikundi kilichoundwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kufanya vitendo vya ugaidi nchini.
Goodluck ametoa madai hayo leo Ijumaa, tarehe 21 Januari 2022, akitoa ushahidi wake katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.
Shahidi huyo wa 11 wa Jamhuri, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, amedai timu hiyo ilianza kazi ya kudhibiti kikundi hicho Agosti 5, 2020, baada ya kuwakamata watuhumiwa wawili, Ling’wenya na Kasekwa, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.