loader
Chuo cha Bandari chafanyiwa mageuzi makubwa kitaaluma

Chuo cha Bandari chafanyiwa mageuzi makubwa kitaaluma

CHUO cha Bandari kilichopo Dar es Salaam kinafanyiwa mageuzi ya kitaaluma kutokana na juhudi za serikali za kuboresha uwezo wa bandari nchini.

Aidha, serikali inaunda kamati maalumu kwa ajili ya kufuatilia suala la Chuo cha Utalii kutumia eneo la Chuo cha Bandari ambayo ripoti yake itapelekwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya hatua zaidi. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa bandari (TPA), Eric Hamisi, alisema hayo kwenye mahafali ya 20 ya chuo hicho jijini Dar es Salaam.

“Napenda kuwataarifu kuwa suala hili limeundiwa kamati ikihusisha vyuo vyote viwili ili kujadili uwezekano wa kurejesha majengo ya Chuo cha Bandari. Watalaamu hawa wataandaa andiko la ushauri na kuliwasilisha kwa Waziri wa Uchukuzi ambaye atatoa mrejesho wake,” alieleza Hamisi.

Hamisi, alisema kwa sasa chuo cha bandari kinazidi kupanuka na hivyo kuwa na uhitaji wa kuongeza miundombinu yake. Alisema kutokana na uamuzi uliofanyika mwaka 2001 wa kugawanya takribani asilimia 70 ya eneo la chuo cha Bandari na kukabidhiwa ka chuo cha utalii, asilimia 30 iliyobaki ya chuo hicho imezidi kuwa finyu.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete alitaka kamati hiyo maalumu kukamilisha majadiliano hayo haraka iwezekanavyo na kuwasilisha maoni yake kwa waziri kwa ajili ya uamuzi kutolewa haraka kwa manufaa ya vyuo vyote. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwakibete alisema chuo hicho miaka ya nyuma kilikuwa kinafanya vibaya kiasi cha kukaribia kufutiwa ithibati yake lakini kwa sasa kimefanya mageuzi makubwa ikiwemo kuongeza idadi kubwa ya udahili pamoja na kuwa na mipango ya kuboreshwa hali inayohitaji kipatiwa eneo kubwa la mafunzo.

Chuo cha Bandari kwa muda mrefu kimekuwa kikiomba serikali kuingilia kati suala la eneo lake lililopo Dar es Salaam kukabidhiwa kwa Chuo cha Utalii Tanzania, huku chenyewe kikikabiliwa na uhaba wa eneo kwa ajili ya kupanua shughuli zake. Akizungumzia wahitimu wa chuo hicho, Mkurugenzi huyo wa TPA aliwahakikishia kuwa mamlaka itatoa kipaumbele kwa wahitimu wa chuo hicho kadri inavyopata vibali vya ajira.

Naibu Waziri Mwakibete alisema, “imesikia mko katika jitihada za kuanzisha kozi ya shahada, nashauri mitaala itakayoandaliwa ilenge changamato za bandari na matarajio yangu mtazingatia viwango vya ubora na mtakuwa kituo cha elimu bora.”

Mkuu wa Chuo hicho, Dk Lufunyo Hussein alielezea mageuzi makubwa ya kuboresha chuo hicho ni pamoja na mpango wa kuanzisha kozi ya shahada na kuanzisha maabara maalumu ya kisasa ya masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika masuala ya bandari.

Jumla ya wahitimu 709 walihitimu jana ambao kati yao wanawake ni 309 na wanaume 400.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2cd4798e7a3b8c254116a180229e665d.jpeg

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa ...

foto
Mwandishi: Na Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi