loader
FRANK NGAILO: Mbioni kucheza soka la kulipwa Uturuki

FRANK NGAILO: Mbioni kucheza soka la kulipwa Uturuki

ULEMAVU si kilema na unaweza ukawa mlemavu ukafanya mambo makubwa. Zamani na hata sasa kuna baadhi ya familia zilidiriki hata kuwaficha watoto wenye ulemavu na kushindwa kupata haki ya msingi kama watoto wengine.

Lakini kwa Frank Ngailo ambaye ni mlemavu wa mguu mmoja hali ni tofauti, kwani wazazi wake walimpatia elimu. Akiwa shuleni ameshiriki michezo mbalimbali na sasa ni mmoja wa wachezaji wa soka la watu wenye ulemavu anayeipeperusha bendera ya Taifa ughaibuni.

Kabla ya kwenda ughaibuni, Ngailo na wenzake 16 wanaocheza timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, ‘Tembo Warriors’ walikata tiketi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia, fainali itakazofanyika nchini Uturuki Oktoba mwaka huu.

Katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Canaf), Ngailo aliibuka mchezaji bora wa mashindano na mchezaji mwenye nidhamu, hatua iliyomfungulia njia kuonekana na timu ya Izmir inayocheza Ligi Kuu ya Uturuki.

Mcheaji huyo alizaliwa Julai 9, 2000, Ludewa Njombe akiwa na ulemavu wa mguu ni mtoto wa kwanza katika familia ya mzee Cassian Ngailo na mke wake, Yusta ambaye alibahatika kupata watoto watano, wanaume watatu na wawili wa kike, kati ya hao, yeye pekee ndio aliyezaliwa na ulemavu.

Licha ya kuzaliwa na ulemavu, wazazi wake hawakujisikia unyonge, walimpatia elimu na kuungana naye bega kwa bega katika kufikia malengo yake, ikiwemo kukuza kipaji chake cha kucheza soka la ushindani.

ELIMU YAKE Ngailo alihitimu kadato cha nne katika Shule ya Sekondari Pugu, shule ya awali alisoma Kimbili wilaya ya Ludewa, Njombe hadi darasa la pili baada ya hapo alifanikiwa kupata udhamini wa Kanisa la la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na kumleta Dar es Salaam na kuanza upya darasa la kwanza hadi la saba katika Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu.

“Nilifanikiwa kumaliza darasa la saba nikapata bahati ya kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Pugu na kusoma hapo hadi kidato cha nne, baada ya hapo sikutaka kuendelea kwa sababu ya soka,” alisema Frank.

MAISHA YA SOKA

Anasema alianza kucheza soka akiwa darasa la nne na baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu kuanzishwa mwaka 2017 lilianzisha Ligi Kuu, ambapo yeye alicheza katika klabu ya L.S.L. Anasema alichezea timu ya shule wakati wa mashindano ya wenyewe kwa wenyewe na mara nyingine kuna timu kutoka nje ya shule ya wachezaji waliokamilika viungo alikuwa akicheza nao.

Anasema mpira wa ushindani alianza kucheza mwaka 2015 baada ya kwenda sekondari na kukutana na wenzake wenye ulemavu na pia alicheza na wanafunzi wenzake wenye viungo vyote.

NAFASI ANAZOCHEZA

Anasema ana uwezo wa kucheza nafasi ya ushambuliaji na kiungo, beki wa pembeni hiyo inatokana na soka la walemavu kutumia wachezaji saba, hali hiyo anamudu kucheza nafasi hizo. “Awali, nilikuwa nacheza kipa muda wote nikiwa katika mashindano ya Umitashumta, niliamua kuacha kucheza nafasi hiyo kwa sababu nilikuwa natumia mguu wa bandia, lakini nilipofika sekondari niliacha kudaka na kucheza ndani,” alisema.

anasema mwaka 2014 baada ya kuacha kutumia mguu wa bandia alipewa magongo na kuanza kujifunza mwaka 2015 alimaliza darasa la saba akiwa bado anacheza nafasi ya kipa.

CHANGAMOTO

Mchezaji huyo anasema kwa upande wa familia yake hakupata changamoto yoyote kwa sababu baba na mama pamoja na ndugu zake walimpa hamasa kubwa kwa kumpa moyo kuwa atafikia malengo yake.

“Kuna siku niliumia wakati niko kwenye mazoezi na vijana wenzangu ambao sio walemavu, ilitokea bahati mbaya nilimgonga mwenzangu na fimbo tunazotumia kutembelea, alichukia na kutoa maneno ambayo si ya kiungwana na kunipokonya gongo na kulitupa, niliumia sana na sikwenda tena kufanya nao mazoezi,” anasema.

Ngailo anasema walitupa gongo lake kwa sababu alikuwa mlemavu na ana imani angekamilika viungo wasingemfanyia hivyo. SIRI YA KIPAJI “Nilikuwa napenda sana kucheza soka, nikiwa nasoma sekondari niliomba Mungu kuwepo na mchezo wa mpira wa miguu kwa ajili ya watu wenye ulemavu,” anasema Frank.

Anasema hatua ya kuomba dua hiyo ni baada ya kukosa mashindano maalumu shuleni na hutengwa na wenzao ambao ni wazima hivyo wanacheza walemavu na wazima. “Nashukuru Mungu akasikia kilio changu mwaka 2018 walikuja watu kutoka nchi ya Ireland, lengo ni kuutangaza na kusambaza mchezo wa soka la walemavu uanze kujulikana,”.

“Walitoa mafuzo kwa walimu na kuleta vifaa vya mchezo huo, kwa kupindi kifupi walichokuja wageni hao kuliandaliwa na ligi nilifanya vizuri na kupata nafasi ya kufanya mazoezi na kupata nafasi ya kucheza na kupata nafasi ya kwenda Uturuki,” alisema Frank. Anasema hakufanikiwa kwenda Uturuki kwa sababu walimu wake walimzuia kwa sababu kipindi hicho walipenda asome na baada ya kumaliza elimu yake afikirie suala la soka.

“Nilikubali tiketi yangu kumpa mtu mwingine lakini haikunizuia kuuchukia mpira nilitoroka kwenda mazoezini, nikirudi nakutana na adhabu, lakini kwangu haikuwa na maana zaidi ya soka,” alisema Frank.

MCHEZAJI BORA

Anasema mbali na kutwaa tuzo msimu huu katika michuano ya Canaf yaliyopita awali, alifanikiwa kupata tuzo katika michuano ya Cecafa na mara tatu akichukua mchezaji bora wa Ligi ya Tanzania akiwa katika klabu yake ya L.S.L kuwa mabingwa mara tatu mfululizo. “Mbali na tuzo alizopata malengo yake makubwa ni kwenda kucheza soka la kulipwa na sasa nimepata nafasi ya kufanya majaribio nchini Uturuki,” anasema Frank.

Ngailo amefurahi kupata nafasi hiyo katika taifa hilo kwa sababu kuna ligi mbalimbali, ikiwemo Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili.

MASHINDANO CANAF

Amefurahi kuona malengo yake ya kuwa mchezaji wa kulipwa yanatimia baada ya kupata nafasi ya kufanya majaribio katika klabu ya Izmir BBSK. “Michuano ya Canaf imetoa fursa ya kujitangaza kwa sababu nimepata nafasi ya kwenda Uturuki na pia nilitakiwa pia Misri, nina furahi kuona malengo ya kucheza soka nje sasa yanaelekea kutimia, “ anasema Ngailo.

KOMBE LA DUNIA

“Serikali iendeleee kutusaidia kwa kila hali, kazi kubwa itakuwa kwetu wachezaji kupambana kuipeperusha vema bendera na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo zinatajwa katika soka la walemavu,” anasema Frank ambaye hajaoa na anaishi Chanika, Dar es Salaam kwa mjomba wake.

MAISHA IZMIR

Frank aliwasili Uturuki Januari 18 na atakuwa na siku 15 za kufanya majaribio na kucheza mechi siku nne katika klabu ya Izmir BBSK. Klabu ya Izmir BBSK inashika nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu nchini Uturuki na ishatwaa mataji 10 ya ndani na Ulaya.

SHUKRANI

Frank pamoja na TAFF wanatoa shukrani kwa wadau watatu waliojitokeza kufanikisha safari hiyo, ambao ni Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Gazeti hili linamtakia kila la heri katika majukumu yake mapya nchini Uturuki na akawe njia ya kuwafungulia njia wachezaji wengine wengi kutoka Tanzania kupata timu nje ya nchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/26641f01d5f82e0da8af5d822415faee.jpeg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Na Rahel Pallangyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi