loader
Wadau wasema hawana tatizo jinsia Uspika

Wadau wasema hawana tatizo jinsia Uspika

WADAU mbalimbali wakiwemo wasomi na wanasiasa wamesema hawana tatizo na jinsia katika kuchaguliwa kwa spika bali wanachotaka ni uwezo, weledi na umakini wa kiongozi huyo kuongoza mhimili huo mkubwa.

Aidha wameshauri mhimili huo kupitia wabunge wake utimize wajibu wao wa kutunga sheria zitokanazo na wataalamu ndani yao badala ya kusubiri kuletewa miswada na serikali waipitishe, hivyo waweke ratiba  ya kuwa na vipindi vya kutunga sheria au kufanya marekebisho zilizopitwa na wakati.

 

Kauli hizo zimetolewa jana  kwenye mjadala wa Kitaifa kuhusu uchaguzi wa spika wa bunge na matarajio ya wananchi kwa kiongozi huyo ajaye, mjadala uliofanywa kwa njia ya mtandao wa  Zoom na kuwashirikisha wasomi, mabalozi, wanasiasa, wananchi na wadau wengine kutoka ndani na nje ya Tanzania.

 

Naibu Makamu Mkuu wa Utafiti na Masuala ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Bernadeta Killian alisema mwenye sifa ya kuwa spika ni miongoni mwa wabunge au nje ya bunge ila awe na sifa ya kuwa mbunge na hivyo suala la jinsia sio la msingi kinachoangaliwa ni uwezo wake katika nafasi hiyo.

 

Alisema hoja ya kwamba spika aliyeteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwania nafasi hiyo ni mwanamke na kuibua mijadala miongoni mwa wananchi hoja hiyo inapaswa isiangaliwe kwa mtazamo wa jinsia ya mtu basi itazamwe juu ya uwezo wa kuongoza mhimili huo.

 

Killian akifafanua kuhusu demokrasia alimtaka spika ajaye akaisimamie taasisi hiyo na kuhakikisha inaimarisha demokrasia na sio kuididimiza, na jambo la pili ni bunge liendelee kujenga umoja wa kitaifa na sio kubomoa.

 

Alisema  kazi ya bunge ni kujadili hivyo wabunge wafanye majadiliano yatakayojenga umoja wa kitaifa na kuleta maridhiano ili kuifnaya nchi iendelee kuwa salama  na tatu ni bunge litunge sheria na kujadili miswada na kutoa hoja zenye kujenga ili wananchi wapate maendeleo.

 

Alitoa angalizo kuwa siasa zinabadilika na inaweza kufika mahali wabunge wakamchagua mtu nje ya chama cha siasa akaongoza bunge ili mradi ana uwezo na wanaona anafaa.

 

Nurali Rashid mchangiaji wa mjadala huo alisema anaamini zaidi kwenye uwezo wa mtu katika kuongoza na sio kuangalia jinsia yake hivyo wananchi waache kujadili jinsia ya mtu na wajikite kuangalia uwezo, weledi na vitu gani anafanya katika kuimarisha mhimili huo mkubwa ndani ya nchi.

 

Igolola Henry mdau mwingine kwenye mjadala huo alisema hana tatizo na jinsia anachoangalia ni kupata kiongozi anayeweza kuongoza mhimili huo kwa weledi na kufuata misingi ya katiba na sheria mbalimbali.

 

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM),alichangia mjadala huo na kusema kama nchi inataka kuendelea na kulisaidia bunge ni lazima Watanzania wakaondoa  hisia potofu kwenye mambo ya msingi.

 

“Tuache kuzungumzia vitu kwa hisia, tujadili mambo ya maana na sio kujadili jinsia ya mtu, hapa tunaangalia uwezo,weledi na uongozi,sasa haya mambo yanayoendelea kujadili jinsi hayana afya kwa taifa letu, kiongozi ni yule menye uwezo wa kuongozi bila kujali jinsia yake,”alisema Lusinde.

 

Alisema kujiuzulu kwa spika aliyepita kulitokana na makosa yake mwenyewe na hayawezi kumhusisha naibu spika hivyo kujiuzulu kwake kulikuwa sahihi na hakuwezi kumhusisha naibu  na hiyo ndio sababu hakujiuzulu.

 

Alisema kwa spika aliyependekezwa na CCM ana sifa na uwezo wa nafasi hiyo na kuwatahadharisha wabunge na mawaziri kuwa makini kwa kujielekeza kujibu maswali sawasawa kwa sababu spika ni mkali na mfuatiliaji wa mambo anayependa kuona kila kitu kiko sawa.

 

Akizchangia majadiliano hayo, Naibu Balozi Hoyce Temu anayeiwakilisha Tanzania jijini Geneva, Uswisi alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameamini viongozi vijana na kuwapa nafasi wanawake wenye uwezo akiamini watawajibika kuwaletea maendeleo wananchi na kazi iliyopo ni kuonesha imani hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii.

 

“Kuhusu uteuzi wa mgombea nafasi ya spika, Dk Tulia Ackson mimi sina wasiwasi nae, manfahamu vizuri alikuwa mbele yangu shule tulikuwa tunamtegemea kwenye kujibu hoja nzito katika mijadala shuleni, tukishindwa yeye ndio anaingia kujibu, uwezo wa kuongoza anao,”alisema Temu.

 

Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima(CCM)alichangia mjadala huo na kusema spika mtarajiwa ni ni mkali kwa kusimamia nidhamu hivyo wabunge na mawaziri wanapaswa kuwa makini na kutoa hoja zenye mashiko.

 

Aliyewahi kuwa Waziri wa Afya Mstaafu na kiongozi wa kambi ya upinznai bungeni, Hamad Rashid alichangia mjadala huo na alionya bunge kutojiingiza kwenye jambo lisilo na tija  na kuwataka wabunge wakijite kutunga sheria kama ilivyowajibu wao.

 

“Wabunge watunge Sheria na sio kusubiri serikali ilete wao wapitishe,waweke ratiba ya kuwa na vipindi vya kutunga sheria au kufanya marekebisho zilizopo ili tuje na sheria nzuri .kazi kubwa ya bunge ni kutunga sheria ila hili halifanyiki, tujenge bunge iwe taasisi iliyokamilika. Wabunge wengi ni wavivu kusoma sheria, niliona hayo hata nilipokuwa mbunge,” alisema Rashid.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6f70f25dde1d0feb089c6a649f140b30.jpg

MBUNGE wa Kigamboni, Dk Fausitine Ndugulile (CCM) ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi