loader
Mabeyo ahimiza jeshi kuchangia uchumi nchini

Mabeyo ahimiza jeshi kuchangia uchumi nchini

MKUU wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo amevitaka vikosi vya jeshi kutumia wataalamu wa ndani kubuni miradi ya kimkakati na kuhimiza uadilifu kwenye miradi iliyokamilika.

Mabeyo alisema hayo wakati wa kuzindua kituo cha mafuta cha R971 kilichojengwa na jeshi eneo la Ihumwa.

Alisema jeshi kama taasisi linaweza kufanya mambo makubwa na kinachotakiwa ni kujiamini, kuwa na mitazamo chanya, wakati wote kuwa wabunifu na waadilifu katika miradi hiyo.

“Hakuna kisichowezekana na wenzetu wameweza kwani sisi tusiweze, kuna taaluma chungu nzima ndani ya jeshi lakini tumezilaza, tuziibue taaluma tulizonazo kwa manufaa ya jeshi na taifa kwa ujumla, mimi bado naamini inawezekana,” alisema.

Mabeyo alisema pamoja na kuwa serikali ina wajibu wa kuhudumia jeshi kwa asilimia 100, bado kuna haja ya jeshi kuwa na mchango kwa nchi kama ilivyo kwa majeshi makubwa kwa kuanzisha miradi mbalimbali

“Nilipata fursa za kutembelea maeneo ya ndani na nje ya nchi yakiwemo majeshi makubwa, wenzetu huko wanafanya mambo makubwa na wanachangia uchumi na pato la Taifa, lakini sisi tulikuwa tunategemea serikali kwa asilimia 100. Wajibu wa serikali kulihudumia jeshi ni kweli ndio dhana, je, sisi hatuna mchango wowote? Mchango wetu ni kuhakikisha tunachochea ukuaji uchumi na jukumu letu la msingi la ulinzi wa nchi na haya yanawezekana,” alisema.

Aidha, Mabeyo alisisitiza vikosi kuendelea kuimarisha miradi iliyokwisha kamilika na kufikiria miradi mikubwa zaidi na ya kimkakati.

“Fikra hizo ni lazima tuelekeze kwenye ubunifu, tubuni miradi mikubwa na ya kimkakati kama huu (kituo cha mafuta). Watu hawaelewi kama mafuta ni mradi wa kimkakati, mafuta yakikosekana katika nchi ina paralyzed nchi na iki paralyze nchi hakuna usalama katika nchi na ndio maana nilifikiria hili lazima tulibebe maana ni suala la kimkakati na la kiusalama,” alisema.

Mabeyo alisema hivi sasa jeshi linaangalia uwezekano wa kuagiza mafuta moja kwa moja ili kuwa na akiba ya nchi na kuwa na mitambo ya kusafisha mafuta nchini.

Alisema kikosi cha R 971 ni miongoni mwa vikozi vitatu vilivyoanzisha miradi ya kimkakati. Vingine ni 12 KJ na 27 KJ. Mabeyo aliahidi kukipatia kituo hicho Sh milioni 100 kwa ajili ya kukipa uwezo zaidi ikiwa ni mbali na Sh milioni 100 zilizotolewa awali.

 

Pia alitoa wito kwa maofisa, askari  na wakazi wa Ihumwa wenye vyombo vya usafiri kuwa wateja wa kwanza kwenye mradi huu wa kituo cha mafuta.

Vile vile alipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kuwa mfano wa kutekeleza miradi ya kimkakati ukiwemo wa skimu ya umwagiliaji ambao umelenga kujilisha na kuweka akiba chakula.

Awali Kamanda wa kikosi R971, Kanali Justus Kitta alisema kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya Sh milioni 280 kikiwa na matangi yenye uwezo wa kuhifadhia zaidi ya  lita 60,000 za mafuta.

Alisema mkakati uliopo ni kuongeza visima zaidi na kujenga kituo kingine jijini Dodoma kabla ya kuwa na vituo vya mafuta kila mkoa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/272f89daef9f37af0d2657a3e594e86b.jpg

Rais Samia Suluhu Hassan, ametajwa kuwa miongoni ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi