loader
Tutumie mvua  hizi kwa kilimo,  tukichukua tahadhari

Tutumie mvua hizi kwa kilimo, tukichukua tahadhari

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la kuendelea kunyesha mvua katika maeneo ya Ukanda wa Pwani ikiwamo Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, mvua hizi zinazonyesha katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, zitaendelea mpaka mwishoni mwa mwezi huu, huku kukiwa na upungufu wa mvua Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Ukanda wa Ziwa Zictoria.

Kunyesha kwa mvua hizi ni baraka ambayo wakulima katika maeneo hayo wanatakiwa kuitumia kupanda mazao mengi ili kupata chakula cha kutosha na kujihadhari na uhaba wa chakula unaoweza kutokea katika maeneo ambayo yatakosa na mvua na kukabiliwa na ukame.

Rai yetu kwa wakulima ni kwamba, watumie mvua hizi kupanda mazao mbalimbali hasa yanayokomaa haraka ili endapo kutatokea uhaba wa chakula huko mbele, tuweze kuwa na akiba ya chakula kwa ajili ya kutumia wakati huo.

Aidha, tunaikumbusha jamii na mamlaka mbalimbali kuchukua tahadhari ya kuzuia au kupunguza maafa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.

Tunawasihi wananchi hasa wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata. Pia tunazishauri mamlaka husika zikiwamo halmashauri na manispaa kuhakikisha mitaro, mito na mifereji yote hasa inayopita katika makazi ya watu na kando ya miundombinu ya barabara inakuwa safi ili maji ya mvua yaweze kupita kwa kurahisi na kutosababisha mafuriko.

Tunasema hivyo kwa kutambua kuwa, mara nyingi mvua kubwa zinaponyesha zinaleta athari mbalimbali kama vile mafuriko katika makazi ya watu, uharibifu wa miundombinu, makazi na mazao mashambani na wakati mwingine vifo kwa binadamu na wanyama.

Tumekuwa mashuhuda mara nyingi mvua zinaponyesha hali ya miundombinu hasa katika miji mikubwa inakuwa mbaya, maji yanafurika hadi barabarani na kusababisha dhiki ya usafiri.

Aidha, serikali ihakikishe mvua hizi zinatumiwa vizuri kwa kuweka usimamizi na utaribu mzuri utakaohakikisha mabwawa ya kuzalisha umeme yanapata maji ya kutosha kwa kuhakikisha mapito ya maji kuelekea katika mabwawa hayo yapo vizuri, pamoja na kuwa na uhifadhi mzuri wa maji yanayoingia kwenye mabwawa hayo ili yasipotee kirahisi.

Wananchi kwa upande wetu, tuwe na utamaduni wa kuhakikisha maeneo yetu tunayoishi ni safi na salama hasa kipindi kama hiki cha msimu wa mvua ili kuepuka mafuriko na magonjwa ya mlipuko.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6e3fe5ce197363ef4a52f1491d71fc98.PNG

JUMATATU Mei 09, mwaka huu, lilifunguliwa Kongamano ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi