loader
WAZO LANGU: Tusafishe mitaro kuepuka magonjwa ya kuambukiza

WAZO LANGU: Tusafishe mitaro kuepuka magonjwa ya kuambukiza

MITARO mingi katika Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ikijaa maji katika kipindi cha mvua na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.

Katika eneo la katikati ya mji kuna maeneo kama Kamata, Akiba, Msimbazi na mengine ambayo yamekuwa yakijaa maji na kusababisha kero kubwa kwa wasafiri.

Mitaro katika mkoa huo inahitaji usafi shirikishi baina ya mamlaka zinazosimamia ujenzi wa mitaro, mamlaka zinazosimamia usafi wa mji pamoja na wananchi ili kuhakikisha kuwa maji yanapita wakati wote hususani katika kipindi hiki cha mvua.

Pia katika maeneo ya nje ya mji kama Mtava, Tazara, Karakana na katika maeneo mengi ya mji yamekuwa yakijaa maji na kusababisha usumbufu mkubwa kwa vyombo vya usafiri na wananchi kwa ujumla.

Kupitia usafi shirikishi mitaro mingi inaweza kufunguka na kuleta hewa nzuri kama maeneo ya Banana ambapo mitaro yake imetuamisha maji hadi yanatoa harufu mbaya na kuwa kero kwa wasafiri na wafanyabiashara wa eneo hilo.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga aliwahi kusema mitaro mingi katika Mkoa wa Dar es Salaam haitiririshi maji kama inavyotakiwa kutokana na kujaa michanga pamoja na wananchi kutupa takataka ndani ya mitaro badala ya kupeleka katika sehemu stahili.

Alisema changamoto kubwa katika Mkoa wa Dar es Salaam ni kwa wananchi kugeuza mitaro ya barabara kuwa kama dampo. Aliongeza kuwa katika kuisafisha mitaro hiyo, Tarura na Tanroads wanashirikiana na Idara ya Usafi na Mazingira ambayo ina majukumu ya kuhakikisha masuala ya usafi na mazingira.

Alisema mitaro yote inayozibwa na mchanga kutokana na mvua inazibuliwa na kusafishwa na Tarura kama barabara ipo chini yake na Tanroads kama barabara hiyo ipo chini ya Tanroads.

Kazi ya Tarura na Tanroads ni kuitunza mitaro kwa maana ya kuizibua ikiwa imejaa mchanga baada ya mvua kunyesha au kuirekebisha ikiwa imeharibika lakini uchafu wowote ndani ya mitaro kwanza wananchi wanapaswa kusafisha mita tano katika eneo lake kwa kushirikiana na idara ya usafi na mazingira ya mkoa.

Hili ni jambo jema la kuwashirikisha wananchi pamoja na idara husika katika kufanya usafi na kuweka mitaro ya Mkoa wa Dar es Salaam katika hali ya usafi ili kuepusha kipindi cha mvua kuleta balaa katika makazi ya watu kutokana na mitaro hiyo kuzibwa na uchafu na matope.

Ni vizuri kila mwananchi kuwa macho na vyanzo vinavyosababisha mitaro kuziba ikiwamo kutupa takataka kwenye mitaro kwa kufanya usafi kama alivyoshauri Mkinga kwamba kila mwananchi afanye usafi mita tano za mfereji kutoka katika makazi yake.

Mratibu wa Magonjwa ya Kuambukiza Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam, Mkamba Alex alikiri kuwa mitaro mingi ya maji ya mvua ambayo haina uangalizi wa karibu inaishia kuwa na mlundikano wa takataka na maji machafu na kugeuka kuwa himaya ya panya na wadudu wengine.

Alisema mitaro yenye kutuamisha maji kwa muda mrefu inasababisha madhara kwa afya ya wananchi pia kama vile kusababisha magonjwa ya malaria, kuhara na kuhara damu, ngozi, mzio, kipindupindu na kujikuna.

Ikiwa serikali itatilia mkazo wa usafi shirikishi katika Mkoa wa Dar es Salaam, ni rahisi kuyafikia malengo ya kuufanya mkoa kushika nafasi ya kwanza kwa usafi barani Afrika kutimia, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Jiji la Kigali nchini Rwanda.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5503ded9b8d60b01e35a2b2c4bd02922.JPG

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi