loader
JESSICA MSHAMA: Mrembo mwenye talanta kibao

JESSICA MSHAMA: Mrembo mwenye talanta kibao

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi za chini na leo wamekuwa ni miongoni mwa watu mashuhuri kutokana na kile wanachokifanya kwenye jamii kibiashara na kuwavutia wengine wanaotamani kuthubutu kuwa kama wao.

Bakhresa ni mfanyabiashara mkubwa mwenye viwanda vingi na amejiwekeza katika sekta mbalimbali nchini na kuajiri wafanyakazi wengi wa ndani na nje ya nchi.

Pia, wapo wengine mashuhuri kama Mohamed Dewji na wengine wasiojitangaza lakini kwa namna moja au nyingine kile wanachokifanya kwenye jamii ya Tanzania wengi wanatamani kuwa kama wao. Hata hivyo, ili kuwa kama wao ni lazima kwanza kujifunza wao walifanya nini, kutengeneza mawazo chanya ya kibiashara, kutafuta mitaji na kuyafanyia kivitendo.

Hakuna jambo lisilowezekana kama mtu ukiamua jambo la muhimu ni kuangalia ndoto yako na kuchukua hatua. Miongoni mwa vijana mwenye ndoto za kuwa kama wafanyabiashara hao mashuhuri ni Jessica Mshama. Gazeti hili lilipata nafasi ya kufanya mahojiano na msichana huyu baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu na kuona mapambano yake namna alivyo na vipaji vingi na maono yake yanakoelekea.

Jessica ni mtoto wa nne katika familia ya Julius na Assumpta Mshama aliyezaliwa miaka 26 iliyopita. Msichana huyu ni maarufu kwani alianza kujitengenezea jina lake kupitia kundi la muziki wa injili maarufu kama J Sisters.

Bila shaka wale mashabiki na wapenzi wa muziki huo wanafahamu vizuri kwani walianza kuimba wakiwa bado ni wasichana wadogo. Leo hii ukiwatazama wasichana hawa wamekuwa ni wadada wakubwa na wengine wameshaolewa lakini Jessica ni msichana ambaye anaendelea na harakati nyingine za maendeleo ndani ya familia. VIPAJI Unaweza kusema ni msichana mwenye vipaji vingi kwanza ni mjasiriamali, muimbaji wa muziki, mwanasiasa anayejaribu kufuata mienendo ya mama yake mzazi, Assumpta Mshama.

Katika nafasi yake ya ujasiriamali amekuwa akifanya vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongoza familia yake, kwa kile anachoeleza ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupangilia mambo.

BIASHARA

Anasema yeye na ndugu zake walianzisha biashara ya duka kubwa maarufu kama Super Market yenye bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuendesha maisha yao na waliajiri vijana wengi. Pamoja na kusimamia biashara hiyo kama kiongozi mkuu, maono yake ni kufika mbali zaidi ya hapo. Mbali na duka, kuna shule waliyoianzisha ya msingi inayofundisha masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) na yeye ndiye Mkurugenzi Mkuu akijitahidi kutimiza maono yake.

“Assumpta Digital School ni shule ya kwanza inayohamasisha matumizi ya teknolojia kwa watoto na mandhari ya kuwafundisha watoto katika malezi na mazingira bora, kumjua Mungu na kuwa na elimu ya kujitegemea. Nimeajiri vijana zaidi ya 20 walimu na wafanyakazi wengine, tunaamini mambo yakiwa sawa, biashara zikirudi katika hali nzuri zikaboreshwa tunaweza kuajiri watu wengi zaidi.

“Najiona kuwa na miradi mingine itakayoajiri watu wengi zaidi kuanzia 100,000 au 50,000, hayo ni malengo niliyoyaweka namuomba Mungu kutimiza kile nilichokusudia kufika mbali.

Tunatamani kuwa kama Bakhresa au Mo lakini kwa lengo kuwasaidia vijana wenzangu. Ukiona mtu kama Mo anaajiri watu takribani laki mbili au tatu hiyo ni idadi ya watu wengi sana kwa hiyo anasaidia jamii sana hata sisi itafika mahali tutafikia huko,” alisema.

Hata hivyo, anasema bado wana safari ndefu lakini inafikika na kuwa matumaini yapo kama sasa hivi anaona wawekezaji wanakuja nchini kuna nafuu kwa taifa na hata vijana wanaweza kufanya fursa nyingi za kibiashara. Anasema kwa hali halisi ilivyo nchini bado fursa za kifedha ni ndogo kwani hakuna madawati ya vijana kwenye mabenki.

“Kijana anaongezewa riba, atafute ‘bank statement’ halafu makato, bado serikali ina kazi kubwa kuwezesha vijana kiuchumi. Tunahitaji tuwezeshwe, kufikia malengo tuliyojiwekea kama vijana,” anasema. Lakini pia, Jessica ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Nakua na Taifa langu ambapo amekuwa akiwasaidia vijana kupata ajira.

Si hayo tu, bali amekuwa akiwasaidia wajasiriamali vijana kuendesha miradi yao kwa kuwapa semina na kuwatafuta watu ambao wanaweza kuwasaidia kuvuka na kwenda hatua nyingine. Anasema elimu ya ujasiriamali imewasaidia vijana wengi kusimamia biashara zao kikamilifu.

SIASA

Ukiachilia mbali masuala ya biashara, Jessica amekuwa akijihusisha na siasa kidogo na amekuwa akionekana kwenye majukwaa mbalimbali ya kitaifa. Kuingia kwake kwenye siasa sio kwa kubahatisha bali anaonekana wazi kufuata nyayo za mama yake mzazi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nkenge miaka iliyopita. Ukiacha historia ya siasa ya mzazi wake huyo, yeye mwenyewe anasema anajivunia kwa sababu amekuwa akichaguliwa kiongozi tangu akiwa anasoma shule ya msingi hadi Chuo Kikuu.

Waswahili hupenda kusema nyota njema huonekana mapema na dalili za mvua ni mawingu. Ndivyo ambavyo hata kwake msichana huyo mambo yanaonekana wazi kuwa kama sio sasa huenda baadaye atakuja kuonekana kwenye majukwaa makubwa ya kisiasa. Ingawa bado ni msichana mwenye bahati unaweza kusema hivyo, kwa sababu ni kiongozi katika kona tofauti, anakubalika kwa vijana wenzake na amekuwa akichaguliwa kama balozi kwenye taasisi mbalimbali. Anasema: “Wito wangu ndani ya siasa umetokana na historia binafsi tangu nikiwa mdogo.

Nakumbuka wakati nasoma shule ya msingi nilichaguliwa kuwa kiranja na sekondari nilikuwa kiranja katika sekta mbalimbali na chuo vile vile nilikuwa Waziri wa Fedha wa nchi za kigeni.”

“Baada ya hapo nikaja kuwa kiongozi kwenye biashara za familia kwa hiyo nimekuwa na wito wa kupata nafasi mbalimbali za uongozi na nilipoona kuwa ninaweza kufanya jambo kwa ajili ya jamii yangu ndio maana nikapenda sana kusaidia vijana wa rika langu,” anasema.

Siasa nimekuwa nikijihusisha kidogo hata kama sina nafasi lakini kwa uwezo wangu kusaidia vijana. Napenda sana uongozi nikiamini vijana ni nguvu ya taifa kwa hiyo lazima tusaidiane kwa pamoja ili kuweza kuonesha umahiri wa hizo nguvu kwa taifa,” anasema. Unajua kuwa katika uchaguzi mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ngazi za vijana kuwa aliwahi kugombea nafasi ya ubunge?

Ndivyo ilivyo ila anasema alishika nafasi ya pili. “Niligombea ubunge mwaka 2020 kupitia umoja wa vijana CCM nikawa mtu wa pili. Licha ya kwamba sikushinda lakini ni kitu ambacho kinanifanya nijivunie uthubutu niliouonesha kwa vijana wenzangu, naamini ipo siku kwa sababu nimejifunza mengi,” anasema.

Jessica anasema kwenye siasa kuna mambo mengi ila kikubwa ni kujua malengo yake na kujitathmini lakini pia, kumuomba Mungu akuongoze na yeye kama msichana anasema kuna changamoto ameziona katika harakati zake hizo za kutafuta uongozi ngazi ya siasa na amejifunza namna ya kuzikabili.

“Changamoto zipo kama binti wa kike. Kwa mfano rushwa ya ngono zipo, kupata nafasi labda uhonge kwa hiyo ni vitu hatarishi, tunapambana navyo na uko pale kwa ajili ya kusudi la Mungu, naamini hivyo vingine vinakuja kama majaribu. Na sisi kama Wakristo lazima tuepuke majaribu mengine huku tukiendelea kupambana na mambo mengine,” anasema.

Ukiachana na masuala ya siasa, Jessica anajivunia kuchaguliwa kuwa Balozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akisema ni jambo linalotia moyo kuona namna vijana wanathaminiwa na kuaminiwa kupewa nafasi kubwa kama hiyo.

Amekuwa akitumia nafasi yake kutembelea vijana mbalimbali na kuwaeleza umuhimu wa jumuiya hiyo lakini pia kuangalia namna vijana wa ukanda huo wanavyojishughulisha na miradi mbalimbali ya kiuchumi inayosaidia kuleta maendeleo katika nchi.

Anasema kitendo cha kupewa nafasi katika ngazi mbalimbali za kitaifa kunawafanya kuona namna gani wanathaminiwa na ni chachu ya maendeleo kwani inawapa hamasa vijana wengine kutamani kuwa kama yeye, kutamani kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo, kufanya miradi ya kiuchumi kwa faida yao na taifa. Jessica anasema kuonekana kwake na kupata fursa kitaifa na hata kimataifa hana budi kushukuru wale wote wanaotambua michango ya vijana wanaojituma na wenye maono makubwa.

“Fursa kama hizi zinawavuta vijana wengine lakini pia, tunapofanya vizuri tunawaaminisha na wengine wataendelea kutoa fursa kwa kuona tunaweza kufanya mambo makubwa katika jamii yetu,” anasema.

Licha ya juhudi zake kuonekana namna anavyotumia fursa kuwaelimisha wengine kwa maana ya elimu na fursa kwa kile kipaji alichonacho anasema kuna changamoto ya kutoaminiwa na jamii.

Anasema kuna watu hawana imani na vijana na wengine ni watu wa kugeuka kwa kutokuwaamini. “Lazima tuoneshe dunia kama tunaweza kutenda au kuongoza vyema kwa hekima na busara kuondoa ule mtizamo au dhana mbaya kwamba vijana hawawezi,” anasema.

SANAA

Kipaji kingine alichonacho msichana huyu ni mwanamuziki. Wakiwa wadada wanne waliozaliwa pamoja. Kundi hilo kwa sasa limepoteza umaarufu kidogo tofauti na hapo nyuma kwa sababu wametengana kwa maana ndugu zake mapacha wawili wanaishi nchini Marekani na wawili wanaishi Tanzania.

Jessica anasema licha ya kutengana bado wanaendelea kufanya muziki wa injili lakini ili kudumisha kundi lao wanapotaka kufanya wimbo wa pamoja walioko nchini wanarekodi sauti kwa wale wa Marekani wanatuma kwao na kuchanganya.

Anasema umbali dhidi ya wenzao unawaathiri kidogo lakini bado wanaendeleza kueneza neno kupitia nyimbo. “Tuliopo hapa nyumbani ni wawili, tumekuwa tukifanya kazi kwa kuunganisha sauti na halafu nyimbo zinatungwa.” Jessica anasema kwa sasa wana wimbo walioachia hivi karibuni unaitwa ni wewe na kuna mwingine wamefanya kwa kushirikiana na msanii wa muziki wa injili nchini, Walter Chilambo

. Gazeti hili lilimuuliza kama ana mpango wa baadaye wa kuingia katika muziki wa Bongo Fleva naye anasema: “Sijawahi kufikiria kuingia katika muziki huo kwa sababu sina matamanio hayo lakini bado naona nina wito mkubwa katika muziki wa injili hata kama dada zangu hawapo. Kiu yangu ya kuimba kupitia muziki wa injili bado iko pale pale kwasababu ninajua bado tuna kazi ya kufikisha ujumbe wa Kristo kupitia uimbaji.”

Anasema tangu wameanza muziki wana albamu tatu na wanakusudia kutoa albamu ya nne kabla mwaka haujaisha. HISTORIA YAKE Jessica ni msichana mwenye elimu ya Shahada ya Masuala ya Fedha aliyopata Chuo Kikuu cha Catholic Eastern Afrika (Kenya).

Pia, ana Stashahada ya Usimamizi wa Biashara, Post Graduate Diploma in International Economics Diplomacy aliyosoma Centre of Foreign Relations. Aliwahi kufanya kazi katika ofisi za Mohamed Enterprise kama Ofisa Rasilimali watu mwaka 2017 hadi 2018

TUZO

Ameshawahi kupata tuzo mbalimbali ikiwemo ya Mjasiriamali Bora Afrika, Leadership Luxury University London, Export Strategy Planning By European Union under International Trade Centre, Africa Next champion- African Union and United Nation Officer, Mwanachama Un Club, Malkia wa nguvu na nyingine zaidi ya 10 kutoka mashirika ya ndani na nje ya nchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/622093e185679558f9e0ad9bb33bed21.PNG

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi