loader
Tanzania, Sudan Kusini, Rwanda zafaidi ufadhili wa masomo IUCEA

Tanzania, Sudan Kusini, Rwanda zafaidi ufadhili wa masomo IUCEA

BARAZA la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) limetoa ufadhili wa masomo kwa waombaji 63 kati ya 1,450 walioomba ufadhili kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huku Rwanda, Sudan Kusini na Tanzania zikiwa na idadi kubwa.

Taarifa iliyolifikia HabariLEO Afrika Mashariki mwishoni mwa wiki kutoka IUCEA yenye makao yake Kampala nchini Uganda kupitia Sekretarieti ya EAC yenye makao yake Arusha Tanzania, ilibainisha kuwa, wanufaika 22 sawa na asilimia 35 ya wanufaika wote 63 katika awamu hii ya tatu ya ufadhili ni wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nchi za Sudan Kusini, Tanzania na Rwanda zimepata ufadhili kwa wanafunzi 11 kila nchi huku Kenya, Uganda na Burundi zikipata nafasi kwa wanafunzi kumi kila nchi.

Vyuo vikuu wanavyokwenda kusoma wanufaika hao na nchi vilipo kwenye mabano ni Chuo Kikuu cha Kenyatta, Chuo Kikuu cha Kibabii, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Dedan Kimathi na Chuo Kikuu cha Nairobi (Kenya).

Nchini Tanzania ni Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Vingine ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbarara, Chuo Kikuu cha Kyambogo na Chuo Kikuu cha Makerere (Uganda) pamoja na Taasisi ya Elimu ya Juu Ruhengeri- INES Ruhengeri nchini Rwanda.

“Tangu kuanzishwa kwa mpango huo wa ufadhili Aprili 2018,” taarifa inasema: “IUCEA imetoa tuzo (ufadhili) wa masomo kwa wanafunzi 180. Tuzo hizo zinawezekana kupitia fedha zinazotolewa na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia KfW, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi waliotunukiwa kutoka nchi zote wanachama wa EAC watafuatilia masomo yao ya uzamili katika maeneo yaliyochaguliwa ya mada ya Hisabati, Informatics, Uhandisi, Sayansi, Teknolojia na Sayansi ya Biashara katika nchi nyingine yoyote ya EAC.”

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi