loader
Wanawake EAC wekeni mikakati kuinuana kiuchumi

Wanawake EAC wekeni mikakati kuinuana kiuchumi

LEO Machi 8, ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Tanzania inafikia kilele hiki baada ya kufanyika kwa shughuli mbalimbali na makongamano kujadili na kuonesha mambo yanayomkabili mwanamke na mafanikio yake.

Kaulimbiu ya maadhimisho haya ni “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu” inayolenga kuhamasisha uwajibikaji kwa wote ili kuleta usawa wa kijinsia na kukumbushana umuhimu wa usawa wa kijinsia katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo jumuishi na endelevu.

Usawa wa kijinsia ni miongoni mwa mambo makubwa ambayo wanawake wameendelea kupigania ili kuweka uwiano kati ya wanaume na wanawake katika ushiriki kamili wa masuala ya uongozi kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inaelezwa kuwa, viwanda vya nyumbani, vidogo na vya kati vinachangia maendeleo ya kiuchumi EAC kwa asilimia 90 ya wafanyabiashara.

Aidha, sekta hiyo inachangia asilimia 80 ya ajira hususani miongoni kwa vijana na wanawake hivyo ni sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi za EAC; Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Ukiangalia maonesho mbalimbali ya nchi za EAC, utagundua kuwa, wajasiriamali wengi ni wanawake hivyo, wanatakiwa kujengewa mazingira bora kufanya shughuli zao bila vikwazo.

Maadhimisho haya yanatoa nafasi kwa EAC na watendaji wake kuangalia kwa undani namna ya kumsaidia mwanamke katika EAC ili amudu biashara zake kwa kutunga sera na sheria madhubuti, rafiki na wezeshi.

Inaelezwa kuwa, karibu asilimia 68 ya wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara maeneo ya mipakani, hutegemea biashara hiyo kama shughuli za msingi za kiuchumi. Hata hivyo, bado wanakumbana na changamoto mbalimbali zinazopaswa kufanyiwa kazi.

Licha ya EAC kusaidia kuwezesha wanawake, ni muhimu wanawake EAC kushirikiana kibiashara na kuhakikisha mjasiriamali wa nchi moja anauza bidhaa za mwenzake wa nchi nyingine ili kuinuana kiuchumi. Hii iondoe mazoea ya wanawake wengi wajasiriamali kusubiri maonesho katika nchi nyingine ili kuonesha bidhaa na huduma zao.

Ndio maana ninasema, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatumike pia kubadili fikra zao kutoka mtu kuuza bidhaa zake nyumbani na kusubiri tu maonesho, hadi kufikia wajasiriamali wanawake wa nchi moja na nyingine kushirikiana kwa kuuziana na kubadilishana biashara katika nchi nyingine.

Ili hili lifanikiwe, hapana budi kujenga ushirikiano kupitia vyama vya wajasiriamali wanawake ndani ya nchi za EAC vitakavyosaidia kukamata fursa mbalimbali zinazojitokeza ndani na nje ya EAC.

Kufanikisha hili, ubora wa bidhaa na huduma lazima upewe kipaumbele ili kukamata soko kimataifa. Ninatoa rai maadhimisho haya yaunganishe wanawake na jamii kupiga vita aina zote za unyanyasaji, ubaguzi na ukatili wa kijinsia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a26c931e754e19cc27f1e247c0211ba6.PNG

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi