loader
Tujipange kutumia vyema mkutano wa utalii wa UNWTO

Tujipange kutumia vyema mkutano wa utalii wa UNWTO

SEKTA ya utalii ina umuhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Kutokana na umuhimu wake, watendaji serikalini wamekuwa wakifanya kila juhudi ili kuimarisha utalii nchini kwa kusimamia ipasavyo mikakati ya kukuza vivutio mbalimbali vya utalii vikiwemo hifadhi za wanyama, maporomoko ya maji, milima, misitu ya mazingira asilia, utamaduni, fukwe na malikale.

Pamoja na kuwapo kwa mafanikio ya kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia 1,510,151 mwaka 2019 kutokana na kuitangaza sekta ya utalii kikanda na kimataifa, serikali imekuwa ikijipanga kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo ili kuwapo na watalii wengi zaidi pamoja na kuwapo kwa majanga mbalimbali ya kidunia ikiwamo ugonjwa wa Covid-19.

Ibara ya 67 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025, serikali imeelekezwa kubuni na kutekeleza mikakati ya kuongeza na kukuza wigo wa bidhaa/ mazao ya utalii ili kufikia watalii milioni tano kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Lengo kubwa la elekezo hilo ni kuhakikisha kwamba taifa linaongeza mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 zilizofikiwa mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 6.0 mwaka 2025. Katika kufanikisha hilo pamoja na mambo mengine serikali ilielekezwa kukuza utalii wa mikutano, ambapo pamoja na Tanzania kujitangaza na kutangaza vivutio vyake itakuwa inaweka msingi wa mipango ijayo ya utalii duniani.

Ndio maana tunapongeza juhudi zilizofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuweza kusaini rasmi mkataba wa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa utalii wa 65 wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya utalii duniani (UNWTO).

Tunaamini mkataba huo uliotiwa saini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro na UNWTO katika Makao Makuu ya shirika hilo jijini Madrid nchini Hispania jana, kuwezesha mkutano kufanyika Oktoba 5 hadi 7, mwaka huu jijini Arusha, utakuwa chachu kubwa katika utekelezaji wa lengo la kuongeza watalii kufikia milioni tano katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Pamoja na kutoa hongera kwa wizara kwani mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na mawaziri wote wa utalii wa Bara la Afrika pamoja na wabobezi wa kutangaza utalii na wataalamu wa masuala ya utalii kutoka nchi mbalimbali duniani, tunapenda kuwaomba wadau wote wa utalii nchini kujiandaa vyema kuweka heshima ya nchi na pia kukamata fursa zinazoambatana nazo.

Ni kweli kama alivyosema Dk Ndumbaro kuwa mkutano huo ni fursa kwa wadau wa utalii nchini Tanzania hivyo ni vizuri kukaa katika mkao wa kula. Ni dhahiri kuwa tumepewa heshima kubwa ya kuwa wenyeji wa mkutano huu ambao utafungua milango ya vivutio vyetu vya utalii kujulikana duniani kote, kinachotakiwa sasa ni kujitambua na kupambana kutoa huduma za msingi na kujifunza namna ya kuendesha utalii hasa wakati huu wa Covid-19.

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi