loader
Hongera Rais Samia, kazi imeonekana

Hongera Rais Samia, kazi imeonekana

LEO umetimia mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipokabidhiwa madaraka ya kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na kifo cha Dk John Magufuli, Machi 17, 2021.

Aliapishwa Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Awamu ya Sita, na ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake, Tanzania imeendelea kuwa nchi ya mfano duniani na imeendelea kushuhudia hatua kubwa za kimaendeleo.

Aprili 22, 2021 akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, Rais Samia alilieleza Bunge pamoja na Watanzania kuwa Dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.

Katika mwaka mmoja wa uongozi wake, mambo hayo matatu aliyoyaahidi, yamedhihirika kwa vitendo kutokana na namna serikali inavyowaletea maendeleo Watanzania kwa kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema na kuleta mengine mapya. Katika hilo, pia amefanikisha kukamilisha baadhi ya miradi iliyokuwa imeanzishwa na watangulizi wake na hasa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Hivi karibuni, Rais Samia amekamilisha ujenzi wa Daraja la Tanzanite katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na madaraja mengine na baadhi ya barabara nchini.

Ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia, Watanzania na dunia imeshuhudia akiifungua Tanzania katika ushirikiano na majirani zake na dunia kwa ujumla, kiasi kwamba amewezesha kupatikana kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo ndani ya muda mfupi aliokaa madarakani.

Watanzania ni mashahidi wa fedha za mapambano ya Covid- 19 na ustawi wa wananchi Sh trilioni 1.3 zilivyobadili maisha katika sekta mbalimbali zikiwamo za kijamii za maji, elimu, afya, barabara hadi nyingine za usafirishaji, ujenzi na utalii.

Leo hii watoto wa Kitanzania walioko shule karibu wote wako katika madarasa mazuri, madawati mazuri, maabara bora, lakini kubwa zaidi wasichana waliopata ujauzito wameanza kurejea shuleni ili kutimiza ndoto za maisha yao kutokana na kazi kubwa ya Rais Samia.

Katika uchumi, Serikali ya Rais Samia imeendelea kufanya mageuzi makubwa ambayo yamesaidia kuufanya uchumi wa Tanzania kuendelea kuimarika, huku akipongezwa kwa jinsi serikali yake ilivyovunja rekodi kwa kutekeleza bajeti kwa asilimia 60.5 ndani ya miezi sita.

Kwa hakika, mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, umedhihirisha azma yake ya kuwasaidia Watanzania wenzake kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Aliyofanya ni makubwa sana ambayo hayatoshi kuelezwa katika safu hii, lakini mengi yamebebwa ndani ya toleo letu la leo, ambalo limesheheni ushuhuda wa mambo hayo kutoka kwa wale waliyoyatekeleza na wale waliofaidika nayo wakiwamo Watanzania wenyewe.

Kwetu sisi tumekopa maneno ya vijana mtaani ambako wanasikika wakisema ‘Mama ameupiga mwingi’, nasi tunaungana nao tukisema Hongera Rais Samia. Umeupiga mwingi na Kazi Iendelee.

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi