loader
Kishindo cha Samia mwaka mmoja

Kishindo cha Samia mwaka mmoja

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ni ule usemao “Kila Zama na Kitabu chake.” Msemo huu una mantiki kubwa kwa siasa za nchi hii ambayo pamoja na mambo mengine, imejengwa katika mtindo wa kubadilishana uongozi kwa njia ya amani kutoka awamu moja hadi nyingine.

Katika awamu zote kuanzia Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Awamu ya Pili ya Rais Mwinyi, Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli na sasa Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuna mambo mengi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yamefanyika.

Akiwa anatimiza mwaka mmoja leo tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania, Machi 19 mwaka jana, Samia ameifungua nchi katika sekta zote zikiwemo za uchumi, siasa na kijamii. Kiuchumi amevutia uwekezaji wenye thamani ya Sh trilioni 37. Thamani hii ya uwekezaji imetokana na juhudi za Serikali ya Rais Samia kusajili jumla ya miradi 294 ya uwekezaji ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 8,129.3 (sawa na Sh trilioni 18.75) ambayo imesajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Aidha, kupitia Maonesho ya Biashara ya Dubai Expo 2020 mwaka huu, Tanzania imesaini hati za makubaliano 37 za uwekezaji na nchi mbalimbali za thamani ya Dola za Marekani bilioni nane sawa na Sh trilioni 18.5.

Sambamba na kuvutia uwekezaji kutoka nje, pia serikali yake imeweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa ndani na kuwafanya waliofunga biashara zao kuzifungua tena kutokana na kuhakikishiwa usalama wao na wa biashara zao, kuweka utaratibu mzuri kwa TRA kukusanya kodi halali na si za dhuluma hali inayofanya mapato kuongezeka mwezi hadi mwezi. Kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa, Rais Samia amefanya ziara katika nchi mbalimbali kwa lengo la kukuza ushirikiano na mataifa hayo pamoja na kuvutia biashara na uwekezaji. Nchi ambazo amezitembelea ni pamoja na Kenya ambako pamoja na mambo mengine amesaini mikataba na kuondoa baadhi ya vikwazo vya kibiashara visivyo vya kikodi, amekwenda Uganda na kusaini mkataba na taifa hilo kuhusu utekelezaji wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, pia amezuru Rwanda, Msumbiji, Burundi na Misri.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, Rais Samia pia amefanya ziara katika nchi za Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kufanya ziara ya kikazi katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji kwa lengo la kuimarisha uhusiano na nchi hizo na kuhamasisha wawekezaji kuja nchini.

Mafanikio ya ziara hizi za Rais Samia ni mengi, lakini moja ya mafanikio hayo kwa Tanzania ni kupokea mkopo wa masharti nafuu wa Sh trilioni 1.3 kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambazo serikali imezielekeza kwenye utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za Covid-19 ukiwemo ujenzi wa madarasa 15,000.

Ili kuhakikisha elimu ya Tanzania inakuwa bora zaidi na kukidhi mahitaji halisi ya nchi, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuboresha mtaala wa elimu kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali na kamati maalumu imeundwa hivi sasa kazi inaendelea. Pia serikali yake pamoja na kuendelea kuboresha elimu kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu, pia imeamua kuwapa tena nafasi wanafunzi waliopata changamoto mbalimbali na kushindwa kuendelea na masomo yao ikiwemo ujauzito, utoro na kufeli mtihani wa darasa la saba kurudi shule na kuendelea na masomo. Serikali ya Samia imeendelea kuimarisha huduma za afya za kibingwa katika kipindi cha mwaka mmoja Huduma hizi ni pamoja na upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu, upandikizaji uloto, matibabu ya kisasa ya saratani, ya moyo katika hospitali za rufaa zilizopo nchini. Mara kadhaa amesema kuwa huduma hizi ni msaada si tu kwa Watanzania, bali hata na nchi nyingine ambapo watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wanakuja kutibiwa nchini na kukuza utalii wa kimatibabu.

Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuikamilisha. Miradi hii ni pamoja na upanuzi wa Barabara ya Morogoro njia nane kutoka Kimara, Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani ambayo sasa madaraja ya juu mawili yanajengwa eneo la Mbezi Mwisho ili kuondoa foleni, Barabara ya Mwendokasi kutoka Mbagala hadi Gerezani, Kariakoo. Zimo pia Barabara ya Kakonko-Kibondo- Kasulu, Kasulu-Buhigwe- Manyovu, Kabingo- Kasulu-Manyovu, Nanganga-Ruangwa, Kidatu-Ifakara, Daraja la Kigongo-Busisi, mkoani Mwanza, Daraja la Wami, mkoani Pwani, Tanzanite la jijini Dar es Salaam ambalo limekamilika linasubiri kuzinduliwa tu.

Watanzania wameshuhudia miradi yote hii ikiendelezwa na Rais Samia na hakuna mradi utakaobaki nyuma kama inavyodhihirika katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Serikali ya Awamu ya Sita pia inakamilisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, inajenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, Dodoma huku viwanja vya Tabora, Sumbawanga, Shinyanga na Kigoma vilivyokuwa vimesimama, sasa vimepewa msukumo mkubwa wa kuanza kujengwa ili kuimarisha na sekta ya usafiri wa anga ambayo ni muhimu kwa uchumi hasa utalii.

Kwa kuwa Rais Samia ameshirikia kwa asilimia 100 kwenye kurekodi kipindi kitakachotangaza utalii, biashara na uwekezaji hapa nchini kinachojulikanacho kama ‘The Royal Tour’, hivyo hatua yake ya kuimarisha viwanja vya ndege ni muhimu kwa kuwa kipindi hiki kitavutia watalii wengi kuja Tanzania. Miradi ya kimkakati ya Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) nayo imeendelea kushika kasi chini ya Rais Samia. Wakati anahojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Samia amesema ataendeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo wa SGR. Wakati anapokea kijiti cha kuongoza nchi, mradi wa SGR ulikuwa kwenye lot3 yaani Dar es Salaam-Morogoro, Morogoro-Dodoma- Makutupora (Singida).

Pamoja na kuendelea na ujenzi wa lot hizi tatu, pia ameanza ujenzi wa kipande cha SGR kutoka Makutupora- Tabora, Isaka-Mwanza wakati kipande cha Tabora-Mwanza kimeshatangazwa na shughuli za manunuzi zinaendelea na lot6 kutoka Tabora hadi Kigoma itatangazwa hivi karibuni huku ujenzi wa JNHPP aliupokea ukiwa asilimia 46 sasa ameufikisha asilimia 58.

Madini nayo ni sekta iliyopewa kipaumbele cha pekee na Rais Samia ambapo katika mwaka wake mmoja sekta hiyo imeweka historia kwa kushuhudia mauzo ya moja kwa moja ya thamani ya Sh trilioni 8.3. Mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi mzuri wa serikali yake. Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nazo zimeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia. Mafanikio hayo katika sekta ya kilimo ni pamoja na kuimarika kwa shughuli za utafiti, uzalishaji mbegu, huduma za ugani, masoko na kilimo cha umwagiliaji.

Katika kilimo kinachochukua asilimia kubwa ya ardhi, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, zimesuluhisha na kumaliza migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji. Kwenye sekta ya mifugo na uvuvi baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ya utafiti na ushauri kwa wafugaji kupitia Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA).

Kisiasa Samia amefanikiwa kuwafanya Watanzania kuwa na amani na utulivu katika kipindi chote cha mwaka mmoja huku akiimarisha demokrasia kwa kujenga siasa za kuvumiliana na maridhiano.

Baada ya kuzungumza na Wadau wa Demokrasia nchini (TCD) vikiwemo vyama vya siasa jijini Dodoma, Desemba mwaka jana, Samia aliteua Kikosi Kazi kwa ajili ya kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano huo wa wadau wa demokrasi.

Kikosi kazi hicho kimemaliza kazi yake na kuwasilisha taarifa yao kwa Rais hivi karibuni, hatua iliyomfanya Rais Samia kumtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Hatua hii ni kubwa kwani kwa miaka mitano kukuwahi kuwa na mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa vyama vya upinzani nchini.

Katika kuonesha dhamira yake ya kuwa na siasa zenye maridhiano, Samia pia amekutana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Ikulu Dar es Salaam siku alipofutiwa mashitaka ya ugaini yaliokuwa yakimkabili.

Rais huyu wa kwanza mwanamke Tanzania, unaweza kumfananisha na Jike la Simba, Ana mengi amefanya kwa muda mfupi, hakika kishindo chake ni kikubwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e172eeb3913d30d4a8d66785571329e6.PNG

MOJA ya misemo maarufu ya Rais mstaafu Ali Hassan ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi