loader
Rambirambi kifo Spika Uganda zamiminika

Rambirambi kifo Spika Uganda zamiminika

RAMBIRAMBI kutoka ndani ya Uganda na nchi jirani zinazidi kumiminika kutokana na kifo cha Spika wa Bunge la Uganda, Jacob L'Okori Oulanyah kilichotokea juzi nchini Marekani huku serikali ikitarajiwa kutoa taarifa kuhusu mipango ya maziko leo.

Miongoni mwa viongozi mashuhuri waliotangulia kutuma salamu hizo kwa Rais Yoweri Museveni na Waganda kwa ujumla ni pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye na Mwenyekiti wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Abdullah Makame.

Katika salamu zake kwa Museveni, familia ya Marehemu Oulanyah na Waganda kwa ujumla, jana Dk Mathuki alimwelezea Spika Oulanyah kama kiongozi aliyekuwa mzalendo na mshirika wa kutegemewa wa EAC.

Kwa upande wake, Rais Ndayishimiye alieleza huzuni yake kutokana na kifo hicho akisema watu wa Burundi wanatoa pole na wamesikitishwa kwa msiba huo.

Kutokana na kifo hicho, Mwenyekiti wa Wabunge wa EALA kutoka Tanzania, Dk Makame, alisema anaungana na wanafamilia, Bunge la Uganda, wananchi wa Jimbo la Omoro, Waganda na wananchi wa EAC katika kuomboleza kifo cha spika huyo aliyekuwa madarakani akisema: “Jumuiya imepata majonzi makubwa.”

Rais Museveni juzi kupitia akaunti yake ya tweeter, alilitangazia taifa lake la Uganda ambalo ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu kifo cha Spika Oulanyah kilichotokea Seatle nchini Marekani alikokuwa akitibiwa.

"Wananchi, kwa huzuni kubwa ninatangaza kifo cha Spika wa Bunge, Jacob Oulanyah. Habari hizi za kusikitisha nilipata saa 10:30 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki kutoka kwa watu ambao wamekuwa naye pamoja na daktari aliyekuwa akimuuguza katika chumba cha wagonjwa mahututi. Alikuwa kada mzuri. Nilichelewesha tangazo hilo ili watoto wake wafahamishwe kwanza,” alisema Museveni.

Waziri katika Ofisi ya Rais, Milly Babalanda, alituma ujumbe kupitia ukurasa wake wa tweeter akisema serikali itasimamia mipango ya maziko ya spika huyo na kwamba leo itatoa taarifa rasmi kuhusu mipango ya mazishi.

"Waganda wenzangu, ni bahati mbaya sana kumpoteza spika wetu. Ninawapa pole wananchi wa Uganda na Waafrika wote kwa ujumla,” alisema Babalanda.

Waziri wa Teknolojia Habari na Mawasiliano, Dk Chris Baryomunsi, alisema serikali inatarajia kufanya mkutano na familia ya Oulanyah ili kujadili maandalizi ya kurejesha mwili kutoka Marekani.

"Lazima tumpe spika mazishi ya heshima. Tunawaomba wananchi kuendelea kuwaombea familia ya marehemu,” alisema.

Alisema Spika huyo kwa mara ya kwanza alilazwa katika Hospitali ya Mulago na baadaye Hospitali ya Nakasero kabla ya kupelekwa Marekani. Hapo awali, alikuwa Dubai ambapo alifanyiwa upasuaji.

"Amekuwa mgonjwa na madaktari na wahudumu wa afya wamekuwa wakimhudumia lakini kuhusu chanzo cha kifo, nadhani tusubiri ripoti ya uchunguzi wa maiti kutoka kwa madaktari waliokuwa wakimhudumia," alisema.

Wengine waliotuma salamu za rambirambi ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mathias Mpuuga huku spika mtangulizi wa Marehemu Oulanyah, Rebecca Kadanga, akisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa nchi, familia, marafiki na chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).

Naye Kamanda wa Jeshi la Wananchi wa Uganda (UPDF), Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alisema Oulanyah alisema taifa limepoteza mtu shujaa aliyekuwa mchangamfu, rafiki, mtanashati na muwazi.

“Alikuwa ni rafiki wa kweli na wa kutegemewa… Uganda imepoteza shujaa…” alisema Kainerugaba.

Kwa mara ya mwisho Oulanyah alionekana bungeni Desemba mwaka jana na Februari 4, mwaka huu, alisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

Oulanyah ambaye pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Omoro, alichaguliwa kuwa Spika Mei 24, 2021, baada ya kumshinda Spika wa zamani, Rebecca Kadaga. Alihudumu kama Naibu Spika wa Bunge tangu Mei 2011 hadi Mei 2021.

Oulanyah alizaliwa Machi 23, 1965 katika Wilaya ya Gulu wakati huo.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

1 Comments

  • avatar
    Baluku chrispus
    07/04/2022

    Asante sana mwandishi wa habari.Ninafurahi sana kwa kazi yenye unafanya. sasa mimi ni mwanafunzi wa uandishi wa habari kutoka chuo kiku cha Bugema hapo mjini mkuu wa Uganga,Kampala

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi