loader
Mechi za kirafiki Stars zitumike vizuri

Mechi za kirafiki Stars zitumike vizuri

WIKI hii yote timu kutoka nchi mbalimbali duniani zipo kwenye mechi za kirafiki za kimataifa zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa. Tanzania imefanya mashindano mafupi ikizialika timu za Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan, ili kunogesha wiki hiyo.

Tayari timu ya taifa, Taifa Stars imeshacheza na Afrika ya Kati ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 3-1. Leo Afrika ya Kati itacheza na Sudan kabla Stars haijamalizana na Sudan keshokutwa.

Uzuri wa mechi hizi ni kupata pointi za kuiwezesha nchi kupanda kwenye viwango vya Fifa kama ikishinda ama kutoka sare.

Lakini pia jambo lingine ni kipimo tosha kwa Stars inayojiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika, Afcon zinazotarajiwa kufanyika Ivory Coast mwakani. Stars itaanza mechi zake kuwania kufuzu fainali hizo Juni mwaka huu. Lakini pia mbali hilo, mwakani kuna michuano ya Chan pia (Kombe la mabingwa wa Afrika) inayohusisha wachezaji wa ligi za ndani, sio mbaya mechi hizi pia zikachukuliwa kama sehemu ya maandalizi maana siku zinasogea.

Sababu zote ni muhimu, hivyo ni vema wachezaji na benchi la ufundi wakatumia vizuri mechi hizo kujifua na pia kuipandisha nchi kwenye viwango vya Fifa. Benchi la ufundi limezipa uzito wa juu mechi hizo ndio maana limeita wachezaji wanaocheza nje ya nchi kadri liwezavyo.

Ni jukumu la wachezaji hao kuipeperusha bendera ya nchi vizuri lakini pia wakijiweka tayari kwa ajili ya mechi za kufuzu Afcon, michuano ambayo Watanzania bado wanatamani kufuzu tena kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 na 2019.

Lakini pia kwa waamuzi, pamoja na kwamba wanaochezesha mechi hizo ni wazawa, wajaribu kutokuwa na upendeleo, hii itasaidia kuwajenga zaidi wachezaji, kwani endapo watachezesha kwa kupendelea wenyeji, itakuwa hasara na maana halisi ya mechi hizo itaondoka. Umuhimu wa mechi hizo usiwe kwa wachezaji na benchi la ufundi na waamuzi tu, Watanzania pia jitokezeni kuiunga mkono Taifa Stars.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/376144e97a94ef95d1720d37bf006765.PNG

JUMATATU Mei 09, mwaka huu, lilifunguliwa Kongamano ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi