loader
‘Na sisi watoto tupo watuwekee katuni’

‘Na sisi watoto tupo watuwekee katuni’

“KWANI hawajui kuwa na sisi watoto tupo kwenye basi?...Watuwekee na sisi katuni?” Hili ni swali la mtoto alilouliza baada ya kuangalia burudani tofauti kupitia runinga kwenye basi moja la masafa marefu. Kama ilivyo kawaida ya mabasi ya masafa marefu, ndani huwa na televisheni kwa ajili ya kuburudisha abiria.

Idadi ya televisheni zilizomo hutokana na daraja la basi husika. Kulingana na utaratibu wa mamlaka za usafirishaji, mabasi yaliyo katika daraja la kawaida yanatakiwa kuwa na si chini ya televisheni tatu; daraja la kati televisheni kuanzia nne na kuendelea na daraja la kwanza ni televisheni zaidi ya tano au kila kitu kuwa kifaa hicho. Katika mabasi mengi, mara nyingi burudani ambazo huwekwa ni pamoja na muziki, maigizo, vichekesho, filamu na mengine nyimbo za injili na kaswida.

Ndani ya basi hilo ambalo binti yangu aliamua kuhoji sababu za watoto kutowekewa pia burudani zinazowahusu, kulikuwa na televisheni zaidi ya nne ambazo zote huangalia picha ya aina moja ambayo wahudumu huamua kuweka kwa utashi wao. Ziliwekwa filamu za vita na mapigano. Pia viliwekwa vichekesho na maigizo ambayo baadhi yalijaa maudhui ya mahusiano, mifarakano ya ndoa huku baadhi ya waigizaji wakitumia lugha zisizo na staha. Kwa upande wa nyimbo za muziki wa kizazi kipya, baadhi yake, mashairi sambamba na uchezaji wake ni wenye kuleta ukakasi katika suala zima la maadili ya mtoto.

Tunaambiwa ndiyo miziki ya kizazi kipya! Miziki ambayo utunzi wake umejikita katika mapenzi na mahusiano! Miziki ambayo uvaaji wa wahusika haupendezi machoni pa watoto kiasi kwamba, inapaswa ibandikwe alama ya X kuashiria kuwa ni maalumu kwa watu wazima pekee. Iliwekwa pia baadhi ya miziki inayosifia au kuhamasisha vitu na vitendo visivyoendana na watoto.

Mathalani, hamasa kwa matumizi ya vilevi. Nyimbo nyingine zimejaa vijembe na mipasho. Kwa upande wa maigizo, kama ilivyo kawaida, hukosi picha zinazoonesha watu wanaotoa matusi, kufanya mambo ya faragha (yasiyostahili kuonwa na watoto) ambayo naamini kwa familia zinazofuatilia malezi na maadili, zisingependa picha za namna hiyo ziangaliwe na watoto wadogo. Maana haya mambo tunaweza kuyapuuza lakini huenda mambo wanayoshuhudia watoto kwenye vyombo vya habari yakawa miongoni mwa vichocheo kwa watoto kuanza ngono mapema, mimba na ndoa za utotoni na hata ulezi.

Kama wasemavyo waswahili, ‘Macho hayana pazia’, binti yangu na watoto wengine katika hilo basi hilo, bila kujali udhibiti walio nao wazazi au walezi wao dhidi ya burudani zisizowastahili, walijikuta wakilazimika kuangalia. Na hadi mwisho wa safari, hapakuwa na burudani yoyote yenye vionjo maalumu kwa watoto. Ndiyo maana binti aliamua kuhoji kama wafanyakazi katika basi hilo hawajui kuwa pia wamo watoto wanaostahili pia kuangalia kile wanachokipenda?

Binti alitaja baadhi ya katuni ambazo alitamani basi hilo lioneshe japo kwa muda mfupi kisha wawarejeshee watu wazima burudani zao. Alitaja katuni za Ben Ten, Tom and Jerry, Kirikuu na za tinga tinga jambo lililoungwa pia na ndugu zake wengine (watoto) waliokuwa kwenye basi hilo. Kwa ujumla, hoja za watoto hao ni ujumbe tosha unaokumbusha umuhimu wa kuheshimu hisia za watoto katika suala la kuburudisha hadhira kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye vyombo vya usafiri.

Swali hili la mtoto linakumbusha umuhimu wa jamii kufikiria mahitaji ya watoto kwa kuwapa mahitaji mbalimbali ikiwamo burudani zinazoendana na umri wao badala ya watu wazima kufikiria matakwa yao binafsi.

Natamani wasafirishaji katika mabasi ya abiria, hususani ya masafa marefu, wafanyie kazi hili kwa kuhakikisha pia kundi la watoto linapata burudani inayowastahili ili wapate ahueni ya safari ndefu ndani ya magari hayo kama ilivyo kwa watu wazima. Visaidie kuonesha pia vipindi au mada zenye mafunzo na vijitahidi kudhibiti picha zenye ukakasi kwa maadili ya watoto. Hata katuni, ni vyema ziangaliwe na kuchujwa kuhakikisha zinakidhi utamaduni, maadili na ustawi wa mtoto wa Kitanzania.

Kwa kuwa ni nadra sana kukosa abiria watoto katika basi lolote la masafa marefu. Hivyo wasafirishaji na wadau wengine wakiwemo wazazi na walezi, tusione jambo hili kama dogo.

Ni suala la kutafakari na hasa yanapobaini kuwapo abiria watoto, pia yawape kile kinachowafaa wafurahi. Watoto wasigeuzwe watumwa wa kuangalia burudani na vipindi vya watu wazima vinavyoweza kuharibu maadili yao. Uamuzi huu si lazima utungiwe sheria au kanuni bali utashi na busara zitumike.

Tusisubiri watoto wengine waulize swali hili: Kwani hawajui kuwa na sisi watoto tupo kwenye basi?... Watuwekee na sisi katuni.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/41228a339e3e1653d3bc18b0fc118bca.PNG

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Stella Nyamenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi