loader
Manufaa ya DRC ndani ya EAC

Manufaa ya DRC ndani ya EAC

WACHAMBUZI wa masuala ya siasa na uchumi wamesema uamuzi wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kukubali Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo una manufaa makubwa.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam, Godwin Amani alisema ujio wa DRC katika EAC utaongeza wigo wa ushirikiano, mapatano na nguvu ya kauli.

Alisema ujio wa DRC utaifanya EAC kuwa na nguvu ya kauli kwa masuala mbalimbali dhidi ya Jumuiya nyingine zenye nguvu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema kuingia kwa DRC katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kutaongeza wigo wa biashara. Alisema DRC ni nchi yenye rasilimali nyingi, hivyo ujio wake utaongeza fursa ya kibiashara kati yake na nchi nyingine wanachama, pia itaondoa vikwazo vya kibiashara kati yake na wanachama wenzake.

“Kwa kuwa DRC hakuwa mwanachama wa EAC, watu wake walilazimika kuwa na viza ya kuingia kwenye baadhi ya nchi za EAC, lakini sasa kikwazo hicho kimeondoka, maana yake watu na bidhaa za DRC wataweza au zitaweza kuingia nchi nyingine za EAC bila kikwazo, kuingia kwa DRC pia kutapanua soko na kuwa na soko takribani la watu milioni 300,” alisema Dk Mbunda.

Kisiasa alisema itaimarisha suala la ulinzi na usalama kwa kuwa kutakuwa na nguvu ya pamoja ya kushughulikia matatizo ya kiusalama ndani ya DRC ambayo pia yanaathiri nchi nyingine za jirani. Mchambuzi wa masuala ya Diplomasia, Profesa Kitojo Watengere alisema kuingia kwa DRC katika EAC ni hatua muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania pamoja na nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo.

Alisema DRC itachangia ongezeko la biashara kupitia usafirishaji wa bidhaa na uagizaji kutoka DRC kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga.

“Tanzania pia iko tayari kuongeza mauzo yake hadi DRC kwa kuuza vyakula na bidhaa nyingine zinazozalishwa nchini. Nchi pia itakuwa na uwezo wa kukuza uwekezaji katika nchi hiyo katika sekta mbalimbali za uchumi,” alisema Profesa Watengere.

Alisema kuingia kwa DRC katika EAC kutaongeza uwezo wa kujadiliana wa kambi ya kikanda katika kufanya biashara na dunia nzima kwa kuzingatia ukubwa wa soko lake na upatikanaji wa maliasili.

Mhadhiri wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi alihamasisha serikali kuwekeza zaidi katika kuboresha miundombinu na kuongeza weledi katika bandari zake.

Profesa Moshi alishauri mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ujenzi wake ufanyike kwa kasi ili kuiunganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi nyingine zilizopo katika jumuiya hiyo.

Alisema nchi za jumuiya ya EAC zina jukumu muhimu katika kuleta utulivu na usalama na kuongeza biashara kwa vile zina mwelekeo wa kupunguza vikwazo vya kibiashara miongoni mwa nchi wanachama. Jana wakuu wa nchi EAC walikubali DRC iwe mwanachama wake.

Kabla ya DRC, EAC ilikuwa na wanachama sita ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Burundi. Viongozi hao walitoa uamuzi huo kupitia kura zilizopigwa wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao, ukiongozwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Mwenyekiti wa EAC, Rais Uhuru alitangaza uamuzi huo na akasema kukubalika kwa DRC kunaashiria tukio muhimu katika historia ya ushirikiano wa eneo hili la Afrika Mashariki.

Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa marais wa jumuiya hiyo walioikaribisha nchi hiyo ya DRC katika jumuiya hiyo.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaikaribisha kwa moyo mkunjufu DRC katika jumuiya. KAZI IENDELEE!,” alisema Rais Samia akiwa katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame alisema nchi yake inaunga mkono hatua ya DRC kujiunga na jumuiya hiyo ya EA na kwamba katika eneo hilo, iko tayari kutekeleza jukumu lake katika kuunga mkono hatua hiyo.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alisema hatua hiyo katika EAC ni tukio kubwa kwani linaashiria ustawi kwa wananchi. “Kama viongozi tuendelee kujitahidi kuhakikisha amani, usalama na utulivu vinadumishwa katika kanda,” alisisitiza.

Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombanza alisema: “Jamhuri ya Burundi inaikaribisha DRC kwa uwazi katika eneo hilo!” “Kukubalika kwa DRC kunaimarisha umoja huo,” alisema Barnaba Marial- Waziri wa Masuala ya Rais, Jamhuri ya Sudan Kusini.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya EA, Dk Peter Mathuki alisema jumuiya hiyo sasa inaanzia Bahari ya Hindi hadi Bahari ya Atlantiki na kufanya eneo hili liwe na ushindani na rahisi kufikia eneo la Biashara Huria la Afrika.

“Baada ya kuingia kwa Mkataba wa kuanzisha EAC na kuweka hati ya kukubalika kwa Katibu Mkuu, DRC itaungana na ushirikiano wa jumuiya katika sekta, programu na shughuli zote zinazokuza nguzo za Mtangamano wa EAC,” alisema Dk Mathuki.

DRC ilituma maombi ya uanachama mwaka wa 2019 na inaingia EAC ikiwa na idadi ya watu wanaofikia milioni 90.

Miongoni mwa faida itakazopata ni kuongeza kibiashara kwa kutanua masoko na usalama. Jumuiya ya Afrika Mashariki ilifufuliwa 1999 na mataifa matatu waasisi Tanzania, Kenya na Uganda baada ya ile ya awali kuvunjika 1977. Burundi na Rwanda zilijiunga 2007 na Sudan Kusini 2016.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha na Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi