loader
Mwaka mmoja wa Rais Samia na mwanga mpya kwa wanahabari

Mwaka mmoja wa Rais Samia na mwanga mpya kwa wanahabari

RAIS  Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Kwanza Mwanamke wa Tanzania Machi 19,2021 kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Magufuli alifariki ikiwa ni miezi mitano katika awamu yake ya pili kama Rais.

Tangu kuingia kwake madarakani, Rais Samia amechukua hatua mbalimbali, kukabiliana na baadhi ya masuala ya haki za binadamu na kuimarisha demokrasia na uhusiano aa mataifa ya nje.

Uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari:

Matarajio ya wengi ni kwamba kitendo cha kufungulia magazeti ni hatua ya kwanza tu katika hatua nyingi zinazotakiwa kufuatwa, ili kurejesha hadhi, heshima na wajibu wa vyombo vya habari katika nchi inayoendeshwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia.

Kama kufungulia magazeti manne ni hatua ya kwanza, zipi ni hatua nyingine zinazotakiwa kufuatwa kurejesha hali katika mstari unaotakiwa?

Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016

Jambo kubwa lililo katika vinywa vya wadau wa sekta ya habari nchini Tanzania linahusu maudhui ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016. Si kila kitu kwenye sheria hiyo kina matatizo, lakini vile vyenye matatizo vimeibua mjadala mkubwa.

Ni sheria hiyo ndiyo iliyoweka masharti ya mtu anayetaka kuwa mwandishi wa habari, awe na angalau stashahada ya uandishi wa habari, ili aruhusiwe kufanya kazi hiyo.

Kwenye mkutano wake na wahariri, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnaye hivi karibuni  alizungumzia uwezekano wa kuongezwa kwa muda wa kutumika kwa sheria hiyo iliyopangwa kuanza kutumika mwaka huu.

Inafahamika kwamba serikali ina mapendekezo ya makundi matatu tofauti yanayohusika na masuala ya kisheria na habari - Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), CORI na Jukwaa la Wahariri (TEF) yaliyotaka kufanyiwa kwa marekebisho sheria hiyo ya mwaka 2016.

Akizungumzia mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile amesema Rais Samia anaupiga mwingi, kwani  kufungulia magazeti na kuruhusu mijadala ni hatua muhimu katika muhtasari wa uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari kwa maslahi mapana ya nchi.

“Sasa hivi simu ya mkononi hakuna anayetumia VPN, watu wamekuwa huru kupiga simu, kuchat, kuzungumza na kutoa mawazo yao, hata  vyombo vya Habari ukiangalia redio, televisheni na magazeti,  kuna uhuru wa kiasi kikubwa ukilinganisha na kipindi kilichopita.

“Hata Waziri wa Habari Mh. Nape Nnauye, mara kadhaa amekaririwa yupo tayari kubadili sheria ya magazeti ya mwaka 2016, ambayo inaitwa sheria ya huduma ya habari, lakini pia ameshafanya mabadiliko kadhaa katika kanuni na kulegeza masharti ya kanuni, ambapo garama za vyombo vya eletroniki kurusha matangazo na kumiliki leseni imepungua kutoka Sh milioni 75 hadi Sh milioni 33 kuna unafuu mkubwa.

“Hata televisheni za kitaifa zinaonekana kwenye king’amuzi, wakati huko nyuma haikuwepo na muda si mrefu tutaanza kuona bunge live, ni jambo jema, mwisho wa siku tutafikia kiwango cha uhuru kinachotakiwa ulimwenguni,” amesema.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Rose Reuben, amesema mwaka mmoja wa Rais Samia hali ni nzuri.

“Mwaka huu tunaona vyombo vilivyokuwa vimefungiwa vimefunguliwa, tunaona serikali imekubali kukutana na wadau kuweka mapendekezo kubadili sheria ya habari, tunaona serikali ipo tayari kuweka sera na sheria itakayoweza kuruhusu uhuru wa habari, inakubali watu kufanya mijadala mbalimbali inayoleta tija katika jamii. 

“Lengo kubwa ambalo serikali inapaswa kuliangalia pamoja na wadau wa habari ni maslahi ya waandishi wa habari, waandishi wanafanya kazi katika mazingira magumu, ili kupata waandishi wanaandika habari zenye tija ni kuboresha maslahi yao na kuboresha mazingira yao ya kazi.”

Kwa mujibu wa takwimu za serikali za 2021 mafanikio mengi katika tasnia ya habari, kufuatia na ongezeko la vyombo vya habari kulingana na takwimu

Mwaka 2015, Tanzania ilikuwa na vituo vya redio 106 na televisheni 25, lakini hadi kufikia mwezi Februari 2021 kuna jumla ya vituo vya redio 193, televisheni 46, magazeti 247, televisheni za mtandao 443 na redio za mtandao 23.

Mwaka mmoja wa Rais Samia, walau waandishi wameweza kuanza kuona mwanga  kuhusu Tanzania mpya, yenye vyombo vya habari imara na vinavyotimiza wajibu wake kwa umma.

Mkataba wa Afrika Mashariki unataka kila nchi lazima ikuze demokrasia na uhuru wa kujieleza, ingawa wanaamini kuwa hakuna uhuru ambao hauna mipaka, lakini sheria hii inafanya uhuru usiwepo.

Naye Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Salome Kitomari amesema Katika siku 365 za Rais Samia Suluhu, kitu cha kwanza kilichofanyika, ni kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru bila bughudha na kuhakikisha vyombo vya habari vinakua.

“Kanuni ya kusajili TV za mtandaoni ilikuwa ni Sh. milioni moja, imepungua hadi Sh 500,000, hii maana yake imeleta ahueni kwa sababu sekta ya habari inakua na teknolojia nayo inakua, kama sekta hii inakua maana yake wapo vijana wataanzisha TV za mtandaoni na kujiajiri,” amesema Salome.

Kwa mujibu wa wadau Sheria zinazopaswa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015, Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020.

Uhuru wa vyombo vya Habari unatambulika kwa mujibu wa sheria za kitaifa, kikanda na kimataifa. Kwa mfano ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Tamko la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu, 1948, Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamuna Watu pamoja na Mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966.

Katiba ya nchi pamoja na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inasisitiza kuwepo kwa vyombo huru vya habari na kuongeza kuwa vyombo huru vya habari vina umuhimu mkubwa kwenye jamii na kwa serikali.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/24aa0fd35772df1647513555128d45de.jpg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi