loader
Wataalamu wana hoja mashirika goigoi

Wataalamu wana hoja mashirika goigoi

JUZI wakati akipokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuna mashirika yanayotumia fedha za serikali lakini hayana tija kwa taifa.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi, kukaa na kuyaangalia mashirika hayo kwa umakini na yale yanayotakiwa kufutwa yafutwe na yale ya kuimarisha yaimarishwe.

Pamoja na maagizo hayo ya Rais Samia, leo katika gazeti letu tumezungumza na wachambuzi wa masuala ya uchumi na wakasema pamoja na nia njema ya Rais ipo haja kwa watendaji hao waliopewa maagizo kutulia na kufanya kazi kitaalamu.

Mmoja wa watu waliokaririwa na gazeti hili ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia na Utawala Bora Afrika (ForDIA), Buberwa Kaiza ambaye alikubaliana na kauli ya Rais Samia na kuongeza kuwa ni vyema kauli hiyo ikafanyiwa kazi kitaalamu kwanza kabla ya kuanza kutekelezwa.

Sisi tunaungana na kauli ya Kaiza ya maagizo hayo kufanyiwa kazi kitaalamu kwa kuwa uanzishaji wake ulikuwa na lengo na kama lengo halifanyiki ni vyema kujua kwanini.

Pia inawezekana shauri hilo kushirikisha wafanyakazi wenyewe na wadau wengine kabla ya kufikiri kulifuta. Kauli ya Kaiza inafanana na kauli ya Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi aliyesema ni ukweli kuwa mashirika ya umma yasipofanya kazi kwa ufanisi yanakuwa mzigo kwa serikali japo kuna mashirika ambayo ni lazima kuwepo.

Alihoji hatua hiyo kwa kusema kabla ya serikali kufikia hatua ya kufuta mashirika hayo, haina budi kuangalia ni kitu gani kimesababisha yasifanye kazi kwa ufanisi. Hakika kuna sababu nyingi ikiwamo mtaji na ukiritimba hivyo kama upo uwezekano wa kuondolewa kwa matatizo hayo kufanyike ili kuwa na ufanisi.

Kama anavyoamini Profesa Moshi kwamba sekta binafsi ndiyo injini ya maendeleo, lakini sekta ya umma ndiyo magurudumu ya hiyo injini, sisi tunasema kuna kila sababu ya kuwa makini katika shauri hili kwa manufaa ya umma.

Inatupasa tukumbuke kwamba mashirika hayo yaliundwa kwa malengo mahususi yenye maslahi kwa Taifa hivyo tunaungana na Watanzania wengine wanaoona haja kwa serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kutokufanya vizuri kabla ya kufikia hatua ya kuyafuta.

Kwa hiyo tunashauri kama walivyoshauri wachambuzi mbalimbali kwamba timu itakayoundwa kuangalia mashirika haya lazima iangalie historia yake na wajibu wake kabla ya kuona mzizi wa kutofanya vyema na kushauri namna ya kuuondoa.

Ni vyema kujua chanzo cha kuzorota kwa kuangalia menejimenti nzima ili kujua katika malengo waliyopewa wamekwama wapi, kwa sababu shirika haliharibiwi na watu wote, anaweza akawa mtu mmoja tu akafanya shirika lionekane halifai.

Tunachotaka kusema hapa kabla ya serikali kufuta mashirika hayo, ni vyema ikazingatia sababu ya kuanzishwa kwake na utaratibu uliotumika kuyaanzisha ikiwemo sheria ya kuyaanzisha na kuangalia kama ndoto hizo zilitimia na kama hazikutimia kwanini, ndipo maamuzi yachukuliwe.

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi