loader
‘Farm Boksi’ yawafikisha  wakulima duniani

‘Farm Boksi’ yawafikisha wakulima duniani

TUME ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imekuwa ikisaidia kuandaa mawazo ya vijana ili yaweze kuwa bidhaa inayouzika. Katika kuwaandaa vijana hao, huangalia mawazo yenye ubunifu yanayoweza kuisaidia jamii katika kutatua changamoto zilizopo.

Pamoja na tume hiyo kuwasaidia vijana pia inawapatia mitaji midogo kupitia fedha za Benki ya Dunia ambazo hazina masharti makubwa ili baadaye waweze kuzirudisha.

Kijana mwenye Shahada ya Upangaji na Usimamizi wa Miradi, Joseph Mwanyika (27) ni miongoni mwa vijana saba wa Tanzania na Afrika Kusini ambao ubunifu wao umeshinda baada ya mchujo kufanywa na Costech pamoja na Wakala wa Teknolojia na Ubunifu (TIA) uliopo Afrika Kusini.

Mwanyika amebuni Farm Boksi, ubunifu ulioibuliwa kutokana na nia ya kuwasaidia wakulima wadogo wasipate hasara baada ya kuvuna, pia waweze kutafuta soko la uhakika la mazao yao.

Farm Boksi ni jukwaa la biashara la mtandaoni ambalo hutoa elimu ya kilimo kwa wakulima wadogo, kuongeza thamani ya bidhaa za shambani na kudhibiti michakato ya usambazaji wa bidhaa za shambani ili kumfikia mnunuzi katika ubora unaotakiwa.

Ubunifu huo umeundwa kuwawezesha wakulima kupunguza hasara wanazopata baada ya kuvuna mazao yao, kuongeza mapato yao kupitia soko la uhakika kitaifa na kimataifa kwa kutumia teknolojia ya jukwaa la mtandaoni.

Kupitia teknolojia ya biashara ya mtandaoni, wanunuzi kutoka duniani kote wanaweza kuagiza bidhaa za shambani kwa urahisi pia wanarahisisha mchakato wa ugavi, kuanzia kujumlisha, kuongeza thamani na usafirishaji hadi kwa mnunuzi aliyelengwa.

Anasema ili kuboresha ubora na upatikanaji wa mwaka mzima wa bidhaa za shambani, wameunda kontena baridi ili kuhifadhi bidhaa za shambani ili kuweka ubora na maisha marefu kabla ya kufika kwenye nyumba ya kufungashia kutoka shambani.

“Mnamo 2018 timu ya Farm Boksi iligundua kuwa wakulima barani Afrika wanapoteza zaidi ya asilimia 40 ya bidhaa zao baada ya kuvuna kutokana na utunzaji mbaya wa mazao na ukosefu wa mifumo ya kuhifadhi mazao ya shamba kabla ya kwenda sokoni.

“Kwa wastani, wakulima wadogo 1,000 hupoteza zaidi ya dola 200,000 kwa mwaka kutokana na hasara ya baada ya kuvuna na hii inaathiri vipato na maisha yao,” anasema. Anasema lengo la kubuni Farm Boksi ni kwa sababu sekta ya kilimo nchini ni muhimu kwa kuwa inachangia robo ya pato la taifa ambayo ni sawa na asilimia 20 ya thamani ya mauzo ya nje.

Kwa mujibu wa takwimu watu milioni 32 ambayo ni sawa na robo tatu ya watu wote wanaishi vijijini, kati ya hao asilimia 80 wanajihusisha na sekta ya kilimo.

“Ikumbukwe kwamba kiwango cha umaskini wa maeneo ya vijijini ni karibu asilimia 33.3 wakati mijini ni karibu asilimia 21.7. “Kwa mantiki hii, maendeleo ya kilimo yanachukua sehemu muhimu si tu katika ukuaji wa uchumi bali pia katika kupunguza umaskini katika nchi yetu. “Hata hivyo, kasi ya ukuaji wa kilimo kwa miaka kadhaa iliyopita kati ya asilimia nne hadi tano kwa mwaka imeshindwa kufikia lengo la kitaifa asilimia sita hadi 10 kwa mwaka,” anasema. Anasema sababu ya utafiti huo ni kwa kuwa waliona kuna umuhimu wa kuwa na maendeleo zaidi kwenye sekta ya kilimo. “Tunaamini kuwa kuongezeka kwa mahitaji ya chakula duniani na kuongezeka kwa kiwango cha ukosefu wa ajira ni baadhi tu ya sababu kwa nini ni muhimu kuboresha mbinu za kilimo na kuwezesha mlolongo wa ugavi wa kilimo kufikia mahitaji ya chakula ya dunia.

“Kutokana na utafiti wetu na mwingiliano na wakulima, tuligundua kuwa changamoto nyingi kwa wakulima ziko katika ukuaji mzuri wa mazao, upotevu wa baada ya kuvuna na upatikanaji wa soko la uhakika la kuuza mazao yao,” anasema.

Anasema katika kutafuta utatuzi wa mawazo yao, walipata njia waliyoibuni ya kujenga mfumo wa utendakazi wa mazao na soko ambao unasimamiwa na mkulima kupitia simu ya mkononi ambayo siyo simu janja.

Anasema suluhisho walilolipata linajumuisha vipengele vitatu ambavyo ni utoaji wa huduma za ugani wa kilimo mtu akiwa mbali kwa kutumia simu ya mkononi lengo likiwa ni kuongeza ujuzi wao wa kilimo na kutekeleza mbinu bora za kuboresha ufanisi wa mazao.

Pia kuwapa wakulima kontena la kuhifadhia nafaka linalotumia nishati ya jua na dijitali ambalo lina uwezo wa kubeba kati ya tani moja mpaka tatu za nafaka. Anasema joto la kontena la kuhifadhia linaweza kudhibitiwa na mkulima kupitia mpango wa utumiaji wa simu ya mkononi.

Pia ukuzaji wa jukwaa la kidijiti ili kumuunganisha mkulima mmoja mmoja na mtumiaji wa mwisho au wateja, hivyo kumsaidia mkulima kuuza kwa bei ya soko kwa kuondoa madalali.

Anasema Farm Boksi walipata nafasi ya kushiriki mashindano ya Twiga ambayo yalifanyika mwaka 2018 yaliyoshirikisha nchi ya Tanzania na Afrika Kusini ambapo walifanikiwa kuwa kati ya washindi wa tatu waliopatikana nchini Tanzania.

Anasema kupitia mashindano hayo yaliyosimamiwa na Costech walifanikiwa kupata ruzuku ya fedha taslimu Sh milioni 10 zilizowasaida katika shughuli zao za ukuzaji wa ubunifu ili waweze kufikia wanufaika wengi zaidi. Mbali na fedha hizo waliwezeshwa kupata mafunzo kutoka kwa wabobezi katika tasnia ya ubunifu ili waweze kufanya matumizi yenye tija katika kukuza bunifu zao.

Costech kupitia mashindano ya Twiga wamewawezesha kuwafikia wanufaika wengi zaidi na kupanua shughuli zao. Naye Mkurugenzi wa Ubunifu na Teknolojia kutoka Costech, Dk Gerald Kafuku anasema katika kuwasaidia vijana wamekuwa na uhusiano na nchi mbalimbali kwa ajili ya kupata uzoefu wao ikiwa ni pamoja na kutumisha mifuko ya kuwasaidia wabunifu.

Anasema mradi huo wa Twiga una fedha za kuwasaidia vijana wenye mawazo ya ubunifu katika nchi za Tanzania kupitia Costech na Afrika Kusini kupitia Technology Innovation Agency (TIA).

Kafuku anasema mwaka 2018 Costech na TIA waliangalia maeneo wanayoweza kushirikiana katika eneo la usalama wa chakula na afya na kukubaliana kuangalia ubunifu katika nchi hizi mbili ambao ziko kwenye soko.

Kwa maelezo yake vijana wengi walijitokeza kushindania nafasi hizo ambapo baada ya mchujo Afrika Kusini walipatikana vijana watano na Tanzania watatu.

Anasema kwa kuwa mradi huo unakaribia kufikia mwisho, wabunifu wa Afrika Kusini wamekuja nchini na wa Tanzania watakwenda Afrika Kusini hivi karibuni, lengo likiwa ni kutafuta masoko pamoja na kutafuta wabia katika ubunifu wao walioufanya.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e3e4d6fb0d2ed8dad43964cc396fd817.JPG

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi