loader
Simba ifanye maandalizi mapema dhidi ya Orlando

Simba ifanye maandalizi mapema dhidi ya Orlando

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba, wamefuzu robo fainali na wanatarajiwa kucheza na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Simba ambayo ndio timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuendelea kuwemo kwenye michuano hiyo, ilifuzu hatua hiyo kwa kishindo baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya US Gendarmerie ya Niger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mechi hiyo ya mwisho ya makundi, Simba ilihitaji ushindi pekee kufuzu hatua hiyo na hicho ndicho kilichotokea. Kwa kufuzu huko, Simba inaweka rekodi ya kufuzu robo fainali mara tatu ndani ya miaka mitano, mara mbili ikiwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunaipongeza Simba kwa hatua hiyo kwani inapeperusha vyema bendera ya Tanzania, na hakuna shaka sasa msimu ujao nchi itawakilishwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa.

Pamoja na pongezi hizo, wawakilishi hao hawatakiwi kubweteka, mechi ya robo fainali iko njiani, Aprili 17 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana Aprili 24 mjini Johannesburg.

Haitarajiwi kuwa mechi rahisi kwa vile wapinzani wao pia ni timu bora na yenye uzoefu kwenye michuano hiyo. Hivyo Simba inahitaji kufanya maandalizi ya hali ya juu ili kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo, jambo ambalo hakuna shaka nchi inatamani lifikiwe.

Umakini unahitajika kuanzia kwa viongozi, benchi la ufundi mpaka wachezaji wenyewe. Wakati maandalizi ya mechi hiyo yakiendelea, Shirikisho la Soka Afrika, CAF, limetoa taarifa kuwa mechi hiyo ni miongoni mwa zitakazotumia VAR (Video Assistance Referee).

Tunafahamu kuwa hilo ni jambo geni nchini, mara zote maamuzi ya VAR hutumika kwenye Ligi Kuu ya England na michuano mbalimbali ya kimataifa. Simba itakuwa ya kwanza kuonja tamu na chungu ya VAR.

Tunaimani katika maandalizi ya kuelekea mechi hiyo, benchi la ufundi litafanyia kazi hilo na wachezaji wapate kuwa na uelewa zaidi juu ya VAR. Ni imani yetu Simba imejipanga vyema kufanya yote muhimu kuelekea mechi hiyo na hakuna shaka inayo pia nafasi ya kufanya vizuri.

Kila la kheri.

foto
Mwandishi: Mhariri

1 Comments

  • avatar
    nicky mvanga
    04/05/2022

    mimi ni Mtanzania naeishi Afrika Kusini jimbo la Pritoria,ni kweli simba wajiandae vizuri,sababu hawa Orando nawaona wanajifua kwelikweli yaani tujiandae,tuwe makini na faulo zisizo na maana,sababu watatumia ujanja wa mchezaji wa simba kupata kadi nyekundu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi