loader
Ujasiri wa wanawake suluhisho kwa mfumo dume

Ujasiri wa wanawake suluhisho kwa mfumo dume

WANAWAKE wamekuwa wakikabiliwa na changamoto katika kufi kia malengo yao hasa pale wanapotafuta haki zao za uwakilishi katika nafasi za uongozi kutokana na mfumo dume uliojengeka miongoni mwa jamii kuanzia ngazi ya familia.

Sehemu kubwa ya jamii yetu hapa nchini, imekuwa ikimwangalia mwanamke kwa dhana tofauti na kumhusisha ama kudiriki kumtolea hukumu huku akionekana kama kiumbe kisichoweza kuleta maendeleo au mabadiliko katika jamii yake.

Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia namna wanawake kadhaa ambao wamepata fursa ya kuongoza akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan kwa ustadi na weledi mkubwa kuliko hata wanaume pamoja na kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Mbali na Rais Samia pia tunajionea namna gani wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walivyomuamini mwanamke na kumpa nafasi ya kuongoza mhimili huo bila wasiwasi.

Katika hili ni dhahiri kwamba mwanamke akipatiwa fursa na kujengewa mazingira ya kuondoa vikwazo vinavyochangia kumfanya ashindwe kufikia kuwa kiongozi, anaweza kuwa kiongozi mzuri katika nafasi anayopata na kuweza kusimamia vizuri nafasi hiyo.

Kuna haja kama jamii kufanya uhamasishaji wa uongozi kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuhakikisha watoto wa kike wanajiamini na kufanya uthubutu katika kugombea nafasi za uongozi wakiwa shuleni au vyuoni.

Hivi karibuni Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) chini ya ufadhili wa Kampuni ya KPMG Advisory ilifanya uchambuzi wa sera, sheria na miongozo mbalimbali inayosimamia masuala ya uchaguzi mkuu na za serikali za mitaa ili kubaini mafanikio, mapungufu na fursa katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi wa kidemokrasia.

Mratibu kitaifa wa WiLDAF Tanzania, Anna Kulaya anasema wanafahamu kuwa serikali iko katika mchakato wa kurekebisha sheria mbalimbali za nchi kwa kuwa wanaamini kuwa ili mabadiliko haya yafanikiwe wanahitaji kujadili kwa undani namna ya kuboresha sheria za uchaguzi pamoja na sheria ya vyama vya siasa na marekebisho yake ya mwaka 2019.

Anasema marekebisho hayo yataongeza ushiriki wa wanawake kwa kiasi kikubwa katika siasa, uongozi na ngazi za maamuzi.

“Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Bunge la Tanzania katika kushirikisha makundi mbalimbali wakati wa michakato ya utungwaji au marekebisho ya sheria, tunaamini kwamba Bunge letu litaendelea kutoa fursa ya kuzungumza na wabunge ili kuimarisha mahusiano baina ya wadau na kujenga mikakati ya pamoja katika kulinda na kutetea haki za wanawake na usawa kijinsia,” anasema Kulaya.

Kulaya anasema takribani miaka 20 sasa, WiLDAF imekuwa ikishirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuboresha mazingira wezeshi na kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye nyanja mbalimbali kama vile kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kulaya anasema kwa hivi karibuni mashirika hayo yamekua yakifanya jitihada za kukutana na wadau wakiwemo wabunge, msajili wa vyama vya siasa, wizara na taasisi za serikali kwa lengo la kuwasilisha mapendekezo yanayojengea na kuongea hoja za mapitio na maboresho ya sheria pamoja na miongozo ya chaguzi.

Akizungumzia nafasi ya mwanamke katika uongozi, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk Balozi Pindi Chana anawapongeza wanawake nchini waliojitokeza katika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Tunatambua kwamba idadi ya wanawake Tanzania ni takribani asilimia 51 kutokana na sensa ya mwaka 2012, hili ni kundi kubwa katika idadi ya watu karibia milioni 60 hivyo ni muhimu wanawake kujitokeza katika masuala ya uongozi,” anasema Chana.

Anasema uongozi unaanzia kwenye kaya hadi familia hivyo wanawake wawe mfano bora katika malezi ya watoto kama ni mama au mtumishi wa taasisi yoyote anapaswa kuwa kiongozi bora.

“Tunasema mara kwa mara ukimuelimisha mwanamke umeelimisha taifa zima kwani mama anaangalia watoto, kaya na jumuiya.

Wanawake jitokezeni katika nafasi za uongozi, mfano bora ni kwa Rais Samia kwa kweli amekuwa mfano bora kutuonesha kwamba wanawake wanaweza katika sekta mbalimbali. Uongozi ni mahali popote mtu anapojitolea na kuongoza wengine hivyo tunatarajia wanawake wawe mfano bora katika masuala ya uongozi,” anasema.

Dk Christina Mzava, Mbunge wa Viti Maalumu kutoka mkoani Shinyanga anasema suala la wanawake na uongozi analizungumzia katika nyanja mbili za kisiasa na kijamii.

Anasema kijamii suala la uongozi kwa mwanamke inaanzia katika ngazi ya familia ambapo wanawake hufundishwa uongozi tangu wakiwa wadogo kwa kuwahudumia wadogo zao nyumbani.

Mzava anasema katika ngazi ya maamuzi wanawake wanakuwa nyuma katika uongozi kwa sababu ya mila na desturi kwani watu wengi walikuwa wanaamini mwanamke hafai kuwa kiongozi lakini imekuwa tofauti kwa sasa ambapo wanawake wengi wamekuwa viongozi akiwemo Rais Samia, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na wabunge wanawake.

Mzava anasema miongoni mwa changamoto zilizopo kwa wanawake wanapogombea uongozi ni pamoja na wanawake wengine kufikiria mtu hadi awe kiongozi ni lazima atoke katika familia fulani au lazima awe na chaneli fulani.

“Nawashauri watoto wa kike wanaotaka kuwa viongozi wawe majasiri na waamini kuwa wamezaliwa kuwa viongozi, wanaweza kuwa viongozi katika ngazi na nafasi yoyote,” anasema Mzava.

Akizungumzia suala la sera katika masuala ya uongozi, Mzava anasema suala hilo lipo vizuri kwani hadi sasa kuna wabunge wanawake na madiwani.

“Sera zipo vizuri ni suala la wanawake wenyewe kuamua kujitokeza na kwenda kugombea na kushiriki nafasi mbalimbali na kama marekebisho ni madogo sana ila sera ya wanawake kuwa viongozi imekaa vizuri kuanzia ngazi ya serikali ya mitaa hadi juu na imewataja wanawake katika masuala ya uongozi,” anasisitiza Mzava. Naye Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya anasema mwanamke anapokuwa kiongozi ana majukumu ya kipekee katika kufanya majukumu yake.

Anasema wakati wowote mwanamke anaweza kuwa mtu fulani hivyo anachotakiwa ni juhudi binafsi, kujiamini, kusoma vizuri, kushirikiana na jamii kuthubutu na kuchukua hatua.

“Sasa hivi nafasi za wanawake zinavyoongezeka bado wanaume wanaona kwanini zinaongezeka kwa namna hiyo, lakini kimsingi bado nafasi za wanawake hazijafikia asilimia 50 katika ngazi mbalimbali za maamuzi, kuna haja ya wanawake kuendelea kujitokeza,” anasema Manyanya.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1d78cabf2f56433752195d31cd88d85b.jpg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi