loader
Vita ya Kagera na Idd Amin ilivyomkera Nyerere

Vita ya Kagera na Idd Amin ilivyomkera Nyerere

“WAZAAAZI, wazazi wetu eee! X 2

Mashujaa walokufa, wamekufa kishujaa,

Mashujaa tulorudi, tumerudi kishujaa,

Lengo na nia yetu wazazi ilikuwa moja,

Kuilinda ardhi yetu eeeee X 2.”

 

Hiki ndicho kiitikio cha Wimbo ‘Mashujaa Tulorudi’ uliotungwa na Zahir Ali Zoro katika bendi iliyovuma katika miaka hiyo iitwayo Polisi Jazz Band ‘Kimulimuli’.

 

Wimbo huu uliimbwa baada ya majeshi ya Tanzania chini ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kupata ushindi wa kishindo dhidi ya uvamizi wa Nduli, fashisti Idd Amin na majeshi yake yaliyovamia ardhi ya Tanzania na kusababisha Vita ya Kagera mwaka 1978 hadi 1979 baina ya Tanzania na majeshi ya Uganda.

 

Kabla ya kiitikio hicho, wimbo huo unasema:

 

“Tulikuwa tupo Arua wazazi wetu ee X2

 Kwenye mipaka ya Uganda, Na nchi ya Sudan,

 Kwenye mipaka ya Uganda, Na nchi ya Zaire,

 Kwenye Kijiji cha Kobokoooo.”

Tukiwa tumemaliza kazi jukumu kubwa, Mlotupa wetu wazazi kutoka Tanzania,

Kumfukuza msaliti, Alovamia nchi yetu, Na kumpa adhabu kisago ndani ya mipaka yakeee.

Dikteta kakimbia na Uganda katuachia na vita tumeshinda ooo!

Ukatolewa mwito, Wazazi munatwita wanenu, Turudi nyumbani,

Makubaliano yakafanywa, Mashujaa nusu wabaki, Wakirekebisha mambo,

Tukiwa nusu tukaanza kufunga safari kurudi nyumbani.

 

Tulipofika Kampala, Tukaaga jamaa,

Tulipofika Masaka, Tukaaga jamaa,

Tulipofika Mbarara, Tukaaga jamaa,

Tulipofika Kagera tukakuta wazazi wetuee,

Kwa vifijo na shangwe, Wanenu kutupokeaaa…!”

 

Itakumbukwa kuwa mwaka 1978, majeshi Nduli Amin yalivamia ardhi ya Tanzania, eneo la Mto Kagera, katika Mkoa wa Ziwa Magharibi (Kagera) na kufanya madhara makubwa dhidi ya mali na wananchi wa mkoa huo.

Hali hiyo, ikamfanya Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kutangaza vita kati ya Tanzania na Uganda ili kulinda na kuikomboa ardhi ya Tanzania na watu wake.

 

Huyo ndiye Nyerere; mjukuu wa Chifu Burito; aliyezaliwa Aprili 13, 1922 na kufariki Oktoba 14, 1999.

 

Sasa inatimia miaka 100 tangu kuzaliwa kwake. Waziri Mkuu na Rais wa kwanza wa Tanzania aliyepigania ukombozi wa Tanganyika na Bara la Afrika kwa ujumla na kuiwezesha Tanganyika kutoka kwenye makucha ya ukoloni Desemba 9, 1961, kisha kuiunganisha na Zanzibar kupata Tanzania, Aprili 26, 1964.

 

Hatasahaulika kwa uongozi na ushujaa wake kwa Tanzania na Bara la Afrika.

 

MAMBO YALIVYOANZA VITA YA KAGERA

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, uhusiano wa Tanzania na Uganda ulidorora tangu Januari 25, 1971, Amin alipoipindua serikali halali ya Uganda iliyoongozwa na Rais Milton Obote aliyekuwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola.

Chanzo kimoja mtandaoni kinasema: “Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, akampa Obote na wenzake 2,000 hifadhi ya kisiasa. Idd Amin hakufurahishwa na hilo kwani aliamini kwamba Nyerere anamuandaa Obote aje kumpindua, kwa hiyo akapanga kumdhibiti kabla hajampindua... Akaivamia Tanzania.”

Januari 30, 1978, majeshi ya Amin yalipovamia Tanzania na kuvunja Daraja la Mto Kagera, aliutangaza Mkoa wa Kagera kama sehemu ya Uganda. Hadi sasa Watanzania wanasema: “Huu ulikuwa uchokozi mkubwa.”

Historia na vyanzo mbalimbali zinabainisha kuwa kutokana na uchokozi huo, Nyerere alimsihi Amin kuondoa majeshi yake, lakini nduli Amin akakataa.

Nyerere akaziomba jumuiya za kimataifa kulaani uvamizi wa Idd Amin, lakini cha ajabu, dunia ikakaa kimya. “Akajiongeza” na kutangaza vita iliyoanza Oktoba 30, 1978.

Baadhi ya mambo yaliyowasha na kusababisha vita ni uongo alioupika Nduli Amin huku vyombo kadhaa vya habari vikiutangaza kama kwamba ndio ukweli.

Miongoni mwa uzushi wa Amini dhidi ya Tanzania ulikuwa ni pamoja na madai kuwa majeshi (Watanzania) yako Uganda yanapiga na kuua watu yakisaidiwa na majeshi kutoka Cuba.

Wakati anatangaza vita, Nyerere aliweka bayana akisisitiza juhudi zilizofanywa na Tanzania kukanusha na kupuuza uongo huo, lakini ndege kadhaa za Amini zilikuwa zikiingia Tanzania na kurusha risasi zikiwamo mbili zilizofanya shambulizi Kyaka kwa kutumia mabomu, japo zilipigwa na kuanguka.

Kilichokera na kuibua hasira zaidi za Watanzania wakiongozwa na Rais wao, Julius Nyerere, ni namna majeshi ya nduli Amini yalivyovamia eneo la Tanzania hadi Kyaka huku mwenyewe akikana na kusema Tanzania ndio imeingia Uganda.

 “Hatimaye,” Nyerere akasema: “Alitangaza (Amin) kuwa kweli majeshi yake yameingia na kuchukua sehemu ya Kaskazini ya Kagera na sasa inakuwa sehemu ya utawala wa kijeshi wa Uganda.” 

Hilo likiunganishwa na ukimya wa jumuiya za kimataifa, likamuudhi zaidi Nyerere na Watanzania kwa ujumla.

Akasema: “Sasa kazi imebaki moja kwa Watanzania; ni kumpiga. Uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo… Tunataka dunia ituelewe hivyo kwamba hatuna kazi nyingine…”

Akawataka hata marafiki wa Tanzania wanazungumzia masuala ya suluhu waelewe hivyo maana pia ikumbukwe kuwa, Amini aliwahi kusema mpaka wa Tanzania na Uganda ni Mto Kagera huku akijua wazi kuwa Mto Kagera ni sehemu ya Tanzania.

Kwa uchungu jemedari huyo wa Tanzania akasema: “Kama Amini angesema ni adui, tungeendelea kumpuuza kama ni maneno tu, lakini kufanya kitendo cha uadui, sasa tumfanye adui na amekuja mwenyewe na ameingia mwenyewe…”

Akawatia ari Watanzania na wakazingatia ukweli kuwa hayo sasa hayakuwa mapambano ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pekee, bali Watanzania wote, hivyo ukawa wajibu wa kila mmoja.

Nyerere akawaambia Watanzania: “Tunamwondoa nyoka katika nyumba yetu… Msibabaike; tulieni… Mtaona vitendo tutakavyofanya tangu sasa hadi kazi ya kumpiga mshenzi huyu itakapoisha….”

Ndipo vita ikaanza. Nyimbo mbalimbali za uzalendo na kuwatia nguvu vijana zikaimbwa kwenye mikusanyiko na sehemu mbalimbali zikiwamo shuleni na katika mikutano.

 

Miongoni mwa nyimbo hizo ni ule ulioimbwa na Mwenge Jazz Band uitwao, “Joka” usemao:

 “Joka hiloo joka, liengia chumbani x2

Watoto wamechachamaa joka kulitoa ndani;

Joka limejaa tele chini ya uvungu…

Joka hilo si lingine bali ni Amini,

Limeingiza majeshi nchini mwetu na kuchukua ardhi yetu,

Si lingine, bali ni Amini…”                               

 

Wimbo mwingine uliochochea ari miongoni mwa nyingi ni ule ulioimbwa zaidi hata na wanafunzi katika mchakamchaka ni ule usemao:

“Idd Amin akifa, mimi siwezi kulia,

nitamtupa Kagera awe chakula cha mamba…”

Kwa uongozi wa Nyerere, kila Mtanzania akashiriki vita kwa namna moja hadi nyingine. Mwenye shilingi 100, akatoa; mwenye kuku akatoa, mwenye ng’ombe akatoa na hata mwenye usafiri akatoa. Vijana mbalimbali wakajitokeza kwa ari na kujiunga na jeshi ili kumkomesha adui.

Watanzania waliendelea kuwa na imani kwa vijana wao waliotumwa ‘kumtoa nyoka chumbani’.

Beda Msimbe wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na mzaliwa wa mkoani Morogoro, anasema wakati huo alikuwa akisoma katika Seminari ya Mtakatifu Petro (St Peter) iliyopo Morogoro.

 

 

“Watu hatukuwa na hofu kabisa kwa kuwa tulikuwa na imani na jeshi letu na pia, mara kwa mara wakazi wa mkoa huo wenye milima mingi mara nyingi walikuwa wako tayaritayari kiusalama kwa hiyo hatukuwa na hofu kabisa na badala yake tulikuwa tukiona magari na vifaa vya jeshi watu wanashangilia kwelikweli,” anasema Msimbe.

 

Jeshi la Tanzania likaungana na vikundi mbalimbali vya Waganda vilivyokuwa vikipinga utawala dhalimu wa Amin.

 

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi akatuma wanajeshi takribani 2,500 kumsaidia Idd Amin wakiwa na silaha za kisasa.

 

Hata hivyo, Walibya hao na Wapalestina wakajikuta peke yao ‘mstari wa mbele’ huku wanajeshi wa Uganda wakirudi nyuma. Askari wa Libya pamoja na Palestina wakatekwa. Kazi ikafanyika kwelikweli; Amini na majeshi yake wakakiona cha moto. Akaikimbia Uganda kwenda Libya na baadaye Saudi Arabia baada ya kushindwa.

 

Mashujaa wa Tanzania wakarudi nyumbani wakiimba kwa ushujaa:

“…Mashujaa tulorudi, tumerudi kishujaa,

Lengo na nia yetu wazazi ilikuwa moja,

Kuilinda ardhi yetu eeeee X 2.”

 

Huyo ndiye Nyerere aliyeamini kuwa Tanzania haiwezi kusema ipo huru, kama nchi nyingine za Afrika bado zinatawaliwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6256f47a271f866f5cabed1ae6b46641.jpg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus   

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi