loader
NYANYA CHUNGU: Zao la kukuza uchumi, faida mwilini

NYANYA CHUNGU: Zao la kukuza uchumi, faida mwilini

NYANYA chungu ni zao la jamii ya mbogamboga linalotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mboga ama dawa. Ngogwe kwa jina jingine ni zao la kitropiki linalotoa mazao yake kama matunda na kutumika kama mboga.

Wataalamu wanasema kuna aina mbalimbali za nyanya chungu, zipo za asili ambazo ni chungu na nyingine chotara ambazo si chungu kama za asili.

Rangi ya matunda huwa kijani kibichi au kijani-njano au njano-nyeupe, na yakipevuka kabisa hugeuka mekundu. Matunda yakifikia hatua ya kupevuka huwa hayafai tena kuliwa, ila kwa kutoa mbegu za kupanda. Matunda yake hupikwa au kukaangwa na kufanywa mchuzi au huchanganywa na mboga zingine.

Zao hili hustawi vizuri maeneo yenye baridi ya wastani na joto la kuanzia nyuzi joto 25 hadi 35, hupendelea udongo tifutifu usiotuamisha maji na wenye rutuba. Endapo itatumika mbolea ya samadi na mboji pamoja na mbolea za viwandani, zinastawisha vizuri zao hilo.

Nyanya chungu lina wingi wa vitamini ikiwemo A, B, C, K pamoja na madini hivyo husaidia kwenye afya. Kutokana na umuhimu wa zao hilo, watafiti wakiwemo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mikocheni, Dar es Salaam, wametafiti mbegu bora inayokinzana na magonjwa pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.

Katika siku za karibuni watafiti hao wa Mikocheni walitoa elimu ya matokeo ya utafiti walioufanya kupitia Mradi wa Kuendeleza Zao la Nyanya Chungu kwa wakulima 123 pamoja na maofisa ugani 29 eneo la Chambezi, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mratibu wa Mradi huo, Dk Ruth Minja anasema wanafanya utafiti huo ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwenye uzalishaji wake, kwa zao hilo muhimu ambalo linazalishwa na wakulima wengi katika mikoa mbalimbali.

“Zao la nyanya chungu lina faida za kiafya, viinilishe vitamini A, B, C na madini K, pia ni dawa. Majani na matunda husaidia kupunguza matatizo ya tumbo, shinikizo la damu la kupanda, kisukari, moyo pamoja na njia ya mkojo.

“Zao hili pia huchangia upatikanaji wa kipato hasa kwa vijana na wanawake wanaojishughulisha na kilimo cha nyanya chungu,” anasema.

Dk Minja akitoa elimu ya zao hilo kwa wakulima hao, anasema TARI inafanya utafiti huo kwa kuwa changamoto kubwa inayojitokeza kwenye uzalishaji wa zao hilo ni ugonjwa wa mnyauko unaosababishwa na fangasi na bakteria Anasema kupitia mradi huo imegundulika kuwa mnyauko huo kwa kiasi kikubwa unasababishwa na fangasi aina ya ‘Fusarium’.

“Watafiti wa TARI Mikocheni kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ikiwemo National Institute of Agricultural Botany (NIAB), Chuo Kikuu cha Uganda Christian, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Masuala ya Kilimo Misitu (ICRAF) na The World Vegetable Center, kupitia mradi huo wamefanya tafiti ambazo zinalenga kutatua matatizo ya uzalishaji wa nyanya chungu.

“Pamoja na upatikanaji wa mbegu zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na ukame. Utafiti ulilenga upatikanaji wa mbinu ambazo ni rafiki kwa mazingira mfano matumizi ya teknolojia za kibailojia, mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya visumbufu pamoja na kufuata kanuni bora za kilimo,” anasema.

Anasema wakulima na wadau wa kilimo walipata elimu ya namna ambavyo matumizi ya kanuni bora za kilimo ikiwemo upatikanaji wa mbegu safi zinazopaswa kupandwa kwenye kitalu safi, zikahamishiwa kwenye shamba safi na matunzo bora ya mimea, vinavyoweza kudhibiti au kuangamiza kabisa ugonjwa wa mnyauko kwenye zao la nyanya chungu. “Usafi unamaanisha pasiwepo na vimelea vya ugonjwa.

Ili kufanikisha hilo watafiti walihimiza kufanya mzunguko wa mazao na pale inapogundulika kuwa tayari ugonjwa uko shambani basi pasipandwe nyanya chungu au jamii ya nyanya chungu kama pilipili hoho, nyanya, viazi mviringo, kwa kuwa navyo hushambuliwa na ugonjwa huo kwa muda wa miaka mitatu.

“Watafiti tuliwatembeza wakulima kwenye mashamba manne ambayo yalipandwa nyanya chungu kwa kutumia mbinu mbalimbali kudhibiti ugonjwa wa mnyauko. Mashamba haya yalipandwa siku moja kwa kutumia mbegu aina moja iliyoandaliwa pamoja na matunzo yalikuwa sawa,” anasema.

Ofisa Kilimo kutoka Wilaya ya Bagamoyo, Patrick Amon, anasema zao hilo ni muhimu kwa kuongeza lishe na kipato kwa wananchi, pia aliishukuru TARI kwa elimu hiyo waliyoitoa kwa wakulima ya kujifunza kwa vitendo na kujionea matokeo ya utafiti.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mkulima, Grancia Msanisa anasema wataitumia vizuri elimu waliyoipata ili kuongeza mavuno ya zao hilo ikiwa ni pamoja na kuisambaza elimu hiyo kwa wengine.

Mkulima mwingine, Robert John, anasema matunda ya nyanya chungu yaliyovunwa yanatakiwa yatumike ndani ya wiki moja tangu kuvunwa. Lakini pia yanaweza kusindikwa ili kuwa unga kwa kuchagua nyanya chungu bora kisha zioshwe vizuri, baada ya hapo zikatwekatwe ili kutengeneza vipande vidogodogo kisha vitandazwe kwenye mkeka au turubai safi.

Baada ya hapo unaweza kuanika vipande hivyo vya nyanya chungu juani hadi vikauke, kisha visagwe kwa kutumia mashine kisha wanaweza kutunza unga huo kwa kifaa ambacho hakiingizi hewa kwa matumizi.

Unga wa nyanya chungu unaweza kutumia kwenye maharage, karanga, nyama na mboga nyingine. Mboga iliyowekwa unga wa nyanya chungu inakua tamu na inakua na virutubisho vya kutosha.

Ni ukweli kwamba utafiti ni tiba kwa kilimo kwa kuwa watafiti wanapambana ili kuhakikisha kuwa mbegu bora na safi zinapatikana kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, pia zenye ukinzani wa wadudu.

Kituo hicho cha utafiti wa kilimo Mikocheni ni moja ya vituo 17 vya TARI kilianzishwa Machi 1996 na kupewa majukumu matatu ikiwemo kutafiti na kuliendeleza zao la minazi, kutafiti mifumo bora na endelevu ya kilimo cha mazao miti katika ukanda wa Pwani pamoja na kukuza utafiti wa bioteknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika sekta ya kilimo.

Kituo hicho kina vituo vidogo viwili, Mkuranga na Chambezi, Bagamoyo vyenye jumla ya hekta 700 kwa ajili ya majaribio.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e6269bb35a23447cb1f3032b68e53616.JPG

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi