loader
Usivute sigara hadharani unaua wenzako, utafungwa

Usivute sigara hadharani unaua wenzako, utafungwa

MATUMIZI mengi ya bidhaa za tumbaku ni hatari kwa maisha ya mtumiaji kutokana na athari zake zinazohusisha hata watu wasiotumia moja kwa moja.

Miongoni mwa madhara makubwa ya matumizi ya tumbaku ikiwemo sigara na ugoro, ni kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile kuharibu mapafu, moyo, saratani ya mfumo wa hewa, kisukari, mishipa ya damu na uhatarishi wa shinikizo la juu la damu.

Tumbaku hupunguza kiwango cha oksijeni inayoweza kusafirishwa na damu na hivyo kuwa na uwezekano wa kuifanya damu kuganda jambo linaloweza kusababisha magonjwa mengine ya moyo ambayo nayo husababisha kiharusi au kifo cha ghafla.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, takribani watu milioni sita hufariki kutokana na matumizi ya tumbaku au kukaa karibu na mvutaji. Hali hii huchangia asilimia sita ya vifo vya wanawake na asilimia 12 ya vifo vya wanaume kwa mwaka.

Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku vitaongezeka na kufikia zaidi ya milioni nane kwa mwaka.

Hata hivyo, mtu anaweza kuepuka matumizi ya tumbaku na hivyo kuwa na dunia ya watu wasiotumia tumbaku kabisa.

Aidha, kila mwaka watu 600,000 hufariki kutokana na kuvuta moshi wa wavutaji kwa kuwa karibu na wavutaji ambapo kati yao asilimia 28 ni watoto.

KWANINI VIJANA WANATUMIA TUMBAKU

Kwa mujibu wa kijana Gerald Mashine, vijana wengi wanajiingiza kwenye matumizi ya tumbaku kutokana na kuiga maisha.

Anasema hali hiyo ya kuiga inasababisha na kutokuwa na uelewa kuhusu madhara ya bidhaa hizo kwa afya.

Anasema mtindo wa kutokuzingatia tahadhari inayotolewa kupitia pakiti ya sigara inakuwa tatizo zaidi.

PIPI, BAZOKA DHANA ILIYOSAMBAA KUACHA SIGARA

Miongoni mwa dhana inayosambaa katika jamii ni namna ambavyo mtu anaweza kuacha sigara au bidhaa nyingine za tumbaku.

Amideus John, mkazi wa Dar es Salaam, anaamini kuwa matumzi ya pipi kifua na bazoka inasaidia kuacha matumizi ya sigara.

“Mimi nimesikia ukitaka kuacha sigara kuna vitu vidogo vidogo kama pipi mfano ukiwa na hamu unachukua pipi kifua na kuanza kutumia hivyo wanaamini kama unataka kuacha kuvuta sigara weka pipi zako 10 mifukoni ukipata hamu ukatumia, hamu ya sigara inatoka.

“Njia nyingine ni ‘bablishi’ nayo huwa wanafanya hivyo hivyo ukisikia hamu ya kuvuta sigara unachukua unatafuna hivyo vinaweza kufanya ukaacha kuvuta sigara,” anasema John.

Anaeleza kuwa kwa kutumia njia hiyo wapo watu watatu anaowafahamu walifanikiwa kuacha sigara.

“Nawashauri vijana unaposema ujiingize kwenye makundi au vitu visivyo vya lazima inaweza kukuharibia maisha yako na utapoteza fedha zako,” anasisitiza.

JE NJIA HIZO ZINASAIDIA

Mkaguzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki, Jafari Mtoro, anasema ili mtu aache kuvuta sigara ni lazima aamue na aazimie kufanya hivyo.

Anasema msaada wa kisaikolojia una maana kubwa katika kuacha kutumia tumbaku hivyo ni muhimu watumiaji kuwatafuta wataalamu wa saikolojia.

“Kuhusu suala la pipi na ‘bablishi’ hilo hatuna uhakika nalo ila suala la kuacha sigara ni maamuzi ya mtu mwenyewe au pia kupata msaada wa kisaikolojia,” anabainisha Mtoro.

WANAOVUTA SIGARA HADHARANI KUSHTAKIWA

TMDA imesema itamchukulia hatua za kisheria mtu atakayebainika kutumia bidhaa za tumbaku hadharani hasa sigara kutokana na madhara yanayotokea.

Sheria ya Udhibiti wa Tumbaku Sura ya 121 inakataza watumiaji kuvuta sigara hadharani ambapo adhabu ni faini Sh 200,000 au kifungo miezi sita.

Kaimu Meneja TMDA Kanda ya Mashariki, Gloria Matemu wakati akitoa elimu katika kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Gerezani, Dar es Salaam, alisema sheria hizo zinakataza watumiaji kuvuta bidhaa za tumbaku hadharani. 

Anasema kuwa pia sheria inakataza kutoa matangazo au kudhamini matangazo kwa kupitia vyombo vya habari, vipeperushi au sauti zilizorekodiwa.

"Tumefika hapa kwa lengo la kutoa elimu kama mnavyojua TMDA iko chini ya Wizara ya Afya ina jukumu la kulinda jamii kupitia Tangazo la Serikali namba 360 ya tarehe 31/4/2021 imekasimishwa jukumu la kudhibiti bidhaa za tumbaku,” alisema Matemu.

Matemu anasema kwa siku tano za Aprili mwaka huu wametoa elimu katika Wilaya ya Ilala lengo likiwa kuwajulisha wananchi kwamba TMDA sasa inadhibiti bidhaa za tumbaku lakini pia kuwapa uelewa wa matakwa ya sheria.

Anasema kwa siku hizo wamefanikiwa kupita maeneo mengi ambapo watu 1,800 wamefikiwa na elimu kwenye masoko, hoteli, kumbi za starehe, vyombo vya usafiri, vikundi mbalimbali vya madereva wa bajaji na pikipiki.

WATAKIWA KUTENGA MAENEO

TMDA imewataka wamiliki wa maeneo ya umma kutenga sehemu maalumu kwa ajili ya uvutaji wa bidhaa za tumbaku.

Aidha, sheria pia inataka kuwekwa kwa mabango yanayokataza uvutaji wa sigara katika maeneo yasiyotakiwa.

Mkaguzi wa TMDA Kanda ya Mashariki, Mtoro, anasema utekelezaji wa matakwa ya sheria ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku ni jukumu lao.

Anasema kuwa sheria imeweka masharti mbalimbali kwa lengo la kulinda watu kutokana na bidhaa za tumbaku ikiwemo kuzuia uvutaji wa sigara katika maeneo ya watu au ya umma.

“Sheria inataka ziwekwe alama zitakazowezesha kubaini kama kuna sehemu isiyotakiwa mtu anavuta sigara, kama mtu anataka kuvuta sigara aweze kwenda kwenye chumba au eneo maalumu ambalo atavuta bila kuathiri afya za watu wengine,” anabainisha Mtoro.

Anasema matakwa hayo ya sheria yasipozingatiwa wengi wataugua moyo, mapafu, saratani na magonjwa mengine yanayotokana na matumizi ya tumbaku.

Mtoro anasema kwa sehemu kubwa wamebaini maeneo mengi hayajaanza kutekeleza matakwa ya sheria kwani hayana alama ya kuzuia watu wasivute sigara.

Anasema hatua ambayo TMDA imechukua kwanza ni kutoa elimu kwa wananchi kufahamu kuwa hairuhusiwi kuvuta sigara kwenye mikusanyiko ya watu.

Anawataka wamiliki wa vyombo vya umma, wasimamizi wa masoko, vituo vya basi, hospitali, hoteli na kwingine kuhakikisha kuna eneo maalumu la kutumia bidhaa za tumbaku na pia kuna mabango ya kukataza maeneo yasiyoruhusiwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/aa048cb4d8013f77162b00d08937f468.jpg

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na ...

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi