loader
Serikali kusimamia fedha za uwajibikaji kwa jamii Tarime

Serikali kusimamia fedha za uwajibikaji kwa jamii Tarime

SERIKALI kuu sasa itakuwa inaweka mkono wake katika mapato na matumizi ya fedha zinazotolewa na migodi ya madini katika kutekeleza sera ya kuwajibika kwa jamii (CSR) katika Mkoa wa Mara.

Kwa msingi huo, sasa kila kitu kitawekwa wazi kupitia mabaraza ya madiwani pamoja na kuwajibika kuzisimamia kwenye vipaumbele vya maendeleo, kwa mujibu wa miongozo itakayotolewa na serikali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa alisema hayo juzi jioni baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nyarukoba na Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Kata ya Nyamwaga na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.

Licha ya kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime, Apoo Tindwa ambaye wakati uamuzi huo ukitangazwa alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, mkoani Mtwara, Bashungwa alimtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo wa sasa, Solomon Shati, kuongozana naye jijini Dodoma ili ‘wakayajenge’.

“Kwa namna fedha za CSR zilivyokuwa zinatumika, serikali tumeamua kusimama kati kwa niaba ya wananchi, kila aliyefuja fedha hizi atazitapika,” alisema Waziri Bashungwa. Awali, Diwani wa Kata ya Nyamwaga, Mwita Magige alilalamikia kasi ndogo ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya hiyo na baadaye malalamiko hayo yalitiwa nguvu na Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara kabla Bashungwa hajamtaka Shati kueleza wananchi kinachoendelea katika mradi huo.

Shati alimlaumu mkandarasi (SUMA JKT) kuwa anawachelewesha kwa kupeleka mafundi wachache, licha ya kupewa mahitaji yote na kwamba alishawapa taarifa ya kutoridhishwa na utendaji wao mara tatu, tena kwa maandishi lakini hawabadiliki na mpaka wakati huo ilikuwa akiwapigia simu, hawapokei.

Bashungwa alielekeza SUMA JKT kufanyia kazi suala hilo huku Shati akipewa maelekezo ya kuongozana naye na kwamba ikibainika anahusika kuchelewesha miradi, atabaki huko huko ikiwa tofauti atarudi kwa sharti la kukamilisha miradi ndani ya wakati. Pia Bashungwa alielekeza Mkurugenzi wa Afya kuhakikisha ifikapo Juni 30, mwaka huu, kituo hicho cha afya kiwe kinatoa huduma, huku akitilia nguvu agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) linalotoa wiki mbili kupeleka mahakamani waliofanya ubadhirifu wa fedha za mradi huo.

Aidha, Bashungwa alielekeza Mkurugenzi wa Afya, Mkuu wa Mkoa Hapi na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk Juma Mfanga kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa hospitali ya wilaya hiyo, ambao walilalamikiwa na wananchi kwa makosa mbalimbali ikiwamo utovu wa nidhamu na wizi.

Aliwaonya watumishi wanaioshi nje na halmashauri hiyo akiagiza ifikapo Juni 30 mwaka huu, wawe wamehamishia makazi yao ndani ya halmashauri hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuza kazi. Shati alielekezwa kuwasilisha majina yao kwake.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/c19c4dcabf483d3320cc88b80595126d.jpeg

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa ...

foto
Mwandishi: Na Editha Majura, Tarime

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi