loader
Wizara yaita maoni kuboresha Sheria ya Ununuzi wa Umma

Wizara yaita maoni kuboresha Sheria ya Ununuzi wa Umma

WIZARA ya Fedha na Mipango imetoa wito kwa wadau wa sekta ya ununuzi wa umma nchini kutoa mawazo ili kuwezesha maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa lengo la kuleta tija kwa serikali.

Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Frederick Mwakibinga, wakati akitoa elimu kuhusu sera, sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma kwa washiriki waliotembelea banda la wizara hiyo, katika wiki ya ununuzi wa umma, jijini Arusha.

Alisema kuna sheria ya ununuzi wa umma sura 410 na kanuni zake ambayo kwa mara ya mwisho ilipitiwa mwaka 2013 na kanuni zake kutoka mwaka 2016. “Tunaendelea kukusanya maoni kutoka makundi mbalimbali na watu wote ambao wanadhani nini kifanyike ili sheria iweze kutekelezeka na iweze kunufaisha nchi.

Hili ni jukumu letu kuhakikisha kuwa eneo la ununuzi wa umma lina sera, sheria, kanuni na miongozo inayokuwa na tija kwa taifa,” alisema. Alisema sheria ya ununuzi wa umma inalinda maslahi ya taifa kwani inawapa wananchi pamoja na wafadhili imani na serikali katika matumizi ya fedha hivyo matumizi ya sheria hayapaswi kuingiliwa na mashinikizo.

Dk Mwakibinga alisisitiza maofisa manunuzi nchini kusimama katika sheria, kufanya kazi kwa nidhamu, kuheshimu taratibu za ununuzi na kuepuka kukiuka matumizi ya sheria kutokana na shinikizo lolote na kuwasiliana na wizara endapo watakutana na changamoto ya shinikizo la aina yoyote.

Aidha, Dk Mwakibinga alisema kuwa Wizara imetoa kanuni za maadili kwa wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma ili kuweza kuwajumuisha wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma kwa kuwa maamuzi yao huathiri ununuzi wa umma. Akizungumza kuhusu wiki ya ununuzi wa umma, alisema kuwa wiki hiyo ni ya muhimu katika kuelimisha umma katika masuala mbalimbali yanayohusu ununuzi wa umma ili kufahamu umuhimu wake.

Alisema kuwa matumizi ya teknolojia katika ununuzi wa umma yanahakikisha eneo hilo linaendeshwa kwa kujali maslahi ya serikali na kushauri watendaji wote kuzingatia sheria, kanuni na kuzingatia maadili. Kongamano la wiki ya ununuzi wa umma limeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini.

Taasisi hizo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/b9c3a7ede5a66ab6f820274efda64b8d.jpeg

WADAU wa Sekta ya Kilimo nchini wameshauriwa ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi