loader
Simba yamaliza hasira kwa Ruvu

Simba yamaliza hasira kwa Ruvu

SIMBA imepunguza gepu la pointi kati yake na Yanga baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 46 na kubaki kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku tofauti ya pointi kati yake na vinara Yanga ikibaki kuwa 10 badala ya 13 za awali.

Mabao ya Simba yalifungwa na Kibu Denis, Larry Bwalya, John Bocco na Hennock Inonga ambaye naye alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja lililofungwa na Kibu dakika ya 39 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Ruvu Shooting na mpira uliookolewa na Jafar Mohamed ulimkuta mfungaji na kupiga shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Ruvu, Mohamed Makaka.

Kipindi cha pili, Ruvu walionekana kukianza kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi huku wakitawala eneo la katikati, lakini kosa lililofanywa na Makaka liliifaidisha Simba dakika ya 66 baada ya Bwalya kufunga bao la pili akimalizia pasi ya Pape Sakho.

Kuingia kwa bao hilo hakukuwakatisha tama Ruvu Shooting kwani waliendelea kupambana kutafuta mabao ya kusawazisha lakini mabadiliko yaliyofanywa na Kocha wa Simba ya kumtoa Meddie Kagere na kuingia Bocco yaliinufaisha Simba baada ya nahodha huyo kuifungia timu yake bao la tatu kwa shuti kali akimaliza pasi nzuri ya Yusufu Muhilu.

Wakati Simba wakiwa bado wanafurahia bao hilo, Haruna Chanongo aliipatia Ruvu Shooting bao la kufutia machozi dakika ya 83 baada ya kutanguliziwa mpira mrefu na nahodha wa timu hiyo, Abdulrahaman Mussa. Kuingia kwa bao hilo ni kama kuliwarudisha mchezoni Simba na kuanza kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Shooting na dakika ya 85 mlinzi wa kati, Inonga aliifungia timu hiyo bao la nne akiunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Sakho.

Katika mchezo wa mapema uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga, wenyeji Coastal Union waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania lililofungwa katika dakika ya 20 na mshambuliaji wake, Abdul Sopu .

Ushindi huo umeiondoa Coastal Union mkiani mwa ligi hiyo na kupanda hadi nafasi ya 12 wakifikisha pointi 24 kwenye msimamo, huku wakibakiwa na michezo saba kabla msimu kumalizika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/39ebb46c81db11eeee9ae6fe482bd77f.jpg

VINARA wa Ligi Kuu, Yanga SC, wanahitaji ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi