loader
Yanga, Prisons kazi moja

Yanga, Prisons kazi moja

YANGA ambao ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, leo wanatakuwa na kibarua kwa kumenyana na maafande wa Magereza Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga haijapata ushindi katika michezo yake miwili iliyopita dhidi ya Simba na Ruvu Shooting, hivyo katika mchezo wa leo utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku, miamba hiyo ya soka nchini inatarajiwa kufanya kila linalowezekana kupata pointi tatu zitakazowaweka katika mazingia mazuri ya kutangazwa mabingwa wapya wa taji hilo msimu huu.

Timu hizo zinakutana zikiwa katika mazingira tofauti, Yanga wapo kileleni wakikusanya pointi 56 na tayari wamecheza mechi 22  sawa na wageni wao Prisons, lakini wapo nafasi ya tatu kutoka mkiani wakikusanya pointi 22.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga,  Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, matokeo ambayo yaliongeza machungu ya maafande hao ambao wamekuwa na mwenendo usio mzuri wakiwa chini ya Kocha Msaidizi, Shaaban Kazumba.

Yanga ambayo inashikilia rekodi ya kutofungwa tangu kuanza kwa ligi ya msimu huu, inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na pointi tatu katika mchezo wa leo kutokana na rekodi yao kwa msimu huu, lakini pia mwenendo wa wapinzani wao Prisons siyo mzuri  kama ilivyokuwa misimu iliyopita.

Kurejea kwenye benchi kwa Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi aliyekosekana kwenye mechi tatu zilizopita kunaweza kuwa chachu ya timu hiyo kurudi kwenye wimbi la ushindi kutokana na mbinu na namna wachezaji wanavyomsikiliza anapokuwa amesimama tofauti na msaidizi wake, Cedric Kaze ambaye katika mechi tatu alizoiongoza timu hiyo ameshinda moja na kupata sare michezo miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nabi alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo wa leo yamekwenda vizuri na wachezaji pamoja na wenzake wa benchi la ufundi ari yao ipo juu kuhakikisha wanachukua pointi zote tatu katika mchezo huo.

“Unapohitaji ubingwa lazima kila mechi upate pointi tatu bila kujali unacheza na timu gani na ipo nafasi gani, hatujapata ushindi  kwenye michezo miwili hivyo mechi ya kesho (leo) ushindi ni jambo la lazima  wachezaji wanalifahamu hilo  na wapo tayari kwa kupambana,” alisema Nabi.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons, Mtupa alisema maandalizi yao yamekamilika na wapo tayari kwa ajili ya kuzipigania pointi tatu ili kujiondoa kwenye ukanda wa kushuka daraja.

 “Tunajua Yanga ina safu kali ya ushambuliaji na sisi Prisons tumejitahidi kurekebisha makosa yetu yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya Kwanza, wachezaji  wote 21 wapo katika hali nzuri ikiwamo kisaikolojia hivyo wapo tayari kucheza na Yanga,” alisema Mtupa.

Mwisho.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ec43c97b84afa8e12881435039ee5661.jpg

VINARA wa Ligi Kuu, Yanga SC, wanahitaji ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi