loader
Samia asikia kilio  cha bei ya mafuta

Samia asikia kilio cha bei ya mafuta

RAIS Samia Suluhu Hassan ameelekeza serikali ijibane na ijinyime ili kupata fedha katika matumizi ya kawaida ya serikali zitakazoenda kutoa nafuu kwa wananchi katika bei ya mafuta kuanzia Juni Mosi mwaka huu.

Amesema katika mwaka ujao wa fedha serikali itachukua hatua za kikodi ili kuwapa wananchi ahueni ya bei ya mafuta. Rais Samia alisema hayo jana alipohutubia taifa kuhusu hali ya bei ya mafuta akiwa Ikulu, Dar es Salaam.

“Pia nimemwelekeza Waziri wa Nishati aende kufafanua zaidi kuhusu hatua hii na hatua nyingine ambazo serikali inatarajia kuzichukua ili kukabiliana nba janga hili kama bunge lilivyotaka kesho (leo) Waziri wa Nishati atatoa maelezo hayo”alisema.

Alhamisi iliyopita Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliitaka serikali leo kutoka na kauli kuhusu hatua za dharura za muda mfupi na za muda mrefu wa kukabili bei ya mafuta.

Rais Samia alisema hatua zaidi za kikodi zitatangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango katika Bajeti ya Serikali mwezi ujao.

Alisema Oktoba mwaka jana alielekeza zipunguzwe tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali kwenye mafuta na uamuzi huo ulisababisha mapato ya serikali yapungue kwa Sh bilioni 102.

Rais Samia alisema serikali inatambua adha inayosababishwa na kupanda kwa bei na haitasita kuchukua hatua stahiki na akasema yapo matukio ya kidunia yanayosababisha bei kupanda ambayo yapo nje ya uwezo wetu.

Rais Samia alisema jambo muhimu ni upatikanaji wa mafuta yenyewe na serikali imefanyika kazi nzuri kuhakikisha nchi haiishiwi mafuta kama ilivyotokea kwenye nchi nyingine.

“Kasi ya kupanda kwa bei za mafuta kumetikisha nchi zote duniani, tajiri na masikini, zenye kuzalisha mafuta na zenye kagiza mafuta…Tanzania kama nchi inayoagiza mafuta haijapona kwenye janga hili. Kwa miezi 18 iliyopita bei imekuwa ikipanda kwa kasi” alisema na akawapa pole Watanzania kwa adha wanayopata kutokana na ongezeko la bei ya mafuta.

Awali usiku wa kuamkia jana Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza viongozi watafute suluhisho la haraka kukabili tatizo la upandaji wa bei ya mafuta.

Akizungumza katika kikao cha dharura Ikulu ya Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana alichoitisha kujadili tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta nchini alitaka kuwepo na suluhisho la haraka.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Nishati, January Makamba, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata na makatibu wakuu wao.

Wiki iliyopita, Majaliwa alisema Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.

Aidha, wiki iliyopita, January aliwaeleza wabunge jijini Dodoma kuwa bei ya mafuta imepanda kutokana na mambo kadhaa zikiwamo gharama ya kununua mafuta, usafirishaji wake, kodi na gharama za biashara.

Alisema Machi mwaka huu bei ilipanda zaidi kwa pipa kuliko miaka 14 iliyopita ikafikia Dola za Marekani 137 ndio maana mwezi huu bei zimepanda na kufikia hali ilivyo sasa ambako kwa Dar es Salaam bei ya kikomo ya petroli ni Sh 3,148 kwa lita, dizeli ni Sh 3,258 na mafuta ya taa ni Sh 3,112 kwa lita

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bfa1edc7b44eff5a0f2cbea801b02d97.jpg

Rais Samia Suluhu Hassan, ametajwa kuwa miongoni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi