loader
Chongolo ahimiza serikali ruzuku ya mbolea

Chongolo ahimiza serikali ruzuku ya mbolea

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametaka kuharakishwa kwa mpango wa upatikanaji wa ruzuku kwenye mbolea.

Alisema hayo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha mbolea ya asili cha Intracom kilichopo eneo la Viwanda Nala ambacho kinajengwa na mwekezaji kutoka Burundi.

Kiwanda hicho kinatarajia kuanza uzalishaji wa awali Juni na Julai mwaka huu na kitatoa ajira 3,000 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 za mbolea ambapo uzalishaji wa awali unatarajiwa kuanza hivi karibuni, ni uzalishaji wa tani 200,000.

Chongolo alitoa maagizo hayo kwa Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo kuharakishwa mchakato wa upatikanaji wa ruzuku kwenye mbolea.

Alisema Rais Samia hivi karibuni aligawa vitendea kazi kwa maofisa ugani na kutoa maelekezo mahususi ya kutaka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo kukaa pamoja ili kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka.

Alisema baada ya maagizo hayo ya Rais waliona kuwe na mpango wa kujua mahitaji ya mbolea kwa nchi na kiasi cha mbolea kinachohitajika ni tani 700,000 na kusimamia hatua kwa hatua upatikanaji wa mbolea hiyo ili iwafikie wakulima kwa wakati. Chongolo alisema kuwa kiwanda hicho uzalishaji wake wa awali utakuwa ni tani 200,000 na wanatakiwa kuwe na mkakati wa kupata tani 500,000 kabla ya msimu kuanza.

Alisema kuwa kuna changamoto ya kampuni za serikali huku akizitaka kufanya kazi kwa ushindani na kwa utaratibu na kusimamia bei ya mbolea.

Chongolo alisema kuwa katika msimu uliopita wakulima walipata changamoto ya upatikanaji wa mbolea, hali iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa ugonjwa wa Covid-19 na mbolea ilikuwa ikigombewa kwenye soko na hata inapotoka nchini inapanda bei na kuwaumiza wakulima.

Aliwataka watu wenye mitaji kufika Dodoma kuwekeza, uwekezaji wa kimkakati. Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Kanda ya Kati (TIC), Abubakari Ndwata alisema uwezekaji huo umetumia karibu Sh bilioni 420 na baada ya kukamilika watu 3,000 watapata ajira ya moja kwa moja.

Alisema kuwa mwekezaji huyo ana soko kubwa hadi Jumuiya ya Ulaya. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka alisema juhudi zimefanyika na sasa kiwanda kimefikishiwa umeme na maji.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita nne ipo kwenye mpango. Kwa upande wake msimamizi wa ujenzi wa kiwanda hicho, Diev Donne alisema kazi za ujenzi zinaendelea vizuri na uzalishaji wa awali unatarajia kuanza hivi karibuni.

Ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Itracom Fertilizer Limited utagharimu Dola za Marekani milioni 180. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe Aprili 4, mwaka huu wakati wa ugawaji wa vitendea kazi kwa maofisa ugani alitoa ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan la kumtaka Rais kuagiza Benki Kuu watenge Sh trilioni moja kwa ajili ya sekta ya kilimo.

“Nakuomba Sh bilioni 150 tuiweke kwenye benki tuanze kutoa ruzuku ya mbolea kwa kuanzia msimu ujao wa kilimo. Nikuhakikishie fedha hii haitapotea,” alisema.

Ujenzi wa kiwanda hicho ni matunda ya ziara aliyoifanya Rais Samia nchini Burundi Julai mwaka jana.

Katika ziara hiyo Rais Samia alikuta kiwanda cha mbolea ya asili cha Itracom Fertilizer Limited ambacho ni kiwanda kikubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na moja ya mazungumzo ni kuwa kile kiwanda kijengwe pia hapa Tanzania na mara moja wawekezaji hawa walikubali kuja kujenga kiwanda mkoani Dodoma.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a9e02a319d7a0f72b376c33fd9363d89.jpg

Rais Samia Suluhu Hassan, ametajwa kuwa miongoni ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi