loader
Umoja wa Afrika waazimia kuwa na jeshi

Umoja wa Afrika waazimia kuwa na jeshi

MAWAZIRI wa ulinzi, amani na usalama kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wameazimia kuanzisha jeshi la pamoja na kituo ili kupambana na changamoto ya ugaidi katika nchi wanachama wa umoja huo.

Kauli hiyo imetolewa nchini Ethiopia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax baada ya kumalizika kwa mkutano wa mawaziri hao ambao hapo awali ulitanguliwa na mkutano wa wataalamu ukijumuisha wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nchi wanachama wa umoja huo.

“Tuna tatizo la ugaidi Kusini mwa nchi yetu lakini likiwa zaidi upande wa Msumbiji, lakini kama mnavyofahamu tatizo la ugaidi sio la nchi moja na nguvu ya nchi moja peke yake inakua vigumu kutokana na jinsi magaidi wanavyofanya kazi zao, tumejadili na kwa kutambua umuhimu wake imepelekea kuwa na pendekezo la kuanzisha kituo na jeshi na nchi wanachama watachangia askari ili kupambana na changamoto ya ugaidi na nyingine za ulinzi na usalama kwa kubadilishana taarifa, uzoefu, kutoa mafunzo ambayo hiyo itaongeza nguvu katika mapambano hayo,” alisema Dk Tax.

Akizungumza juu ya ushirikiano wa nchi za Afrika kukabiliana na changamoto za uhalifu unaovuka mipaka, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema wameweka mikakati mbalimbali huku akiweka wazi jitihada za pamoja katika kupambana na ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya.

“Katika mambo ambayo tumeazimia kuyapa mkazo maalumu kupitia vikosi vyetu ni suala zima la ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya kwa ujumla wake…imekua jambo la faraja kuona nchi zote wanachama wamekubaliana na wazo hilo huku tukisubiri idhini ya wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika kutoa maamuzi katika kikao kinachotarajiwa kufanyika muda si mrefu kutoka sasa,” alisema.

Akielezea majukumu waliyopeana wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nchi wanachama, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro alisema wao kama wakuu wa vyombo wameazimia kubadilishana taarifa hasa za uhalifu unaovuka mipaka.

“Tumezungumzia suala la uhalifu Afrika na hasa yale makosa yanayovuka mipaka na moja kati ya makosa ambayo yamejitokeza kwa wingi sana ni ugaidi… tumeuzungumza ugaidi kwa mapana sana kwa sababu utaona nchi nyingi sana zimeathirika na ugaidi lakini unaweza kuangalia nchi kama wenzetu Msumbiji, Afrika Magharibi ugaidi umekua ni mkubwa sana.

“Kwa hiyo suala ambalo limesisitizwa katika hili ni suala la kubadilishana taarifa, kwani ni suala la msingi sana na huwezi kupambana na ugaidi bila kubadilishana taarifa maana ni makosa ambayo leo wanafanya hapa kesho wanaondoka wanaenda kufanya nchi nyingine,” alisema.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Meja Jenerali Jacob Mkunda akimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/18a176c6b7cf662031efc920b3b0d847.jpg

BAADHI ya wanaume katika Kijiji cha Ikondamoyo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Addis Ababa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi