loader
Wabunge waliotimuliwa Chadema watinga bungeni

Wabunge waliotimuliwa Chadema watinga bungeni

BAADHI ya wabunge wa viti maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walioshindwa rufaa yao ya kupinga kusimamishwa na chama chao, wametinga bungeni, huku Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila, akiwasilisha bungeni barua ya uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho kuhusu kuwavua uanachama.

Jana asubuhi wabunge hao takribani wanane walihudhuria vikao vya Bunge isipokuwa Mwenyekiti wao, Halima Mdee, Ester Bulaya, Naghenjwa Kaboyonga na wengine 11.

Aliyeanza kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge ni Ester Matiko saa 2:50 asubuhi akifuatiwa na Salome Makamba na wengine waliingia baada ya kikao cha Bunge kuanza. Wabunge hao walihudhuria kikao hicho cha bunge ikiwa ni siku mbili tu baada ya kushindwa rufaa yao ya kupinga kuvuliwa uanachama.

Akizungumza na gazeti hili nje ya viwanja vya Bunge, Kigaila alisema amewasilisha barua ya uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema juu ya kukubaliana na adhabu iliyotolewa na Kamati Kuu Novemba 27, mwaka jana ya kuwavua uanachama wabunge hao 19.

“Nimeleta leo barua kwa Spika asubuhi wameipokea saa 2:42 amepokea Katibu wake Muhtasi nilitaka sana nimuone Spika lakini wakasema hajafika na akifika atakuwa anaenda kwenye kikao cha Bunge hatakuwa na muda wa kuonana na mimi,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Sikutaka kuiweka masjala nikaipeleka akaipokea Katibu wake Muhtasi akisimamiwa na Msimamizi Mkuu wa ofisi ile.” Kigaila pia alisema pamoja na kuiwasilisha barua hiyo bungeni alipeleka nakala Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) saa 6:00 mchana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa saa 7:00 mchana.

Kuhusu utaratibu wa kuteua wabunge wengine watakaochukua nafasi za wanachama hao 19, Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa hilo ni suala litakalofanyika baadaye na kwamba hivi sasa wanachotaka ni kuwaondoa waliojiteua wenyewe kuwa wabunge.

Awali, katika kipindi cha asubuhi cha maswali na majibu mmoja wa wabunge hao baada ya kuhudhuria kikao hicho cha Bunge, Salome Makamba aliuliza swali la nyongeza linalohusu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari lililojibiwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Andrea Kundo.

Wabunge waliohudhuria kikao hicho na kushuhudiwa na gazeti hili ni pamoja na Esther Matiko, Salome Makamba, Tunza Malapo, Jesca Kishoa, Annatropia Theones, Asya Mohammed na Stella Fiao.

Gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na Matiko aliyekuwa eneo la Bunge kuzungumzia kuhudhuria kwao bungeni wakati wamevuliwa uanachama alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na zaidi asikilizwe akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji uliokuwa ukiendelea jana.

Aidha, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alipotoka bungeni baada ya kikao cha asubuhi kuahirishwa pia aligoma kuzungumzia suala hilo, akisema atazungumza baadaye.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Haki, Kinga, Madaraka na Maadili ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka alikiri kuwa amesikia suala la wabunge hao 19 kusimamishwa uanachama na Baraza Kuu la chama chao.

“Mimi kama mbunge ambacho ninaweza kusema sisi msemaji wetu mkuu ni Spika Dk Tulia yeye ndio atatuambia kama Mkuu wa Mhimili wa Bunge kuna nini kinaendelea. Kwa sababu yale yaliyotokea kule Chadema sio automatic (moja kwa moja) kwenye Bunge,” alisema Mwakasaka.

Alisema kama mmoja wa viongozi wa kamati ya uongozi ya Bunge hafahamu kama Spika ameshapewa taarifa na baada ya hapo nini kinaendelea.

“Ila wenzetu (wabunge wa Chadema) tumeona wanaendelea na shughuli za Bunge na mpaka sasa tunawatambua kama wabunge mpaka tutakapoambiwa vinginevyo na Spika,” alieleza.

Wabunge wote waliovuliwa uanachama na Baraza Kuu la Chadema ni Mdee, Bulaya, Kaboyoka, Matiko, Kishoa, Malapo, Asya, Theones, Makamba, Fiao, Cecilia Pareso, Agnes Kaiza, Nuzrat Hanje, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga, Felista Njau, Sophia Mwakagenda, Kunt Majala na Conjesta Rwamulaza.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b74b93e50a826cfbac9a2fa1a03f26d1.jpg

MBUNGE wa Kigamboni, Dk Fausitine Ndugulile (CCM) ...

foto
Mwandishi: Na Halima Mlacha, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi