loader
Mradi wa  maji miji 28  wafagiliwa  bungeni

Mradi wa maji miji 28 wafagiliwa bungeni

MRADI wa maji katika miji 28 umewakuna wabunge baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kubainisha mipango ya kuanza kuutekeleza ikiwa ni miaka sita tangu kuanzishwa kwake. Imebainishwa kuwa serikali kwa kushirikiana na serikali ya India kupitia Benki ya Exim - India inategemea kuanza ujenzi wa mradi huo wa miji 28 ya Tanzania Bara na mji mmoja visiwani Zanzibar kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 500.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alitoa taarifa hiyo akisoma makadirio na matumizi ya mapato ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2022/23 bungeni Dodoma juzi.

Alisema hadi Aprili, mwaka huu, taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi katika miji 24 zimekamilika na ujenzi wa miradi katika miji hiyo utatumia fedha za mkopo wa India na miji minne ya Mafinga, Makonde, Songea na Tarime Rorya utekelezaji wake utafanywa kwa kutumia fedha za ndani.

“Mikataba ya ujenzi itasainiwa kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2021/22,” alieleza.

Waziri Aweso alitaja miji hiyo ni Muheza, Wanging’ombe, Kayanga, Makonde, Njombe, Makambako, Manyoni, Songea, Sikonge, Chunya, Kasulu, Kilwa Masoko, Rujewa, Mugumu, Geita, Chato, Zanzibar, Singida Mjini, Kiomboi, Mpanda, Chemba, Mafinga, Urambo, Kaliua, Pangani, Ifakara, Rorya/Tarime na Chamwino. Akizungumzia mradi huo, Mbunge wa Nanyumbu, Yahya Mhata (CCM), alisema wabunge safari hii wana kila sababu ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tangu ameingia madarakani ameleta mageuzi makubwa katika eneo la maji.

“Mama amefanya mageuzi tuwe wakweli na hili limeonekana wazi kwenye mradi wa maji wa miji 28. Kwanza naomba uzinduzi wake ufanyike mapema tena hapa hapa Dodoma ambako wabunge wote wanaoguswa na mradi huu wapo,” alisisitiza.

Wakati akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi (CCM) aliomba kutoa taarifa kwa Mhata na kuunga mkono hoja yake kuhusu mradi huo kwa kusisitiza kuwa mradi huo ulianzishwa tangu mwaka 2016 na umepita chini ya mawaziri takribani wanane bila kutekelezwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2a224431dd7f0ebae18971a9ebd67ca4.jpg

BAADHI ya wanaume katika Kijiji cha Ikondamoyo ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi