loader
Tucta: Ni ahueni kubwa nyongeza ya mshahara

Tucta: Ni ahueni kubwa nyongeza ya mshahara

S HIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafanyakazi kwa nyongeza ya mshahara aliyowapatia ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kupanda kwa asilimia 23.3.

Hayo yalibainishwa na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alipozungumza na HabariLEO jana baada ya Rais Samia kutangaza nyongeza hiyo ya mshahara. Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana ilisema Rais Samia ameridhia mapendekezo ya nyongeza ya mshahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyongeza hiyo imefanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP), mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa katika mwaka 2022/2023 na hali ya uchumi wa ndani na nje ya nchi. Taarifa hiyo ilisema mapendekezo hayo yaliyowasilishwa Ikulu ni mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alichofanya hivi karibuni mkoani Dodoma na kupokea taarifa ya wataalamu kuhusu nyongeza ya mishahara.

“Kutokana na hatua hiyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023, serikali imepanga kutumia Sh trilioni 9.7 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bajeti ya mishahara ya mwaka 2022/2023 ina ongezeko la Sh trilioni 1.6 sawa na asilimia 19.51 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022. Taarifa ilisema Rais Samia pia amepokea mapendekezo ya kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni kama Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lilivyoomba Mei Mosi mwaka huu.

Sambamba na hilo, Rais Samia pia aliridhia na kuielekeza wizara yenye dhamana na masuala ya hifadhi ya jamii kuendelea kushirikiana na TUCTA na Chama cha Waajiri nchini (ATE) ili kukamilisha taratibu za kuhakikisha malipo ya mkupuo ya asilimia 25 yaliyokataliwa na wadau mwaka 2018 yanapandishwa hadi asilimia 33.

Akimshukuru Rais Samia, Nyamhokya alisema nyongeza hiyo italeta ahueni kwa mfanyakazi na kwamba anaamini kuwa huo ni mwanzo tu kwa kuwa huko mbele wataendelea kumwomba Rais ili kiwango hicho kiendelee kupanda kulingana na mahitaji ya wakati. “Suala la nyongeza ya mishahara tumelipokea vizuri kwa sababu ni ahadi yake ya Mei Mosi aliposema tuna jambo letu na tuwape muda wakaone tutapanda mshahara kwa kiasi gani…

Tunamshukuru kwa kutujali wafanyakazi. Mwaka jana alipandisha madaraja na wengine mpaka leo wanaendelea kupanda madaraja,” alisema Nyamhokya. Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif alisema walimu waliielewa vizuri kauli ya Rais Samia aliyoitoa kwenye maadhimisho ya Mei Mosi kuhusu ahadi ya nyongeza ya mishahara na wanamshukuru kwa kuitimiza ahadi hiyo kwa kuridhia nyongeza ya asilimia 23.3 ya mishahara kwa watumishi.

“Baada ya kauli yako ya Mei Mosi, Rais, walimu tulikuelewa na tukasema tupo pamoja nawe, tunachapa kazi, kama uliweza kuwapandisha madaraja (vyeo) katika kipindi cha mwaka 2021/2022 pekee asilimia 92.9 ya walimu wote ambao ni takribani 260,000, hata hili la kuongeza mishahara tulijua tu litafanikiwa,” alisema.

Aliongeza: “Kama umetoa ajira kwa awamu nne, ya kwanza walimu 13,000, ya pili 7,000, ya tatu 6,000 na ya nne ni hii ya juzi 12,000 ambayo ni sawa na asilimia 15 ya walimu waliopo na kupandisha madaraja (vyeo) mwaka jana walimu 127,000 na mwaka huu zaidi ya 60,000, watakaonufaika na Daraja la Mserereko ni walimu 52,000 na jumla ya walionufaika na madaraja ni sawa na asilimia 92.9, hata hili la mishahara tulijua litakamilika tu.”

Wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika Dodoma, Rais Samia aliwahakikishia wafanyakazi kuwa jambo la nyongeza ya mishahara mwaka huu lipo kama alivyowaahidi mwaka jana. Alisema mahesabu yanaendelea ili kujua mishahara itapandishwa kwa kiasi gani na jana ameridhia nyongeza ya mishahara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba, alisema ongezeko hilo la mshahara ni kwa ajili ya sekta ya umma kwa kuwa serikali ndio inalipa mshahara. Kuhusu sekta binafsi, Ndomba alisema mchakato wa bodi ya kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi unaendelea na ATE ina wajumbe katika bodi hiyo, hivyo waajiri watashirikishwa ili kupata maoni yao kuhusu nyongeza ya mishahara.

Akifafanua kuhusu nyongeza katika sekta binafsi, Nyamhokya alisema kima cha mshahara kwa sekta hiyo kitatangazwa na waziri husika kwenye gazeti baada ya kupokea mapendekezo ya bodi. Alisema waziri mwenye dhamana aliwaahidi kuwa kabla ya watumishi wa umma hawajaanza kupokea mishahara hiyo, sekta binafsi nao watakuwa wameshapangiwa kiwango chao cha kima cha chini cha mshahara kulingana na sekta zao.

Baadhi ya wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii walimpongeza Rais Samia kwa nyongeza hiyo ya mshahara kwa watumishi wa umma. Miongoni mwa wananchi hao ni Oscar Kissanga, aliyempongeza Rais Samia kwa kuthamini na kujali maslahi ya wafanyakazi wakati Mwaki Nsubisikapula alisema ni miaka minane imepita bila mishahara kuongezwa, hivyo akamshukuru Rais kwa uamuzi huo.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/73b3a2bbf5dd43e99006abb1b6a0bd04.jpg

Rais Samia Suluhu Hassan, ametajwa kuwa miongoni ...

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

1 Comments

  • avatar
    Soterius Kamala
    15/05/2022

    Ahsante Raise wetu Kipenzi kwa kuwajali wafanyakazi. Mwenyezi Azidi kukupa nguvu uishi maisha marefu.

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi